Katiba yatikisa nchi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Katiba yatikisa nchi

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by nngu007, Apr 12, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 12, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145




  *Muswada waendelea kupingwa kila kona
  *Sheikh Zanzibar achana vipande rasimu yote
  *Sitta: Kuvunja Muungano ni uwendawazimu
  *Kisumo: Tukivaa vilemba vya vyama tutaumia

  Na Waandishi Wetu
  [​IMG]

  MJADALA wa kujadili muswada wa marejeo ya Katiba mpya, umeanza kuitikisa nchi kutokana na kupingwa karibu kila kona ya taifa hili.

  Watu wa kada mbalimbali, wasomi, wanasiasa wakongwe na wananchi wameonyesha wasiwasi wao kutokana na muswada huo kujaa vipengele vinavyoonekana kuleta utata.

  Baada ya wanasiasa hasa wa upinzania kuukataa, sasa Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara (TLS) kimepinga utaratibu uliowekwa na Rais Jakaya Kikwete wa kutoa maoni kuhusiana na muswada wa sheria na mapitio ya Katiba.

  Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho, Francis Stolla, alisema lengo la muswada huo ni zuri, lakini kasoro zake ni nyingi kiasi kwamba hautatoa haki kwa wananchi walio wengi.

  ‘Tumepata taarifa kwamba muswada huo, umepelekwa bungeni na Rais kwa hati ya dharura, hivyo hakutakuwa na muda wa kutosha kuujadili, kufanya hivyo kutawanyima haki Watanzania wengi kuujadili,” alisema Stolla.

  Alisema kutokana na hali hiyo, wanamshauri Rais Kikwete aondoe hati ya dharura ili mjadala uwafikie watu wengi zaidi.

  “Kwanza kabisa maeneo yaliyotengwa ni machache ukilinganisha na idadi ya Watanzania, ukiachilia mbali jambo hilo pia siku zilizotengwa ni chache.

  “Wananchi wengi hawatapata muda wa kushiriki, lakini sisi tukiangalia jambo hili hatuoni sababu ya kuharakishwa namna hii, kwa sababu ni jambo linalogusa maslahi ya Watanzania wengi.

  “Tunahitaji muda mwingi zaidi wa kujadili, lakini pia tatizo tuliloliona ni kwamba muswada huu umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

  “Hebu tujiulize ni Watanzania wangapi wanaielewa lugha hii, tunajua kabisa Watanzania walio wengi hawajui lugha hii watapata shida kutoa maoni yao.

  “Pamoja na mambo mengine tunaiomba ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) imshauri Rais kuhusiana na mambo haya ili wananchi wapate muda na eneo pana zaidi la kujadili jambo hili.

  “Tunachotaka kusisitiza hapa ni kwamba Rais Kikwete asiwe taasisi ya kuunda Tume wala kuteua wajumbe kama ilivyoainishwa katika muswada huo, kwani kufanya hivyo hakutatoa haki, yeye anaweza akaunda chombo kinachoitwa Baraza la Katiba kwa ajili ya kushughulikia jambo hili, mckahakato huu tunataka uwashirikishe zaidi wananchi.

  “Jambo jingine ni kwamba haifai Bunge la Tanzania kuwa Bunge la Katiba katika mchakato huu kwani kile ni chombo cha kisiasa, Bunge la Katiba linatakiwa kujumuisha watu mbalimbali wakiwemo wakulima, wataalamu wa sheria na watu katika kada mbalimbali,” alisema.

  Ikulu yakanusha uvumi

  Hata hivyo, akizungumza na Mtanzania Jumapili, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alikanusha taarifa za muswada huo kuwasilishwa bungeni chini ya hati ya dharura. “Hakuna kitu kama hicho. Kuna dharura gani katika kuwasilisha muswada huu? Tafuteni ukweli wenyewe, huo ni upotoshaji,” alisema Rweyemamu.
  Mtanzania Jumapili ilipowasiliana na Afisa wa Bunge aliyeomba jina lake lisitajwe, alisema muswada huo utasomwa bungeni Jumanne wiki ijayo, na baada ya hapo utajadiliwa kidogo kwani utakuwa umesomwa mara ya kwanza, na baadae utasomwa mara ya pili Juni.

  Alisema Bunge la Bajeti linaanza Juni 8, lakini utaandaliwa utaratibu ambapo muswada wa Katiba mpya utajadiliwa kwa wiki moja kabla ya kuanza kwa Bunge la bajeti, kisha mambo yataendelea.

  Naye alisisitiza kuwa utakuwapo muda wa kutosha kujadili muswada huo na kuwa hakuna hati ya dharura iliyotumika kuwasilisha muswada huo.

  Sheikh auchana muswada

  Mbali ya chama hicho, tayari muswada huo wa mapitio ya Katiba umepingwa na watu mbali ikiwemo wananchi wa Zanzibar ambao wamepinga kuujadili kwa madai kuwa una mapungufu mengi.

