Karibu elimumsingi bila malipo

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
KAMA Mzazi inapenda kuanza mwaka huu mpya wa 2016 kwa kuwapongeza wote waliobahatika kwa mapenzi ya aliyetuumba kuwa hai na salama na kuendelea kuomba Mungu awalinde kwa mwaka huu tangu mwanzo hadi mwisho wake.

Tunawajibika kushukuru kwa sababu kuna wenzetu hawakubahatika kuuona mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wetu. Lakini kubwa kwa Januari hii ya 2016 ni zawadi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa wazazi na walezi kwa kuanzisha elimumsingi bila malipo kwa vitendo.

Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali,ya msingi na sekondari, kuwa bure kwa gharama za serikali kwa shule za ngazi hiyo zinazomilikiwa na serikali ispokuwa shule 11 tu nchi nzima. Hongera sana serikali ya Rais Magufuli kwa kuishi kwa vitendo.

Kwa mujibu wa waraka wa serikali uliotolewa katikati ya Desemba mwaka jana, uliainisha wazi majukumu ya serikali katika utekelezaji wa elimumsingi bila malipo lakini pia ulioanisha majukumu ya wazazi katika utekelezaji wa jambo hili ili watoto waweze kusoma bila kupata changamoto zisizo za lazima.

Kama Mzazi nataka kuwakumbusha majukumu ya wazazi na walezi katika utekelezaji wa jambo hili kwani yale ya serikali, yenyewe inayajua vilivyo na tayari imeshaanza kutekeleza kwa kutenga fedha za kugharimia elimu hiyo.

Wazazi na walezi kwa mujibu wa waraka wa serikali wanatakiwa kununua sare za shule na vifaa vya michezo,vifaa vya kujifunzia ikiwa ni pamoja na daftari na kalamu, vifaa vya usafi binafsi, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na bweni na gharama za matibabu.

Gharama nyingine kwa wazazi na walezi ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni kwa wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka na vifaa vya usafi.

Ili kuhakikisha kwamba hayo yanafanyika bila kuleta manung’uniko kwa kutumbukiza gharama zisizokuwemo katika orodha hiyo, wazazi na walezi wanatakiwa kukemea na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya mienendo inayokwenda kinyume na utaratibu wa elimumsingi bila malipo.

Kwa uhalisia wake kila mzazi na mlezi anatakiwa kuwa macho kwa kuwa msimamizi wa utekelezaji wa sera hiyo ya serikali ya elimumsingi bila malipo huku watoto wakibakiwa na jukumu la kusoma kwa bidii na uwezo waliojaliwa kwa ajili ya kujipatia ufunguo wa maisha yaani elimu. Visingizio na figisufigisu zisipewe nafasi katika hili ili tuweze kunufaika vilivyo.

Visingizio vya watoto kutokwenda shule kwa sababu ya wazazi au walezi kushindwa kumlipia ada mwanafunzi katika ngazi hizo tatu visipewe nafasi kama ilivyokuwa kabla ya utaratibu huu mpya. Kila mmoja wetu, hususan ni wazazi na walezi wajiandae kwa gharama zilizoorodheshwa ili watoto wetu wote waingie madarasani kwa kazi moja ya kujifunza. Hapa Kazi Tu sasa!
 
Back
Top Bottom