Katika hili, natofautiana na Kikwete | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Katika hili, natofautiana na Kikwete

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Apr 23, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Apr 23, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,401
  Likes Received: 81,426
  Trophy Points: 280
  Katika hili, natofautiana na Kikwete

  Godfrey Dilunga Aprili 22, 2009

  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  INGAWA Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka ya uteuzi Rais, uteuzi ambao wakati mwingine unalindwa kisheria kutohojiwa bado milango ya kufuatilia nyendo za wateule hao iko wazi.

  Watanzania wanaweza kupiga kelele za kutoridhishwa na uteuzi wa viongozi unaofanywa na Rais, hususan uongozi serikalini, japokuwa wakati mwingine kelele hizo hazibadili chochote.

  Hata hivyo, pamoja na wakati mwingine kelele hizo kutobadili chochote bado Watanzania wanaweza kufuatilia na hata kuhoji utendaji wa wateule hao.

  Ni haki yao kufuatilia nyendo za wateule wa Rais kwa lengo la kupima tija yao kwa Taifa. Ni muhimu kufuatilia utendaji wao ili kujiridhisha kama kweli wanamsaidia Rais kutimiza ahadi zake kwa wananchi wake au vinginevyo.

  Kwa bahati mbaya katika muktadha huu wa uteuzi, Tanzania imekuwa ikiishi katika utamaduni usio na tija sana kwa raia wake walio wengi. Utamaduni wa mtu mmoja kurundikiwa vyeo.

  Ingawa utamaduni huo usio na tija ya wazi umedumu kwa miongo kadhaa sasa, sitapenda kuzungumzia serikali za awamu zilizopita.

  Kuzungumzia serikali zilizokwisha kupita hakuna tija kwa kuwa kama nitafanya hivyo hakutajitokeza mabadiliko yoyote.

  Nitajadili kwa kuitazama Serikali ya Awamu ya Nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kwa kusaidiwa na viongozi wenzake waandamizi, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

  Katika kujadili, nitawatazama wabunge walioteuliwa na Rais Kikwete tangu serikali hii ianze maisha yake. Nawajadili wabunge kama sehemu tu ya viongozi wengi walioteuliwa na Rais, kumsaidia.

  Kundi hili la wabunge wa kuteuliwa linajumuisha wabunge ambao wamewahi kuwa mawaziri au naibu mawaziri. Baadhi wakiwa wamekwisha kujiuzulu kwa sababu mbalimbali.

  Kwanza tukumbushane majina ya wabunge hao wa kuteuliwa na Rais. Zakia Meghji, huyu alipata kuwa Waziri wa Fedha; Kingunge Ngombale-Mwiru, naye alipata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, na Sophia Simba ambaye mwanzo wa maisha ya Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Utawala Bora.

  Katika kundi hilo la wabunge wa kuteuliwa na Rais pia yumo Mohammed Aboud Mohamed ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, sasa ni Naibu Waziri wa Afrika Mashariki.

  Hao ndiyo wabunge wa kuteuliwa na Rais lakini pia ni wateule wa Rais katika nyadhifa za uwaziri na naibu waziri.

  Wabunge wengine wa kuteuliwa na Rais ni Yusuf Makamba, ambaye pia ni mteule katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Yumo pia Thomas Mwangíonda na Hadija Saleh Ngozi.

  Lakini kwa kuwa tunazungumzia moja ya mihimili ya Taifa (Bunge) wenye jukumu la kikatiba la kuisimamia na kuishauri Serikali, tukumbuke kuwa wapo wabunge wa majimbo walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa.

  Hao ni pamoja na Mohammed Abdulaziz ambaye ni Mbunge wa Lindi Mjini, Monica Mbega ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini, William Lukuvi wa Ismani, Dk. James Msekela wa Tabora Kaskazini.

  Katika kundi hilo la wabunge wakuu wa mikoa yupo pia Mbunge wa Vitimaalumu, Dk. Christine Ishengoma.

  Lakini pia ipo sura nyingine ya wabunge ambao wamepewa uteuzi mwingine. Hapa tunakutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, George Mkuchika, ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na wakati huo huo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM.

