Kiangi: Elimu yetu ya sasa si ile ya miaka ya 1980 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kiangi: Elimu yetu ya sasa si ile ya miaka ya 1980

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Dec 22, 2010.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Dec 22, 2010
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  NCHI ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyotia saini Mkataba wa Elimu Kwa Wote (EFA) wa mwaka 1990.
  Mkataba huu ulikuwa na takribani malengo sita ikiwemo kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015, watoto wote na hasa wa kike wanaoishi katika mazingira magumu wanapata elimu ya msingi iliyo bora na itakayowawezesha kumudu kuishi katika mazingira yanayo wazunguka.

  Malengo mengine ya mkataba yalikuwa kupunguza kwa asilimia 50 kiwango cha watu wasiojua kusoma, hasa wanawake ifikapo mwaka 2015, kujenga uwezo sawa wa kujiendeleza katika elimu kwa wananchi wote na kuhakikisha kuwa ubaguzi wa kupata elimu kwa wanawake unakuwa historia ifikapo mwaka 2025.


  Aidha, mkataba ulizitaka nchi husika kutenga asilimia 20 ya bajeti katika sekta ya elimu na kuhakikisha kuwa, ubora wa elimu inayotolewa, unapimwa kwa matunda yatokanayo na elimu yenyewe.
  Miaka 20 baada ya Tanzania kukubali malengo haya, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Action Aid Tanzania, Aida Kiangi anasema bado Tanzania ina changamoto kubwa kutimiza kikamilifu malengo hayo.
  Kwa mfano, anasema wakati nchi hizo zikitakiwa kutenga asilimia 20 ya bajeti yake katika sekta ya elimu, mpaka sasa Tanzania inatenga asilimia 18.3.

  Anaongeza kuwa hata nchi wahisani zimeshindwa kutimiza ahadi zake za kuchangia sekta ya elimu kama zinavyotakiwa na mikataba mbalimbali, hali inayosababisha upungufu wa rasilimali fedha kuendelea kuiandama sekta hii.
  “Lakini kibaya zaidi, hizo hizo fedha chache zinazotengwa na serikali kusaidia sekta ya elimu, nyingi zinafujwa na watu wasiokuwa waaminifu. Kuna vitendo vingi vya rushwa katika sekta hii,” anabainisha na kuilaumu serikali kwa kuelekeza zaidi fedha za bajeti ya elimu katika mambo yasiyo na umuhimu katika sekta hiyo.

  Analia na ufujaji wa fedha katika sekta ya elimu akitoa mfano wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2007/08, iliyoonyesha upotevu wa fedha za serikali kuongezeka kutoka Sh2.4 bilioni mwaka 2006/07 mpaka kufikia Sh3.6 mwaka 2007/08, ikiwa ni ongezeko la asilimia 52.

  Kwa Kiangi, bado Tanzania ina safari ndefu kufikia utoaji wa elimu bora. Anasema kiwango cha elimu cha sasa hakilingani na kile cha miaka ya 1980, akitoa mfano wa ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika kama kiashiria cha hali hiyo. Mwaka 1980 asilimia ya watu walioshindwa kusoma na kuandika ilikuwa 10 lakini sasa ni asilimia 32.
  “Katika hali ya kawaida tu, ubovu wa elimu wanayopata watoto wetu, unaonekana wazi kwa kuangalia ongezeko la idadi ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika,” anafafanua.

  Kiashiria kingine ni ongezeko la watoto wanaohitimu elimu ya msingi huku wakikosa stadi muhimu za kusoma, kuandika na kuhesabu.
  Sababu nyingine ni upungufu wa walimu ambapo, licha ya umuhimu wao katika maendeleo ya elimu, pengo lao nchini ni kubwa. Anasema walimu wanaohitajika ni 110,000, lakini serikali kwa mwaka imekuwa ikisomesha walimu 36,000, ambao pia siyo wote wanaokwenda kufundisha.

  Tatizo la ubora wa elimu ni suala la mfumo ambao anasema bado haujatengemaa. Mathalani, huu ndio mfumo ulioruhusu matumizi ya lugha mbili za kufundishia katika daraja la elimu ya msingi.
  Wakati shule za serikali zikitumia Kiswahili, shule za watu au taasisi binafsi zimekuwa zikitumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia.

  “Mkanganyiko huu wa lugha za kufundishia katika shule za msingi, kunafanya kusiwe na usawa katika elimu wanayopata watoto, na ukweli huu huonekana pale wanapofika shule za sekondari,” anaeleza.
  Anasema katika shule za sekondari, watoto wanaotoka shule za msingi za serikali hususan zilizopo vijijini wanapata tabu zaidi katika kuelewa wanachofundishwa.

  Hawa wanalazimika kutumia nguvu kubwa kujifunza Kiingereza badala ya masomo ya kawaida, mwishoni hujikuta wakifanya vibaya katika mitihani.
  Anashauri kuwepo na mwafaka wa kitaifa kuhusu matumizi ya lugha ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari huku serikali ikifuatilia kwa karibu mitalaa inayotumika katika shule mbalimbali nchini.
  “Mambo hayo yanatakiwa yawekwe wazi na serikali katika sera ya elimu. Pia iyaeleze katika usajili na taratibu za uendeshaji wa shule binafsi na taasisi nyingine za elimu,” anasema.

  Kuhusu ongezeko la wanafunzi wa kike wanaipata mimba shuleni. Kiangi pamoja na mambo mengine anaishukia serikali kwa kuwa na sera ya elimu inayowazuia wasichana waliopata ujauzito kuendelea na masomo.

  “Jambo la msingi hapa ni kuwa, mimba zinachangia asilimia 4.5 ya wanafunzi wanaoacha shule. Wengi wao ni wale wanaotoka shule za vijijini, wamekuwa wakishindwa kurudi shuleni kama wanafunzi wa kawaida wakisha jifungua kutokana na sheria zilizopo,” anaeleza.

  Kwa kuwa sekta ya elimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi, anashauri serikali kuendesha mjadala wa kitaifa utakaosaidia pamoja na mambo mengine kupata malengo na dira ya elimu kwa miaka ijayo.
   
Loading...