Kifo cha Albert Eboisse na funzo kwetu

Kifo cha Albert Eboisse na funzo kwetu

Mphamvu

JF-Expert Member
Joined
Jan 28, 2011
Posts
10,702
Reaction score
3,350
Alber-624x350.jpg

Hatunae tena Albert Eboisse, huo ndio ukweli mchungu kwa washabiki wa Soka barani Afrika. Klabu ya JS Kabylie ilimpoteza mshambuliaji huyo raia wa Kameruni mwenye umri wa miaka 24 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Algeria kati yao na wapinzani wao wakubwa, USM Algiers.

Kifo cha mtu ambaye ni sehemu ya jamii ya soka ni jambo moja, lakini kifo hicho kinaposababishwa na kundi jingine kutoka kwenye jamii hii hii ya soka ni jambo lingine na linalosikitisha.

Eboisse alifariki kutokana na kupigwa kichwani na kitu kigumu ambacho kilirushwa kutoka jukwaani. Kwa maneno mengine ni kuwa mchezaji aliuwawa na washabiki, ambao wanadaiwa kuwa washabiki wa timu yake, JS Kabylie.

Vurugu katika mchezo wa Soka hazikuanza leo huko Afrika ya Kaskazini. Mwaka 2012 washabiki walipigana katika mechi ya Ligi Kuu Misri kati ya Al-Masry na Al Ahly, watu takriban 80 walifariki na makumi wengine kujeruhiwa.

Vurugu za Port Said, pamoja na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa wakati huo nchini Misri, zilipelekea Ligi ya Misri kusimama kwa karibu miaka miwili. Zilimfanya Mohamed Aboutreka atangaze kustaafu soka kwa muda na kocha wa wakati huo wa Ahly, Manuel Jose aliondoka nchini Misri.

Vurugu za aina hii ambazo zinasababishwa na mashabiki zimewahi kutokea pia katika nchi za Morroco, Kenya, Ivory Coast na Mali katika vipindi tofauti na zote zilisababishwa na mashabiki wakorofi wa soka.

Mchango wa washabiki katika mchezo wa soka ni mkubwa kwani wao ndio wateja wakubwa wa mchezo. Wao ndio hulipa viingilio kuingia uwanjani lakini pia ndio ambao hushangilia pindi timu inaposhinda na kuhuzunika timu inapofungwa.

Ni vigumu kuwatenganisha washabiki na mchezo, ndio maana sehemu ya adhabu za vurugu za mchezoni ni pamoja na kucheza bila mashabiki.

Hapa nyumbani vurugu katika viwanja vya soka zipo, ingawa hazijafikia hatua ya kuua wachezaji lakini kama hazitadhibitiwa huko ndiko tunakoelekea.

Novemba 2013 washabiki wasiojulikana walishambulia kwa mawe basi lililokuwa limewabeba wachezaji wa Yanga katika eneo la Kabuku mkoani Tanga wakati wakiwa njiani kwenda kucheza na Coastal Union mkoani Tanga.

Kilichodhaniwa kuwa ni majibu kilikuja kutokea baadae msimu msimu wa 2013/14 wakati basi la timu ya Coastal Union liliposhambuliwa nje ya Uwanja wa Taifa na mashabiki wa Yanga baada ya mechi ambayo iliisha kwa sare ya 1-1.

Mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu 2013/2014 washabiki wa Mbeya City walishambulia kwa mawe basi la timu ya Yanga na kumjeruhi dereva wa basi hilo kabla ya mchezo uliozikutanisha timu hizo nje ya uwanja wa Sokoine.

Uwanja wa Taifa kwa mara kadhaa umeshuhudia vurugu za kiwango cha kawaida, huku washabiki wa Simba na Yanga wakiwa na maeneo yao ya kudumu katika uwanja huo. Umiliki huo usio rasmi ambao wamejipa huwa unaendana na haki ya kumpiga mshabiki aliyevaa nguo ya wapinzani anapokatiza katika jukwaa lisilo lake na zaidi ya mara moja nimeshuhudia mashabiki wakipigwa, kuchaniwa nguo na udhalilishaji mwingine.

Matukio ya washabiki kupiga wachezaji si mengi sana katika Ligi Kuu, lakini ni mengi sana katika ligi za mchangani na mara kadha katika Ligi Kuu imetokea waamuzi kupigwa ama na washabiki au wachezaji wenyewe.

Tukio maarufu ya wachezaji kushambulia waamuzi ni yale ya wachezaji wa Yanga kumpiga mwamuzi Israel Mujuni katika mchezo ambao walifungwa goli 3-1 na Azam. Kibaya zaidi ni kuungwa na mkono na washabiki kwa kitendo kile ambacho hakikuwa cha kiungwana hata kidogo. Matokeo yalikuwa ni kufungiwa kwa wachezaji wanne wa Yanga pamoja na klabu kulipa faini.

Washabiki wa Simba na Yanga kwa nyakati fulani tofauti wamewahi kuvunja viti vya Uwanja wa Taifa ambao hutumika kama uwanja wao wa nyumbani katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Huko katika ligi za mchangani huonekana kama ni haki ya washabiki kumpiga refa wajkati anapofanya maamuzi kinyume na matakwa yao na hata timu fulani fulani husifika kwa ukorofi wao.