  Makundi haya tunaweza kuyaweka katika sehemu tano. Kundi la wabunge wa kuteuliwa na Rais, pili kundi la wabunge wa kuteuliwa na Rais lakini pia wameteuliwa kuwa mawaziri au naibu mawaziri.

  Tatu, wabunge walioteuliwa kuwa mawaziri lakini pia wameteuliwa kuwa viongozi waandamizi wa CCM. Nne, wabunge walioteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa.

  Tano, ni mbunge wa kuteuliwa na Rais na ambaye pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM.

  Sina tatizo katika uteuzi wa wabunge kuwa mawaziri au naibu mawaziri kwa kuwa hayo kwa sasa ni maelekezo halali ya Katiba. Maelekezo ambayo hata hivyo, hayana tija sana kwa Taifa.

  Nitajadili utashi huu wa Rais Jakaya Kikwete wa kuteua mawaziri kuwa viongozi waandamizi wa CCM, na namna anavyopima utendaji wa wabunge wake wa kuteuliwa. Lengo ni kutaka kujua kama vipimo vyake vinaonyesha majibu yanayofanana na maoni ya wananchi wengi kuhusu wabunge hao.

  Tuanze na hili la mawaziri kuteuliwa kuwa viongozi waandamizi wa CCM. Hapa nawazungumzia akina Chiligati na Mkuchika.

  Nitatumia mifano ya wazi. Kama inavyofahamika Waziri Chiligati anaongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Hakuna utata kwamba wizara hii imezongwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

  Ni kati ya wizara isiyoridhisha Watanzania wengi kiutendaji. Mara kwa mara, watendaji wa wizara hii wametumbukia katika migongano na wananchi. Wananchi ambao kimsingi ndiyo wapiga kura wa CCM na vyama vingine vya upinzani.

  Kwa mfano, Waziri Chiligati anajua kuwa katika eneo la Kwembe, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam watendaji wake wizarani wapo kwenye mvutano mkubwa na wakazi wa eneo hilo.

  Ardhi ya wakazi wa eneo hilo ipo katika mchakato wa kupimwa. Lakini kinachowaudhi wakazi hao si mantiki iliyopo ya upimaji maeneo yao, bali ni namna mchakato huo unavyoendeshwa. Inadaiwa mchakato huo unafuka moshi wa ufisadi.

  Waziri wa wizara hii mbele ya wananchi wa Kwembe anaonekana kushindwa kupata ufumbuzi wa haraka na wa uhakika wa suala hilo.

  Kushindwa kwa waziri huyo kunathibitishwa na kauli za baadhi ya wakazi hao kwamba malalamiko yao wameanza kuyaelekeza kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

  Katika hali ya kawaida, kitendo cha wananchi kuelekeza malalamiko yao kwa Waziri Mkuu na huku Waziri mwenye dhamana akiwa ofisini kina maana kubwa.

  Ukweli ni kwamba kitendo hicho cha kuelekeza malalamiko kwa Waziri Mkuu, wananchi wanakuwa wametoa ujumbe kuwa waziri mhusika ameshindwa kutumia madaraka yake vema kumsaidia kiutendaji Rais au Waziri Mkuu.

  Ndani ya mazingira kama hayo ya waziri kuonekana kushindwa kutatua matatizo ya wananchi, tena matatizo ambayo yapo ndani ya uwezo wake, ni ishara kwamba mawasiliano au uhusiano kati ya wananchi husika na kiongozi wa wizara husika yamekatika au si mazuri.

  Na katika mazingira hayo kwa mfano, CCM inafanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuomba kura ili kupata ushindi wa uchaguzi wa ngazi fulani na kwa kuwa Chiligati ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, bila shaka atapaswa kuwapo jukwaani.

  Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba tayari taswira ya chama hicho katika muktadha wa kuwatumikia wananchi itakuwa imechafuliwa na kuwapo kwa Chiligati jukwaani.

  Mifano ya namna hii ya viongozi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wao kwa umakini katika madaraka yao serikalini na wakati huo huo kutakiwa kutimiza wajibu wao wa kiuongozi katika chama imekwisha kubainisha gharama kubwa kwa CCM.

