Kemikali hatari zinavyouzwa mitaani Mara

Kemikali hatari zinavyouzwa mitaani Mara

figganigga

Platinum Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
27,912
Reaction score
63,601
Serengeti. Ni kama sheria hazipo ama wasimamizi wa sheria husika wamelala, kwani kemikali hatari aina ya mekyuri inauzwa bila udhibiti wala tahadhari za kitaalamu katika migodi ya wachimbaji wadogo, wilayani Serengeti, Mara.
Mekyuri ama kwa jina la Kiswahili, zebaki ni kemikali ambayo imepigwa marufuku na Serikali kuingizwa nchini, lakini zuio hili ni kama halipo kwani inaingizwa nchini na wamachinga na wanunuzi wa dhahabu katika migodi hiyo midogo.

Gazeti hili lilithibitisha kemikali aina ya mekyuri inauzwa katika vijiji vya Majimoto na Park-Nyigoti wilayani Serengeti, ambako tayari wananchi wana hofu ya kuathiriwa na kemikali zinazotumika kwa ajili ya kusafishia dhahabu.

Baadhi ya wachimbaji wa dhahabu katika migodi iliyopo kwenye vijiji hivyo, wamethibitisha kuwapo kwa biashara hiyo na kwamba kemikali ya mekyuri hutunzwa kwenye chupa za dawa za binadamu na mifugo. "Wakati wa mfumko wa dhahabu kemikali hiyo huwa nyingi sana na inasemekana inatokea nchini Kenya kwa kupitia mpaka wa Sirari….kipindi hicho wamachinga hutembeza kama wanavyouza sumu ya panya na

bidhaa zingine," anasema mmoja wa wachimbaji wa dhahabu huku akiomba kuhifadhiwa jina lake.

Anasema mekyuri hupimiwa kwa mifuniko ya chupa za dawa za binadamu zenye vipimo. "Mifuniko yenye alama za vipimo (milligram)hutumika kama vipimo na tunainunua kati ya Sh20,000 - 30,000 na wakati mwingine huwa zaidi ya hapo hupimwa bila tahadhari yoyote kwa kuwa hata sisi tunatumia bila kuvaa mipira (gloves)," anasema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Majimoto, Johannes Masirori anakiri kuzagaa kwa kemikali hizo na kwamba zinaingizwa kwa wingi kutoka Kenya kupitia Nyamongo. "Hakuna elimu inayotolewa kwa watumiaji wake ili kuwaepusha na madhara kwao na kwa watu wengine kwa sababu kemikali hizo zinaweza kuwa zinaingia kwenye vyanzo vya maji," anasema Masisori na kuongeza:

"Kama Serikali imepiga marufuku na haiingizi kemikali hii mbona imezagaa na hakuna hatua zinachukuliwa? wamachinga wanatembeza kemikali kama ilivyo sabuni…kama hakutakuwa na usimamizi mzuri tutegemee madhara makubwa kwa viumbe hai".

Uchunguzi katika machimbo ya dhahabu ya Park-Nyigoti ambako kuna migodi zaidi ya mitatu ya wachimbaji wadogo, wahusika wanadai kwamba wanapata kemikali hiyo kwa wingi kutoka kwa wauzaji wa Mwanza ambao pia wanasema wanaipata kwa wingi kutoka jijini Dar es Salaam.

Raphael Mwera ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Park-Nyigoti anasema kemikali hiyo inaingia na kutumiwa bila tahadhari na watu wako hatarini kupata madhara kwa kuwa hakuna ufuatiliaji au ushauri wowote wa watalaam.

"Hapa wanapima kwa kutumia vipimo vya soda, mfuniko mmoja huuzwa kati ya Sh40,000 na 60,000 kulingana na hitaji kwa wakati huo, kuna wakati mekyuri hukosekana na kusababisha kusimama kwa baadhi ya kazi za usafishaji wa dhahabu, kwahiyo soko lake ni kubwa,"anasema Mwera.

Anashuhudia kuwa kuna mnunuzi ambaye aliwahi kufariki dunia kutokana na kemikali hiyo, lakini taarifa nyingine zikadai kwamba alifariki dunia kutokana na kifua kikuu kutokana na moshi mkali uliotokana shughuli zake za uchomaji wa dhahabu.

Mkemia: Mekyuri ni hatari

Uchunguzi unaonyesha kuwa wachimbaji wadogo hufanya kazi za kusafisha mchanga wa dhahabu kwa kutumia mekyuri karibu na vyanzo vya maji, hali ambayo ni miongoni mwa vyanzo vya uchafuzi wa mazingira na kusababisha madhara kiafya kama inavyobainishwa kwenye sera ya afya ya 2007.

Sera hiyo inaweka wazi kwamba magonjwa mengi yanayoathiri afya ya jamii yanatokana na uduni na uchafuzi wa mazingira, suala ambalo lipo chini ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake, wakala huyo unawajibika kusimamia huduma za uchunguzi wa sampuli za bidhaa za viwandani na mashambani.

Kadhalika wakala huyo unatakiwa kuimarisha uchunguzi wa kemikali, maji, maji taka, udhibiti wa kemikali na tafiti ili kulinda afya za wananchi, mazingira na kusaidia vyombo vya dola kufikia uamuzi sahihi na kutoa haki.

