GE2025 Kesi ya wachokonozi yaahirishwa tena mpaka Agosti 19, 2025

GE2025 Kesi ya wachokonozi yaahirishwa tena mpaka Agosti 19, 2025

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Just Pray

JF-Expert Member
Joined
Nov 7, 2023
Posts
2,142
Reaction score
4,779
Kesi ya jinai inayowakabili wamiliki wa jukwaa la mtandaoni la Wachokonozi, Jackson Kabalo na Joseph Mrindoko, imeahirishwa kwa mara nyingine tena katika Mahakama ya Wilaya ya Meru na sasa itasikilizwa Agosti 19, 2025 kwa ajili ya hoja za awali.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili- kuchapisha taarifa za uongo kinyume na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, na kutoa maudhui mtandaoni bila leseni kinyume na Kifungu cha 116(3)(b) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 marejeo ya mwaka 2020.

Awali, Juni 27, 2025, walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ambapo walikana mashtaka yote mawili na kuachiwa kwa dhamana. Kesi hiyo ilipangwa kuendelea Julai 21, 2025, lakini upande wa Jamhuri ulidai kutokuwa tayari kuwasilisha hoja za awali, jambo lililopelekea Mahakama kuwaachia huru washitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Mara baada ya kuachiwa huru, walikamatwa tena na kupelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Meru ambapo walipelekwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Sodeyeka, na kusomewa upya mashtaka hayo hayo. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, hakimu aliagiza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi kabla ya Agosti 13, 2025, siku ambayo shauri hilo lingepangiwa kusikilizwa.

Hata hivyo, leo kesi hiyo imeshindwa kuendelea baada ya Wakili wa Serikali kudaiwa kupata msiba na kushindwa kufika mahakamani. Hakimu Sodeyeka amesisitiza kuwa endapo upande wa Jamhuri hautakuwa tayari siku ya kutajwa tena, atafutilia mbali shauri hilo.

Washitakiwa wanaendelea kuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya wadhamini wawili kila mmoja, kwa dhamana ya maneno yenye thamani ya shilingi milioni tatu.

Washitakiwa wanatetewa na mawakili Ally Mhyellah na Simon Mbwambo kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).


 
Back
Top Bottom