Kashfa tano zimeitesa Serikali ya awamu ya nne

Kashfa tano zimeitesa Serikali ya awamu ya nne

waltham

JF-Expert Member
Joined
Jan 23, 2014
Posts
2,522
Reaction score
1,045
Hebron+mwakagenda.jpg

Hebron Mwakagenda

Ndugu wasomaji wangu leo nikiwa hapa hapa Tanzania baada ya mwaka wa 2014 kugeuka na sasa tuko 2015, ni mwaka ambao kwanza kwa maombi yangu na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu tuliouona mwaka 2015 tujiandae kwa mengi makubwa.

Mwaka 2015 ni mwaka ambao kwetu kitaifa utakuwa na mambo makubwa sana ikiwemo kura ya maoni au maamuzi tarehe 30 Aprili 2015 na Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Umuhimu wake pia unakuwepo zaidi kwa sababu Rais Kikwete anamaliza muda wake kwa hiyo lazima tupate Rais mwingine kwa miaka mitano ijayo, ingawa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ndiyo kwanza amemaliza miaka yake mitano ya uongozi wake na sasa atakuwa anatafuta ridhaa ya miaka mitano mingine.

Baada ya kuandika mambo mengi sana ya siasa na kijamii siku za nyuma leo, nimuangalia Rais wetu mpenzi Profesa Jakaya Kikwete ambaye sasa yuko kwenye mwaka wake wa mwisho na wa 10 tangu awe Rais wa Jamhuri, Novemba 2005.

Kwenye makala hii najaribu tu kuwakumbusha Watanzania kashfa nzito zilizotikisa nchi na uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa nchi, ukiachilia mbali kashfa ndogondogo ambazo nazo zilikuwa nyingi katika kipindi hiki cha miaka 10 cha uongozi wa awamu ya nne.

Katika nchi nyingi za Afrika, vyama vya siasa vilivyoshika madaraka kwa muda mrefu, utafiti unaonyesha kuwa huendelea kukaa madarakani kupitia uchaguzi uliosimamiwa na vyombo ambavyo siyo huru, kwa jina la Tume za Taifa au Huru za Uchaguzi.

Utafiti huo unaendelea kusema kuwa pia kila uchaguzi unapokaribia, vyama hivi na serikali zake hubuni mbinu za kushinda mchakato wa uchaguzi kwa kuchukua fedha maeneo ambayo hayakupangwa.

Kimsingi, utafiti wa madeni ya taifa unaonyesha kuwa katika kila miaka ya uchaguzi, madeni ya taifa husika, ikiwemo Tanzania, hupanda tofauti na miaka mingine.

Katika makala haya, nitajaribu kuwakumbusha Watanzania masakata mbalimbali yaliyotikisa taifa kabla ya Rais Kikwete kuingia Ikulu na zile ambazo zilitokea wakati yeye akiwa madarakani na hatua alizochukua.

1.0. SAKATA LA EPA

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005 kampuni mbili za Meremeta Gold Limited naTangold Limited zilifanya wizi wa zaidi ya Sh155 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu (BoT) na wakati huohuo makampuni 22 yalijihusisha na wizi wa Sh133 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo ya EPA.

Hatua zimechukuliwa kwa baadhi ya maofisa wa Benki Kuu ambao wamefungwa, lakini ni watuhumiwa wachache kampuni nyingi waliokwapua fedha hizo wamefungwa na walio wengi wameshinda kesi zao, wanaendelea ‘kutanua' uraiani na wengine waliambiwa na Rais mwenyewe warejeshe fedha hizo.

Wachambuzi wa masuala ya uchaguzi wanaunganisha hatua zilizochukuliwa dhidi ya wezi husika katika kashfa husika na kwamba ni kiinimacho tu kwa Watanzania ili waone kweli kwamba ni wizi wa kawaida na kuonyesha kuwa hatua zinachukuliwa.

Aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali alifukuzwa kazi na Rais Kikwete na akarudi Marekani ambako alikuwa na uraia wa nchi hiyo na baadaye tukaambiwa amefariki dunia, jambo ambalo nalo Watanzania walio wengi walilitilia shaka.

Hata hivyo wananchi wanaandika kuwa yuko hai na anakula maisha huko na wakati mwingine picha zake zinaonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ameonekana maeneo fulani fulani. Ikumbukwe kuwa Daudi Balali alikuwa ni shahidi muhimu sana kwenye kesi ya EPA.

2.0. MABILIONI YA JK

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 Rais Kikwete alikuja na mpango maarufu kama mabilioni ya JK na Sh50 bilioni zilitolewa kwa Benki ya NMB kwa ajili kukopesha wafanyabiashara wa kati ili kuendeleza biashara zao.