Sera ya afya inasema uchunguzi wa sampuli na udhibiti wa kemikali utafanywa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kulingana na sheria iliyounda wakala kwa kuzingatia sheria, miongozo na kanuni zinazoelekeza na kusimamia utoaji wa matokeo ya uchunguzi .

Hata hivyo, Mkemia wa Serikali Kanda ya Ziwa, Christopher Anyango anasema kemikali hiyo inayotumiwa na wachimbaji wadogo kusafishia dhahabu ni hatari kwa maisha ya viumbe hai na madhara yake ni makubwa na matokeo huonekana baadaye.

"Watu wako hatarini sana kwa kuwa kuna kemikali mbili hatari kwa maisha ya viumbe hai kama Cyanide na Zebaki…hizi kemikali zinatumiwa sana migodini na wachimbaji wadogo, ina madhara makubwa sana,"anasema Anyango na kuongeza:

"Mekyuri ni mbaya na wachimbaji wadogo wanaitumia bila kuchukua tahadhari, madhara yake yanamgusa anayeitumia kusafisha, ikiingia kwenye maji huleta madhara kwa watumiaji wa maji hayo, samaki wakinywa maji anakula anapata madhara …maana huingia kwenye neva za mwili na kusababisha usifanye kazi sawasawa".

Anyango anasema kuwa madhara yanayosababishwa na kemikali hiyo huchukua muda mrefu kuonekana, ikiwemo magonjwa ya kansa, mwili kutokufanya kazi sawasawa, kutetemeka, magonjwa ya ngozi na mwisho wake huwa ni mauti.

Mkemia huyo anasema kutokana na madhara yake, nchi nyingi duniani zimepiga marufuku matumizi yake. "Ni suala la kimataifa maana hiyo kemikali ikichemka, hewa yake husafiri Kilometa 300 hewani, ndiyo maana Ulimwengu unapiga kelele sana kwa kuwa ni hatari,"anabainisha.

Serikali imeshindwa

Wakati kemikali hiyo inazagaa na madhara yake yanajulikana, Serikali inakiri kushindwa kuzuia matumizi na kusambaa kwake kwa kuwa hakuna njia mbadala ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wanaotumia zebaki.

"Wachimbaji wadogo ni kundi kubwa sana ambalo limekuwepo kwa miaka mingi…kuzuia matumizi ya kemikali hiyo bila kuwapa njia mbadala utaleta mgogoro mkubwa na kundi hili….ndiyo maana tunashindwa kuzuia licha ya kutambua madhara ya kiafya kwa viumbe hai, tunajitahidi kuwaelimisha," Anyango.

Anyango anakiri kwamba ofisi yake ilianza kufanya ufuatiliaji kuhusu suala hilo baada ya kuulizwa na gazeti hili. "Ulituzindua wewe ulipoanza kufuatilia, tumefanya ukaguzi kwenye migodi hii midogo na tayari ripoti tumeishapeleka ofisi ya Mkemia Mkuu, ikiwa tayari utafahamishwa na hatua zitakazochukuliwa," anasema.

Wakati hayo yakiendelea, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekuwa likifanya uchunguzi kwenye migodi mikubwa zaidi, wakati migodi midogo inachangia madhara makubwa ya mazingira kwa kuwa wawekezaji hao wengi wao huajiri wafanyakazi wasiokuwa na sifa kwa kuwalipa ujira mdogo.

Agosti 2013 wataalamu wa NEMC walifanya uchunguzi kwenye migodi mikubwa tisa na kubaini migodi sita kukiuka Sera ya Mazingira ya 1977 na Sheria ya Mazingira namba 20 ya 2004 na kuwapiga faini ya Sh450 milioni.

Taarifa za afya

Mganga Mfawidhi kituo cha afya, Iramba katika Wilaya ya Serengeti, Stephen Maiga anakiri kuwepo kwa wagonjwa wengi wa kifua kikuu na mambukizi ya Virusi vya Ukimwi, magonjwa ya ngono, na magonjwa ya ngozi.

"Wagonjwa wanatoka maeneo tofauti maana hapa ni kituo cha afya, lakini hali si nzuri kwa magonjwa hayo hasa maambikizi,"anasema Maiga.

Muuguzi katika Zahanati ya Majimoto, Sophia Nyamwino anakiri eneo hilo kuwepo kwa magonjwa mengi ya ngozi, kikohozi, minyoo na malaria.

"Magonjwa mengi hapa ni Malaria, UTI…magonjwa ya kikohozi, minyoo ni mingi, ugonjwa wa ngozi (Ukurutu) ni tatizo kubwa …lakini pia kuna maambukizi mengi ya magonjwa ya ngono na Virusi vya Ukimwi, nadhani ni kwa sababu ya muingiliano na shughuli wafanyazo wakazi wa maeneo haya," anasema.

Anasema hawajajua sababu kubwa ya magonjwa ya ngozi na kikohozi yanachangiwa na shughuli za uchimbaji ama maji, hivyo inakuwa vigumu kuyahusisha na maji hayo, mpaka uchunguzi wa kina na katika vituo vikubwa ufanyike.

"Kwa kuwa kuna Maambukizi ya magonjwa ya ngono na Virusi vya Ukimwi yako juu…wagonjwa wa Tb nao ni wengi nawatuma kwenda ngazi za juu,maana hapa hatuna vipimo zaidi na sijui kama wanaenda ama la,"anasema. Mia

Chanzo
:Mwananchi
 
Back
Top Bottom