Kesi tano za mabilioni Uswisi zachunguzwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,450
33,359
sitta.gif

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta akiwa na Meya wa Jiji la Boston, Martin Walsh's alipomtembelea Marekani hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi ya kujifunza mbinu mbalimbali zinazoingizia jiji hilo mapato.

Dar es Salaam. Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.

Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.

Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na kubaini kuanza kwa uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba zinatokana na vitendo vya rushwa.

Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema: "Tuna makubaliano na Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji wa fedha, hivyo tuko katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano ya moja kwa moja kwa sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa katika utoaji wa taarifa."

Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.

"Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini kutokana na uwezo wao mdogo tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema tunazo kesi tano hivi… ni kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu masuala ya fedha. Hatuwezi kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa na mkataba wetu na taasisi tunazofanya nazo kazi."

Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema wanaochunguzwa katika kesi hizo wanahusishwa na kampuni hewa zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha kisha kwenda kuzificha nje ya nchi.

"Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa wakipokea rushwa au wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni kivuli na ushirika mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda kwenye kampuni fulani kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na wafanyabiashara kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha," alisema.

Jaji Werema

Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini akakataa katakata kutaja watu wala kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.

"Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili, tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.

"Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu kwa utaratibu ili tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani tumekaa kimya hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika mtaona na mtasikia."

Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema watu au taasisi zilizoweka fedha nchini humo hawawezi kutajwa kwani ulinzi wa faragha za watu ni suala la kimataifa... "Sizungumzii tu akaunti za Tanzania, suala la kulinda faragha za watu ni la kimataifa. Ukiwa raia wa Uingereza, Ufaransa au Tanzania, huwezi kupata taarifa za maisha ya mtu binafsi. Kwa sababu wewe kama ni raia mwema, una haki ya kuwa na faragha yako."

Taarifa za 2011 kutoka Uswisi zilionyesha kuwa kuna kiasi cha Sh327.9 bilioni zilizofichwa kwenye benki za nchi hiyo, lakini Ripoti mpya ya mwaka 2012 ya Benki za Uswisi inaonyesha kuwa fedha hizo zimepungua hadi Sh291.96 bilioni.

Akizungumzia kupungua kwa fedha hizo, Balozi Chave alisema: "Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za nchi nyingine."

Taarifa ya Global Financial Integrity ya 2013 inaonyesha kuwa utoroshaji haramu wa fedha kutoka Tanzania kati ya 2008 na 2011 umefikia jumla ya Dola za Marekani 2.935 bilioni (Sh4.2 trilioni) na inakadiriwa kuwa Watanzania wanamiliki utajiri wa Dola za Marekani 750 milioni (Sh1.23 trilioni) katika Visiwa vya Jersey.

Muda wa uchunguzi

Wakati Tanzania ikiwa imepeleka kesi hizo mbele ya taasisi hizo ndani ya mwaka mmoja, Zinkernagel alisema zinaweza kuchukua miaka mitano hadi 10 ili kufanikisha kurejesha fedha zilizofichwa.

"Tangu uchunguzi unaanza hadi fedha zirudishwe kwa nchi husika inaweza kuchukua hadi miaka 10. Sisi hatuna muda mrefu tangu tuanzishe taasisi hii, lakini tunafahamu baadhi ya kesi zimechukua hadi miaka 20. Hizi ni kesi za kimataifa, hivyo unaanza kufuatilia akaunti na mifumo ya taasisi nyingine… hiyo tu inaweza kuchukua hata miezi sita. Bado mtuhumiwa anaweza kukata rufaa. Ni kweli unataka mambo yaende haraka lakini pia huwezi kukiuka utawala wa sheria."

Mbali na Tanzania, Zinkernagel alisema taasisi yake pia inashughulikia kesi za nchi nyingine 12 duniani na kwamba wamefanikiwa kukamata baadhi ya fedha na mali zilizoibwa katika baadhi ya nchi.

Alisema kazi hizo hufanywa bila malipo yoyote kwa kuwa taasisi hiyo hupata fedha kutoka serikali za Uswisi na Uingereza.

Changamoto

Akieleza changamoto zilizopo katika kupambana na uhalifu wa fedha haramu, Zinkernagel alisema ni ushirikiano hafifu kati ya nchi zinazoibiwa fedha na zile zinazoficha.

"Mamlaka za Uswisi zikigundua kuwapo kwa mali labda kama za Tanzania, wanaweza kuanzisha uchunguzi wao lakini ili kuhusisha uchunguzi na nchi husika watahitaji msaada kutoka nchi husika. Mamlaka ya Uswisi haiwezi kuendeleza kesi bila ushirikiano na mamlaka za Tanzania, kwa mfano. Hapo ndipo tunapokumbana na siasa nyingi pale tunaposhughulikia kesi kama hizo. Inakuwa vigumu kupata ushirikiano wa wanasiasa tunapouhitaji, hiyo ni changamoto kubwa.

"Changamoto nyingine, ni uwezo mdogo wa vyombo vya usalama vya Tanzania wa kushughulikia kesi za rushwa, matumizi mabaya ya fedha na madaraka. Ni kazi ngumu kufuatilia kesi kama hizo kwani unahitaji kuhusisha sekta mbalimbali. Changamoto hiyo ya utaalamu pia inaigusa Tanzania ndiyo maana haina uwezo wa kuchunguza kesi kama hizo."

Kwa upande wa nchi zinazoficha fedha, Zinkernagel alisema kuna tatizo la kutoweka vikwazo kwa taasisi za fedha zinazotuhumiwa kuhifadhi fedha haramu.

Tanzania imetajwa kuwa nchi ya 13 kati 20 duniani kwa utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.

Taarifa zilizopatikana kutoka katika mitandao mbalimbali ikiwamo Global Financial Integrity, Carl Smith, One Dola Bilioni na Taarifa ya Swiss," zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na biashara haramu ya uhamishaji wa fedha na misamaha ya kodi na mikataba mibovu.

Chanzo;Mwananchi


 
Yalijadiliwa hadi Bungeni. Serikali ikaahidi kuyafuatilia. Habari za mwisho kuhusu mabilioni haya ni zipi?

Aione: Zitto
 
Last edited by a moderator:
Zitto aliyekuja na hiyo hoja alikiri MBELE YA KIAPO kwa Mwanasheria mkuu Werema kuwa hajui jina hata moja la mtu mwenye fedha huko Uswisi...

Sasa hivi Zitto yuko busy kutuletea chama kipya cha ACT Tanzania, muacheni kwanza amalize assignment ya sasa.
 
Sasa alianzisha mgogoro wa nini na wenye chao? Sasa ndio amekaa kimya labda hela hizohizo ndio wanammegea kuanzisha chama? Nchi hii kwa kweli ni akili kichwani tu kwa kwenda mbele!
 
Zitto aliyekuja na hiyo hoja alikiri MBELE YA KIAPO kwa Mwanasheria mkuu Werema kuwa hajui jina hata moja la mtu mwenye fedha huko Uswisi...

Sasa hivi Zitto yuko busy kutuletea chama kipya cha ACT Tanzania, muacheni kwanza amalize assignment ya sasa.

Tangu Werema aseme vile,ukimya umetawala sana
 
Back
Top Bottom