Kiama kwa wagombea

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
*Tendwa kutangaza orodha ya waliotoa rushwa Julai
*Asema jina likitajwa chama kisimteue, vinginevyo…
tendwa_thumb.jpg

*Ataja wabunge walioanza kulalamika, dawa yapikwa
Na Maregesi Paul
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, itawataja kwa majina, wanasiasa wanaopita majimboni na kutoa rushwa kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kushinda wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa, alipofungua semina ya siku mbili ya wadau wa siasa nchini iliyoandaliwa na Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD).
“Mikakati ya kampeni zenu wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu lazima iwe mizuri, isiwe ya rushwa kama ile iliyotumika katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005.
“Nakumbuka mwaka fulani rafiki yangu Musa Nkangaa alikwenda kugombea ubunge huko Singida akipambana na huyu jamaa Mohamed Enterprises.
“Baada ya kampeni kuanza, akashangaa mwenzake anamwaga pesa, akaja kunilalamikia akasema mwenzagu anatembea na viroba vya pesa, anagawa pesa kwa kila mtu, kwa hiyo, nimeshindwa kukabiliana naye.
“Kwa hiyo, safari hii mikakati yenu ya kampeni iwe mizuri vinginevyo mtaharibikiwa kwa sababu baada ya Bunge la Bajeti kuahirishwa Julai mwaka huu, tutawataja kwa majina wale wote waliotuhumiwa kwa rushwa majimboni na wale waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya rushwa.
“Lazima tutafanya hivyo kwa sababu lengo letu ni kuvifanya vyama vya siasa viwajue watu hao, vijue hawana sifa za kugombea na kuongoza ili wawaache wakati wa ‘nomination’ (uteuzi),” alisema Tendwa.
“Kampeni zitakapoanza lugha za kampeni ziwe za kiungwana, matusi, kejeli vitendo vya baadhi ya wafuasi wa chama fulani kumvalisha mbwa bendera au tisheti za chama fulani, viacheni kwa sababu huo ni ukiukwaji wa sheria za uchaguzi,” alisema Tendwa.
Katika mazungumzo yake, Tendwa alimtolea mfano Mbunge wa Lulindi, Suleiman Kumchaya na kusema mbunge huyo juzi alifikisha ofisini kwake malalamiko ya vitendo vya rushwa vinavyofanyika jimboni mwake.
“Jana mbunge mmoja anaitwa Kumchaya (Suleiman) alileta malalamiko ya ‘page’ (kurasa) nane ofisini kwangu akilalamikia vitendo vya rushwa vinavyofanyika jimboni mwake kuelekea uchaguzi mkuu.
“Katika malalamiko yake, anasema kuna mtu jimboni humo anagawa baiskeli pamoja na vitenge vyenye picha yake.
“Baada ya kupokea malalamiko hayo, jana hiyo hiyo niliwasiliana na wahusika na hivi sasa suala hilo linafanyiwa kazi ili tuone ukweli wake,” alisema.
Kwa mujibu wa msajili huyo wa vyama vya siasa, ofisi yake inaendelea kupokea malalamiko ya vitendo vya rushwa vinavyotokea katika maeneo mbalimbali nchini na kuzifanyia kazi taarifa hizo.
Mbali na hayo, Tendwa alizungumzia usajili wa kudumu wa Chama cha Jamii (CCJ) na kusema uhakiki wa chama hicho umeanza rasmi jana.
“Uhakiki wa CCJ umeanza leo (jana), kama wakikidhi vigezo vinavyotakiwa kama nyinyi mlioko hapa, tutawapa usajili wa kudumu kama kawaida.
“Mimi sina mtimanyongo nao, wasilalamike, ninapenda vyama viwe vingi kwa sababu vilivyopo sasa ni 18, hivi ni vichache ukilinganisha na nchi nyingine duniani.
“South Afrika kuna watu milioni 50, vyama vya siasa ni 150, vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka jana ni vyama 46, lakini sisi hapa tunavyo 18 tu kama nilivyosema,” alisema.
Mkutano huo unalenga kuwakutanisha wanasiasa kuelimishana juu ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, pamoja na masuala mengine yanayohusiana na uchaguzi.



Kiama kwa wagombea
 
Back
Top Bottom