  Wengi watakumbuka mfano wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Omar Ramadhani Mapuri.

  Katikati ya pilikapilika za uchaguzi, Mapuri alijikuta akitumia madaraka yake ya uwaziri vibaya baada ya kutoa kauli za kejeli dhidi ya wanahabari, lakini wakati huo huo saa chache baadaye akitakiwa kufanya mkutano na wanahabari kuhusu kampeni za CCM.

  Haya yanaweza kuepukwa kama Rais ataamua kuwa msikivu kwa kuteua mtu mmoja katika cheo kimoja. Watu wapeane nafasi ili waweze kuwajibishana na hata kufokeana lakini kwa maslahi ya Taifa.

  Lakini jambo jingine muhimu ni kuhusu wabunge wa kuteuliwa. Kwa wananchi wa kawaida naweza kusema ni vigumu kwao kupima ufanisi wa wabunge hawa.

  Inawezekana Rais anachokipimo sahihi kupima utendaji wa wateule wake hao. Hata hivyo, swali moja kubwa la kujiuliza ni je, kipimo hicho cha Rais kimeonyesha majibu sawa na kile wanachokiona Watanzania walio wengi?

  Awali, nimewataja kwa majina wabunge wa kuteuliwa na Rais. Sasa kwa kuzingatia majina hayo tujiulize ni kweli wametoa tija ya wazi kwa Taifa?

  Jibu linaweza kuwa ndiyo au hapana kulingana na mtazamo wa mtu kwa kuwa hakuna kipimo cha jumla kuwapima wabunge hao.

  Ingawa tunajua kuwa jukumu la msingi la mbunge ni kuishauri na kuisimamia serikali lakini bado ni vigumu kuwapima wabunge hawa wa kuteuliwa na Rais.

  Ni vigumu kwa sababu hawana ahadi yoyote kwa wananchi ikilinganishwa na wabunge wa majimbo au hata wa viti maalumu. Ahadi yao ipo katika kiapo lakini kiapo pekee si kipimo cha ufanisi wa kiongozi.

  Kikubwa ninachozungumzia hapa ni kwamba matakwa ya wakati sasa yanatushinikiza kuweka mfumo wa kupima utendaji wa wabunge wa kuteuliwa na Rais.

  Lengo kuu hapa si kutaka kuwakomoa wabunge hawa bali ni kujijengea uwezo madhubuti wa kupima ufanisi wao. Si sahihi kuwaacha huru kama ilivyo sasa, kwamba ni hiari yao kuwajibika au la.

  Tusipokuwa na mfumo wa kupima utendaji kazi wa wabunge wa kuteuliwa na Rais, inaweza kutokea siku moja Rais akafanya uteuzi unaozingatia kujaza nafasi tu, badala ya vigezo muhimu vya bidii, maarifa na uwajibikaji.

  Mfumo ninaolenga hapa uwe na uwezo hata wa kutengua uteuzi wa mbunge aliyeteuliwa na Rais, kama itathibitika kuwa mteule amekuwa akizubaa kiutendaji kadiri miaka inavyozidi kusogea mbele.

  Kwa upande mwingine, nizungumzie wabunge walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa. Kwa kuwa wabunge hawa wameendelea kuwa wakuu wa mikoa kwa kuhamishwa vituo vyao vya kazi tu hivi karibuni, nathubutu kusema kuwa katika hili, Rais Kikwete hakuwa msikivu.

  Nafahamu Rais amewahi kuwa msikivu katika baadhi ya mambo, ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri. Hata hivyo, katika suala la wabunge kuwa wakuu wa mikoa nadhani ni vema zaidi Rais Kikwete akawa msikivu.

  Wanaomshauri kutowarundikia madaraka baadhi ya Watanzania wana nia njema kwa Taifa lao kama ilivyo kwa yeye Rais Kikwete alivyo na nia njema kwa Watanzania hao, vinginevyo uteuzi huu unaweza kuwa unanasa miguu ya wateule hawa katika serikali na CCM, katika kuwatumikia Watanzania kwa tija ya kiwango cha juu.
   
Loading...