Taarifa zilizotolewa na watu mbalimbali waliokopa fedha hizi ni kwamba watu wamezichukua kama ruzuku na siyo mikopo na urejeshaji wake umekuwa wa shaka na wa kusuasua.

Taarifa ya Dk Mary Nagu, Waziri wa Uwezekezaji na Uwezeshaji aliyoitoa mwaka 2012 alisema ni Sh43 bilioni tu kati ya Sh50bilioni zilizorejeshwa serikalini na wafanyabiashara waliokopa na akaendelea kusema mikopo hii ilibadilisha maisha ya watu 70,000 nchi nzima.

Huu ni ushahidi tosha kuwa huu mpango huo inawezekana kuwa haukuwa umelengwa kwa kundi maalumu, bali kuwapa asante baadhi ya Watanzania kwa kampeni na kushinda uchaguzi.

Je, hizi Sh7bilioni zimekwenda wapi na hatua gani zimechukuliwa na serikali au hata NMB ambao ndiyo walikuwa wakala wa Serikali katika ukopeshaji huu.

3.0. SAKATA LA RICHMOND AU DOWANS

Sakata hili lilitokea mwaka 2008 baada ya Tanzania kupata upungufu mkubwa wa umeme mwaka 2006 na serikali iliingia mkataba na kampuni hewa ya Richmond Development Company LLC kwa mkataba wa Sh172 bilioni za kitanzania.

Kampuni hii ilikuwa haina uwezo wa kufanya kazi hiyo kubwa ya kuzalisha umeme wa megawati 100 na hata majenereta hayakufika kwa wakati licha ya mpango wenyewe kuwa wa dharura.

Baada ya kelele za wapinzani bungeni, Bunge liliunda kamati iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ambayo iligundua mambo mengi na kuja na mapendekezo 23, likiwemo la kumtaka aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujipima na waliokuwa mawaziri wa wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati mbalimbali, yaani Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.

Huu ukawa ndiyo mwisho wa mchezo. Hakuna hatua zaidi zilizochukuliwa dhidi ya wahusika na kampuni feki ya Richmond ikauza kazi zake kwa kampuni halali ya DOWANS na inaendelea na kazi ya kuzalisha umeme hadi leo hii.

4.0. FEDHA ZA KUPUNGUZA MAKALI YA UCHUMI ya 2008/2009

Baada ya mdororo wa uchumi uliotokea Ulaya na Marekani ambao athari zake zilifika hata Afrika na Tanzania. Serikali ya Tanzania ilitenga fedha kwa ajili ya kufidia na kupunguza makali ya athari zilizotokana kutetereka kwa uchumi duniani.

Serikali ya Tanzania ilitenga fedha kwa ajili hiyo na kuwafidia baadhi ya wakulima na wachuuzi. Hata baada ya Bunge kutaka kujua kiasi cha fedha na kampuni zilizofidiwa mpaka leo jambo hili limekuwa ni siri.

5.0. AKAUNTI YA TEGETA ESCROW

Hili ni sakata la mwaka 2014 ambalo lilihusu Sh306 bilioni kuhusu gharama za umeme ambazo kampuni ya IPTL ilikuwa inaitoza Tanesco tangu ilipoanza kuzalisha umeme.

Fedha zilichukuliwa na mmoja wa wanahisa kampuni ya VIP Engineering dola 75milioni na ziligawiwa kama njungu kupitia Benki ya Mkombozi kwa watu mbalimbali aliowataka yeye wakiwemo na watumishi wa serikali, jambo ambalo limeleta mjadala mkali sana kwenye jamii kuhusu nia ya mgawo huu kwa watumishi wa serikali, akiwemo na Waziri Anna Tibaijuka. Fedha zilizopitishwa kwenye benki ya Stanbic toka kampuni ya PAP bado ni siri na imeleta hisia mbaya kwamba huenda viongozi wa serikali wakubwa wamo au familia zao za karibu zimo ndiyo maana imekuwa siri, muda unavyoenda huenda siri hii ikafichuka.

HITIMISHO

Tunasema BoT ihakikishe kwamba ‘Kashfa ya EPA na Akaunti ya Tegeta Escrow hazijirudii katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Tunasema hivyo kwa sababu kashfa hiyo ilitokana na udhaifu wa uongozi wa benki hiyo uliokubali kuvurugwa na kuingiliwa na wanasiasa.

Source:
Mwananchi
 
Back
Top Bottom