Katika kukabili uhaba wa dola na mfumuko wa bei, tuanzie hapa

Ndimbo M

Member
Aug 30, 2023
13
62
Wadau,

Nafikiri wengi tunakubaliana kwamba kukuza uchumi ni njia rahisi ya kuepuka tatizo la uhaba wa dollar na mfumuko wa bei unaoambatana nao.

Hapa nitaeleza eneo moja la kisiasa kiutendaji lakini lenye athari kubwa sana kiuchumi kwa Tanzania...,eneo la viongozi wa mikoa.

Kama ilivyokuwa kwa DC wakati wa ukoloni, ndivyo hata leo, kiongozi wa wilaya au mkoa, anaweka umakini katika kumtumikia aliyemteua kisiasa badala ya kuwaza kulikuza eneo analoliongoza kiuchumi. Hali hiyo imefanya Tanzania kushindwa kutumia fursa ya ukubwa wa eneo lake zuri la kijiografia katika kukuza uchumi wake.

Wanaoteuliwa kuongoza mikoa wala siyo wabunifu wanaoweza kusoma eneo lao na kuishawishi Serikali Kuu iwezeshe miradi ya kiuchumi watakayoibuni na kuanzisha katika maeneo yao,..na ndo maana ilikuwa siyo ajabu hasa wakati wa Magufuli madarakani, kusikia kwamba fedha za mendeleo zilizotengwa kwa mkoa fulani, hazikutumika na kurudishwa hazina. Kwa kukosa ubunifu waliona zile fedha bora zikae tu zisifanye kazi.

Tanzania yenye km za mraba 945,000 na pato la taifa, GDP, kiasi cha $75 bilioni inaizidi Rwanda kiuchumi yenye km za mraba 26,000, na GDP kiasi cha $13 bilioni.

Lakini tukizingatia uwiano wa maeneo yao kijiografia na matumizi yake kiuchumi, Rwanda inaizidi Tanzania.
Iko hivi, Tanzania ina mikoa 31. Sasa tukichukua GDP yake ya $75 bilioni na kuigawa kwa mikoa yake hiyo unapata wastani kila mkoa una pato la $2.4 bilioni.

Hiyo ina maana mkoa mpya wa Songwe wenye eneo sawa kabisa na Rwanda,..km² 26,000, una pato la $2.4 bilioni. Vilevile, Tabora yenye ukubwa wa km² 76,150,..eneo ambalo ni sawa na ukubwa wa nchi za Burundi, Rwanda, Swaziland, Seychelles na Comoro kwa pamoja lakini inapitwa kwa mbali kwa kipato na Seychelles yenye pato la $14 bilioni na Rwanda yenye $13 bilioni.

Hiyo ina maana endapo Tabora na mikoa mingine 25 tu kati ya hiyo 31 ingeingiza pato la mwaka kama Rwanda kila mkoa, Tanzania ingekuwa na pato la kiasi cha $325 bilioni kwa mwaka. Lakini hata kama hii mikoa kila moja ingeingiza pato sawa na Seychelles au Rwanda,bado tutajiuliza kwa nini iwe hivyo ukichukulia ukweli kwamba mkoa wa Morogoro,mathalan, wenye ukubwa wa km² 70,000, unaizidi Seychelles kieneo mara 155.

Tanzania ina hali ya hewa inayowezesha kukuza mazao ya aina mbalimbali. Kama kungekuwa na viongozi wabunifu,wenye kuweka mkazo katika kukuza uchumi kwa kushirikisha wananchi wa maeneo husika, leo hii Tanzania ingekuwa mbali sana kiuchumi na kusingekuwepo hii habari ya uhaba wa dollar na mfumko wa bei.
Mathalan, Tanzania inatumia mamilioni ya dollar kwa mwaka kuagiza mafuta ya kupikia kwa vile mafuta yanayozalishwa ndani hayatoshelezi wakati mazao ya alizeti na karanga yanastawi karibu kila mkoa lakini hayalimwi kutosheleza hata mikoa husika.

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alitoa taarifa kwa wazalishaji wa mafuta ya kupikia wa Tanzania, kwamba wawasiliane naye kwa vile amepata soko la hiyo bidhaa, maeneo ya Caribbean. Ni jambo la heri lakini kama hadi sasa wenyewe ndani hatujitoshezi kwa mafuta tunaanzaje kupeleka nje?

Matufaa (apples) yanaingia Tanzania kutoka South Africa kitendo kinachomaanisha utokaji wa fedha zetu za kigeni kwenda nje. Sasa viongozi wanaoongoza mikoa ya Njombe na Tanga, ambako hali ya hewa inaruhusu matufaa kustawi wanafanya nini katika kuhakikisha kunazalishwa matufaa kuitosheleza Tanzania na kuuza nje?

Miaka ya karibuni nchi za jirani zimeigeuza Kariakoo, Dar kama China yao katika kuagiza bidhaa. Sasa viongozi wa mikoa wamejipangaje kiubunifu katika kuishawishi serikali kushirikiana na wadau wakuu katika sekta binafsi ili kuhakikisha dollar zinazoletwa na wachuuzi toka nchi jirani zinabaki Tanzania..zisiende China, lakini zile bidhaa wanazotaka wapate?

Koloni la Ujerumani la Tanganyika mwaka 1884 hadi 1916 lilijumuisha pia eneo la Rwanda na Burundi ina maana kama kusingekuwa na mabadiliko hizo nchi zingekuwa sehemu ya Tanzania pengine mojawapo ya mikoa ya magharibi pamoja na Kigoma. Nina uhakika mikoa hiyo ya Rwanda na Burundi kwa sasa ingekuwa katika hali inayofanana na Kigoma kimaendeleo na pato la kiuchumi kwa mwaka.

Rai yangu ni hii, tunatakiwa sasa kubadili mfumo wa namna wanavyopatikana viongozi wa mikoa. Muombaji wa nafasi ya mkuu wa mkoa anatakiwa kutoa na maelezo kwa kna namna anavyoujua mkoa husika kiundani akielezea ni hatua zipi atachukua katika kuzitumia fursa za rasilimali zilizopo katika mkoa ili kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa mkoa kwa ujumla.

Muombaji anatakiwa aoneshe ratiba ya utekelezaji wake ili watu watambue ndani ya miaka 5 ya kazi yake, mkoa utakuwa katika hatua zipi kiuchumi...na mengine mengi.
 
Mkoa wa njombe unafaa Kwa kilimo Cha alizeti lakini hakuna uhamasishaji wowote wa kilimo Cha zao hilo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom