sirluta
JF-Expert Member
- Nov 28, 2012
- 6,325
- 2,487
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa hata bunge la Uingereza halionyeshwi ''LIVE " kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo lilikuwa likionyeshwa kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana, na kuanzia saa 10 jioni hadi saa 2 usiku na kupelekea watu kutokufanya kazi na badala yake kuamka asubuhi kufuatilia bunge kwa muda wa miezi hadi mitatu.
Mosi, Tanzania bado haina taasisi zinazojisimamia na kufanya maamuzi Yake hivyo kutumiwa na serikali ktk kufanya mambo Yake mfano ni taasisi ya Bunge ambalo limekuwa dhaifu sana mbele ya serikali kwa muktadha huo kitendo cha kuonyesha bunge Moja kwa Moja linapunguza nguvu hiyo ya serikali kuzikandamiza taasisi ambazo zilipaswa kuwa huru hofu ya wananchi inakuwa ndio kinga za Moja kwa moja kwa taasisi hizo kama bunge.
Pili, kama lengo la serikali ni kutaka watu wafanye kazi basi ni muhimu kutoa amri ya kutokuwa na TV ktk maeneo ya ofisi za serikali na mahospitalini.
Tatu viongozi wasitumie waandishi wa habari popote waendako maana pia habari zao ni upotevu wa muda.
Nimetazama ITV hotuba ya Waziri Mkuu Bw.Kassim Majaliwa kwa wana CCM waishio LONDON, kweli ni aibu, Kama Taifa tumefikia huku, ni aibu sana, nilijisikia aibu zaidi pale waziri Mkuu aliposema kuwa wamezuia BUNGE LIVE ili wananchi wafanye kazi, kwani BUNGE LIVE linasababisha watanzania wasifanye kazi na kubaki kukodolea macho bunge kwenye TV!
Kilichonisikitisha zaidi ni wale MA- DIASPORA kupiga makofi na kumsifia! Kweli watanzania tumefikia mahali huku? Hivi hawa wanaCCM wanaoishi nje ya nchi nao wamekuwa kama akina Agnesy Marwa? Nilitegemea kukaa kwao nje ya Nchi kutawapa Exposure kumbe hamna kitu! Hii ni aibu sana! Hizi TV zilizozuiwa kuonyesha LIVE bunge, wakati bunge linaendelea huwa zinakuwa zinaonyesha vipindi vingine au zinakuwa zimezima mitambo yake? Hivi vipindi vingine havizuii watu kufanya kazi?
Majaliwa: Kuzuia Bunge Live ni kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu
Kwa ufupi
Awali, Waziri wa Habari, Nape Nnauye ambaye alitoa tamko hilo bungeni, pia alisema vyombo binafsi vinaruhusiwa kurusha matangazo hayo moja kwa moja, lakini navyo vimepigwa marufuku.
Dar es Salaam. Sababu za kuzuia vituo vya televisheni kurusha moja kwa moja shughuli za Bunge zimezidi kuongezeka baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusema uamuzi huo ulifanywa kutekeleza kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”.
Tayari Bunge limeshaelezwa sababu mbili tofauti za kukatisha matangazo hayo ambazo ni gharama ambazo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linalipia na hivyo kulazimika kupunguza matangazo hayo.
Awali, Waziri wa Habari, Nape Nnauye ambaye alitoa tamko hilo bungeni, pia alisema vyombo binafsi vinaruhusiwa kurusha matangazo hayo moja kwa moja, lakini navyo vimepigwa marufuku.
Sababu nyingine iliyotolewa na Nape ni kuwa uamuzi wa kuzuia matangazo hayo ulifanywa na Bunge la Kumi wakati likipitisha uamuzi wa chombo hicho wa kuanzisha studio yake.
Lakini juzi, akiwa nchini Uingereza Majaliwa alikuwa na sababu nyingine ya kuzuia matangazo hayo kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.
Akijibu swali kuhusu sakata hilo wakati akizungumza na Watanzania waishio London, Majaliwa, alisema kurusha moja kwa moja matangazo ya shughuli za Bunge ni kwenda kinyume na “Hapa Kazi Tu”, kaulimbiu ya Rais John Magufuli aliyoianzisha wakati wa kampeni.
“(Kurusha shughuli za Bunge moja kwa moja) Maana yake ni kuwa katika kipindi cha Bunge la Bajeti ambalo linaendeshwa kila siku, Watanzania wangekuwa wanaangalia Bunge kwa miezi hiyo mitatu bila ya kufanya kazi,” alisema mtendaji huyo mkuu wa Serikali.
“Tulilazimika kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. Hivi hapa Uingereza mnaangalia Bunge live kila siku?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa kuwa linarushwa moja kwa moja kwa kipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu.
Majaliwa alisema Bunge la Tanzania lilikuwa pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani ambalo lilikuwa likirushwa moja kwa moja kuanzia asubuhi hadi usiku.
Waziri Mkuu aliendelea kufafanua kwamba Bunge la Tanzania linarusha moja kwa moja kila siku asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu.
Alisema mijadala yote hurekodiwa na kuhaririwa, kisha hurushwa kati ya saa 8:00 mchana na 9:00 alasiri na kati ya saa 3:00 na 4:00 usiku.
“Kwa Watanzania wanaopenda kufanya kazi na wanaopenda kufuatilia mambo ya bungeni, walikuwa hawaoni ‘live coverage’ kwa sababu walikuwa kazini, lakini sasa hivi wanaweza kufuatilia masuala ya Bunge,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa muda wa jioni uliopangwa, mtu anakuwa ametoka kazini na anaweza kuangalia televisheni akiwa nyumbani.
Vita ya rushwa na watumishi hewa
Kuhusu suala la rushwa, Majaliwa alisema katika mkutano huo kwamba Serikali imeamua kupambana na wala rushwa ili kiasi kidogo cha rasilimali kilicholengwa kiweze kuwafikia wananchi.
“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua kufanya hivyo ili kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania, tunataka tuibadili Tanzania ili iwe ni ya Watanzania wote,” alisema Majaliwa.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba Waziri Mkuu alizungumzia suala la kusaka watumishi hewa na kusisitiza kwamba Serikali itawashughulikia wale wote waliohusika na udanganyifu huo.
“Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000 na tumeokoa zaidi ya Sh4.5 bilioni zilizokuwa zikipotea kila mwezi. Tukikamilisha zoezi la kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni kina nani walikuwa wakipokea fedha hizo. Waliohusika tutashughulika nao,” alisisitiza.
Alisema hivi sasa Serikali inalenga kuwa na watumishi ambao wanafanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi. “Hiki ndicho kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano na tena zoezi hili litakuwa endelevu”, alisema Waziri Mkuu.
Uchumi
Kuhusu ukuaji wa uchumi, Waziri Mkuu ambaye alikuwa London kwa niaba ya Rais Magufuli kuhudhuria mkutano uliojadili mapambano dhidi ya rushwa, alisema lengo la Serikali hivi sasa ni kuona kuna ukuaji wa uchumi unaokwenda sambamba na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alisema viwanda vingi viliuzwa na watu waliovinunua wakageuza kuwa ni maghala ya kufugia wanyama. “... Sisi tunataka vifufuliwe ili teknolojia mpya na za kisasa zije Tanzania.”
“Tunataka usindikaji wa mazao na bidhaa ufanyike nchini mwetu badala ya kupeleka mazao ghafi nje ya nchi, kwa njia hiyo tutakuwa pia tumezalisha ajira kwa watu wetu,” alisema Majaliwa.
“Kuna Watanzania waishio Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta wawekezaji nchini. Kwa mfano, wa Poland wameleta mradi wa umeme katika vijiji vitano vilivyopo Wilaya ya Ileje.
“Kwa hiyo nanyi endeleeni kuishi Uingereza, lakini mhakikishe kuwa ukaaji wenu hapa, unaleta tija kule nyumbani. Ikumbukeni Tanzania na muwe tayari kuihudumia nchi yenu,” alisema.
Chanzo: Mwananchi