Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,243
- 34,903
OTHMAN Masoud Othman, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kabla ya kutimuliwa kwa kuunga mkono mapendekezo ya serikali tatu, amesema Katiba inayopendekezwa itajenga mfumo utakaosababisha kizazi kijacho cha Zanzibar kidai uhuru badala ya haki ndani ya Muungano.
Othman alifutwa kazi na Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na nafasi yake kuchukuliwa na Said Hassan Said baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba 2014, ambapo alipiga kura ya wazi ya kuunga mkono mapendekezo ya serikali tatu kinyume na msimamo wa chama tawala.
Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Katiba uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Othman amesema;
“Kwa ujumla Katiba inayopendekezwa sio tu kwamba imerasimisha kero za Muungano lakini inajenga mfumo utakaofanya kizazi kijacho cha Zanzibar kidai uhuru badala ya haki ndani ya Muungano.”
Amesema katika kujenga mustakbali wa kikatiba ndani ya Tanzania, suala la Muungano haliwezi kuepukwa kuwa ajenda kubwa na ya msingi.
“Taifa letu limepata uzoefu wa kutosha wa kasoro za Muungano. Ni dhahiri kuwa itikadi na kutokuwepo upeo na uthabiti katika kujenga mfumo mpya wa kikatiba kumesababisha Katiba inayopendekezwa kuwa mbaya na dhaifu zaidi, katika kujenga mustakbali huo,” amesema Othman