  Lakini pia wanasiasa mbalimbali hapa nchini wamepinga muswada huo kwa madai kuwa umetungwa kwa maslahi ya watu wachache.

  Mjini Unguja, Zanzibar, mkutano wa kujadili muswada wa kuundwa kwa Tume ya Katiba ulivunjika jana baada ya Sheikh Farid Hadi Ahmed, kuchana rasimu ya muswada huo mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.

  Tukio hilo, limetokea katika Ukumbi wa Haile Sellasie mjini hapa ambapo Sheikh huyo aliamua kuuchana muswada kwa madai kuwa hauna maslahi kwa Wazanzibari.

  Viongozi waliokuwapo kwenye mkutano huo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliyetoa mada kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan na wajumbe wengine wa Kamati hiyo ya Bunge ya Katiba na Sheria.

  Baada ya Sheikh huyo kufanya hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, Jadi Simai Jadi, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni mkoa wa Kaskazini Unguja, alisimama na kusema: “Jamani hapa ndio mwisho wa mjadala huu kufuatia kuwepo kwa usalama mdogo.”

  Kabla ya kuuchana, Sheikh huyo alidai muswada huo hauna uhalali wa ridhaa ya Wazanzibari kwa kuwa hawakushirikishwa na hivyo si sahihi kuujadili.

  “Mheshimiwa Mwenyekiti mimi naamua kuuchana muswada huu kwa sababu hauna ridhaa ya Wazanzibari, wajumbe vipi mnasemaje niuchane ni nisiuchane?”

  Mara zikasikika sauti kutoka kwa wajumbe zikisema: “Chanaa.” Naye akauchana vipande.

  Hata hivyo wengine walilaumu kitendo hicho kuwa haikuwa busara.

  Awali akizungumza katika mkutano huo, Sitta alisema ni uwendawazimu kuwa na fikra za kutaka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 47 sasa.

  “Hatuwezi kuwaachia watu kwa mfano anakuja mtu anasema hataki Muungano, au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ifutwe… huyu hatuwezi kumvumilia,” Sitta alisema.
  Alisema pamoja na maoni yote suala la kulinda Muungano ni jambo la msingi. Alisema Ibara ya 9 ibara ndogo ya (2) imeiwekea Tume mwongozo wa jinsi ya kushughulikia masuala yenye maslahi kwa Taifa.

  Alitaja mambo hayo kuwa ni kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuwepo kwa mihimili ya dola, kuwepo kwa nafasi ya Rais; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwepo kwa mshikamano wa Kitaifa na amani ya nchi.

  Mengine ni kuwepo kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, kuwepo kwa haki za binadamu, kuwepo kwa dhana ya utu wa mtu, usawa mbele ya sheria na mfumo unaweka utaratibu wa kufuata sheria na dhana ya nchi ya Tanzania kutokuwa na dini; na kuwepo kwa uhuru wa mahakama.

  Peter Kisumo aonya

  Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo, amesema amesikitishwa na jinsi hali ya ukusanyaji maoni juu ya Katiba mpya ilivyoanza kutikisa nchi.

  Alisema malumbano yaliyoanza kuibuka hayana tija kwa taifa wala vyama vya siasa.
  “Hivi sasa kuna chama fulani kinadhani ndiyo kimebeba dhamana ya taifa hili, tusikubali hali hii ikaendelea.

  “Huu si wakati wa kuvaa vilemba vya vyama kwani ajenda hiyo, italeta fujo. Kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake.

  “Mpaka sasa sijapata rasimu ya Katiba, lakini juzi nilimsikiliza Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, alishauri wananchi washirikishwe.

  Taasisi ya JOPA

  Katika hatua nyingine, uongozi wa Taasisi ya JOPA umesema umeandaa maandamano kwa wiki ijayo, yatakayoanzia Viwanja vya Jangwani hadi lango kuu la ofisi ndongo za Bunge jijini Dar es Salaam.

  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utafiti uliyofanyika katika mikoa ya Tanzania Bara kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na mchakato wa Katiba, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Praygod Mmassy, alisema imeonyesha Watanzania wengi hawaukubali muswada wa Katiba mpya.

  Alisema taasisi yake inawashauri Watanzania, asasi za kidini na makundi yote kupinga kwa nguvu zote mapendekezo ya Serikali, kwa kutoa matamko na kufanya maandamano ya amani kupinga muswada huo.

  Habari hii imeandaliwa na Elizaberth Mjata, Kulwa Karedia, Dar na Juma Mohammed, MAELEZO, Zanzibar.
   
 2. Kigogo

  Kigogo JF-Expert Member

  #2
  Apr 12, 2011
  Joined: Dec 14, 2007
  Messages: 20,498
  Likes Received: 1,453
  Trophy Points: 280
  ndo kikwete ajue hatutaki utanikwenye mambo serious..ye anadhani huu ni muswada wa katibu wa kuunbda chama cha wacheza drafti pale magomeni mapipa
   
Loading...