Kuna umhimu, kwa maoni yangu, kujua kwamba vikundi kama hivi Jukwaa la Katiba ni vipaza sauti vya nani? Mimi nimepata kuwafuatlia kwa karibu Jukwaa la Katiba. Tamko lao walilolitoa kabla ya mjadala Bungeni juu ya Mswaada wa Tume ya Katiba haujaanza, ni kwamba kama wabunge wataafiki kwamba Mkatba usomwe mara ya pili Jukwaa litawashawishi watu wafanye maandamano Tanzania nzima. Na kabla ya maandamano wangejipa mwezi mmoja kupita Tanzania nzima kuwashawishi watu juu ya maandamano. Tofauti na walichokisema mbele ya watu, mara baada ya Mswaada kusomwa mara ya pili na kupitishwa, Jukwaa la Katiba likaja na kauli mpya kwamba maandamano ya taifa zima yanafanyika Jumamosi, siku chache baada ya mswaada kusomwa mara ya pili. Hii inatia wasiwasi na umakini wa kauli zao.
Sasa baada ya Jukwaa la Katiba kutoa matamko hayo ya kutisha (kwa maoni yangu) zimezuka tena taasisi mbalimbali nyingine zinafahamika na zingine hazifahamiki zinazotaka kufanya maandamano nchi nzima kwa sababu tofauti. Kama kila taasisi, kila mtu, kila kikundi kitakuwa na haki ya kuhamasisha wananchi kufanya maandamano nchi nzima kulishinikiza Bunge, Mahakama au Raisi kufanya wananchokitaka tutaweza kuishi kwa amani na kuheshimiana kweli? Tutaweza kuishi katika mazingira ya ustaarabu wa utawala wa sheria? Nionavyo mimi sisi kama watanzania ambao tunapaswa tutafakari kwa pamoja na kuwa makini juu ya tunayoyafanya. Siasa zikizidi sana ni matatizo. Kila mtu anayejua kusema siasa akiruhusiwa kuwahamasisha watu kuandamana kwa lengo la mashinikizo kwa vyombo vya dola kufanya anachotaka itakuwa ni mtafaruku.
Ndio maana ndugu zetu wa Chadema baada ya kutafakari kwa kina wameona busara kuunda kamati ya watu wenye busara na upeo wa juu kwenda kumuona Raisi na kumpa kwa kina maoni ya Chadema kuhusiana na Tume ya Uchaguzi. Wameenda kumuona Raisi sio kama kiongozi wa juu wa CCM bali kiongozi Mkuu wa Dola.