Mwamuzi Issa Salum Kipunje aliwahi kujizolea umaarufu mwaka 2013 kutokana na kuchezesha mechi za Ligi za KIFA-Chama cha Soka Kinondoni kutokana na kuchezesha mechi zake akiwa na panga na shoka kiunoni. Hali hii imetokana na kukosekana kwa usalama viwanjani, hali ambayo imetokana na ustaarabu ambao ndio kama sheria ya 18 katika soka letu.

Kuendelea kwa matukio haya si jambo la kistaarabu la linapingana na kanuni ya msingi ya FIFA inayohamasisha mchezo wa kiungwana maarufu kama 'Fair Play'.

Najiuliza maswali marahisi sana, wahusika wanangoja hadi mchezaji/mshabiki afariki ndio wachukue hatua kubwa dhidi ya hizi vurugu ndogondogo?

Vurugu za Port Said ziliuonesha ulimwengu kuwa Misri si sehemu salama kucheza soka na ligi ilifungwa kwa kipindi cha karibu miaka miwili. Novemba 2013 zikachezwa mechi mbili kubwa katika Jiji la Cairo, mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa kati ya Orlando Pirates na Al-Ahly tarehe 10 na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia kati ya Misri na Ghana tarehe 19 katika Uwanja wa Jeshi wa Cairo.

Pamoja na historia mbaya ya soka la Misri, mechi mbili kubwa barani Afrika zilichezwa mbele ya mashabiki katika mji uliokuwa bado ungali na vuguvugu la kisiasa na zikaisha kwa amani. Hii ni kumaanisha kuwa vurugu katika soka zinaweza kutulizwa kama tukiamua.

Vyombo vya dola vinao uwezo wa kudhibiti vurugu viwanjani lakini kwa uzembe fulani wamewapa washabiki haki ya kuamua nini wafanye wanachotaka hata kama wanaongozwa na mhemko na hisia.

Matukio ya kushambuiwa kwa basi la timu za Yanga na Coastal Union misimu iliyopita hayakuchukuliwa kwa uzito unaotakiwa, kulikuwa na makaripio mepesi na faini ambavyo vililenga tu kuonesha uwajibikaji na sio kutokomeza kabisa tatizo la vurugu mchezoni.

Kama tutaendelea kuwaendekeza washabiki wanaopiga waamuzi, kushambulia wenzao, kuvunja viti na kurusha vitu uwanjani hatuna muda mrefu kabla hatujasikia vifo vya mkupuo vya washabiki au wachezaji.

Albert Boisse apumzike mahala pema, ametuacha na tafakari juu ya tunakoelekea na kile ambacho Waingereza huita 'football hooliganism'

Soma zaidi:​Kifo cha Albert Eboisse na funzo kwetu | Fikra Pevu
 
Si jambo la kubeza hata kidogo.

Ufumbuzi ni kutibu maradhi yenyewe, sio dalili zake. Mwandishi ametutajia dalili za gonjwa linaloanza kusambaa kwa kasi.

Lakini chanzo ni nini? Upendeleo wa waziwazi wa marefa (mara nyengine ukiambatana na kauli za kejeli kwa wachezaji)? Matokeo yaliyopangwa mapema hivyo kutoupa nafasi uwezo wa timu inayokusudiwa kushindwa? Mgongano wa kimaslahi baina ya waamuzi/viongozi na timu iliyoko uwanjani? Maslahi madogo kwa wachezaji/waamuzi kiasi cha kukubali hongo ili wahujumu mchezo?

Ukosefu wa maadili kwa watendaji, unaowapa beji waamuzi dhaifu na kuwaacha wenye uwezo? Tofauti kubwa ya ushawishi (influence) unaozinyima imani ya kukata rufaa timu zinazohisi zimeonewa, hivyo kuchukua sheria mikononi? Vilabu kutokuwa na mfumo wa kudhibiti wanachama wao? Mashabiki kuhamasishwa kuzipa wakati mgumu timu zinazocheza ugenini kama mkakati mmojawapo wa 'uzalendo' kwa timu mwenyeji?

Walinzi viwanjani kugeuka kuwa watizamaji, hata baada ya mkasa wa shabiki kumvamia 'kishkaji' Kaka siku ya mechi ya Brazil? Vivutio vidogo kwenye ligi, vinavyoifanya timu isijute itakapoadhibiwa kwa kufanya fujo? Uhakika wa kusamehewa kwa walioadhibiwa hata kwa makosa hayo kila kiongozi mshikaji anapoingia madarakani?

Makundi ya wazi miongoni mwa viongozi, yayayotofautiana hata kwa mambo ya wazi, ukiwamo ukosefu wa nidhamu wa vilabu au viongozi? Dhana potofu kwamba ukorofi kwa mchezaji ama kiongozi ndio 'mpango mzima' hivyo kuendelea kuulea, kuuvumilia na kuutetea? Ushabiki wa wazi wa waandishi wa michezo, unaotetea, kusifia au kushajiisha ukorofi kwa upande wanaoushabikia?

Chanzo nini?
 
Kuna funzo kubwa hapa,kwa TFF,na washabiki wa kabumbu nchini..

Funzo kubwa hakika, wanasema mpumbavu hujifunza kwa makosa yake mwenyewe. Kwanini tusiwe wajanja kwa kujifunza kutokana na makosa ya wengine?
 
Back
Top Bottom