Kandarasi ya mwisho

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
Rais wetu aliwahi kusema hawapendi wanasiasa; alisema wengi wao ni waongo waongo!

Vioja vya uongo wa wanasiasa tunavyoshuhudia leo vimenikumbusha kisa cha Mwinyihaji, mtu mwaminifu na msema kweli aliyefanana na wale watakatifu tunaowasoma katika misahafu. Katika miaka arobaini yote ya utumishi kama msimamizi mkuu wa kandarasi za ujenzi kwenye kampuni ya KANJIBAI CONSTRUCTION LTD, Mwinyihaji hakupata kuiba hata mfuko mmoja wa saruji.

Wakati ambapo wasimamizi wengine walijijenga nyumba kwa saruji na nondo za kuwaibia waajiri wao. Mwinyihaji aliendelea kutumaini kuwa malipo ya uaminifu wake yagetoka kwa Mungu!

Cha ajabu, pamoja na uchapakazi na uadilifu ulioiingizia kampuni faida kubwa, Kanjibhai hakuwahi kumpa motisha wowote Mwinyihaji! Mara nyingi alimwambia tu, “Mungu bariki weye!”

Kanjibhai alikuwa tayari kutoa bonas ya kitita cha pesa kwa msimamizi mdogo aliyesimamia ujenzi wa ghorofa moja tu lakini Mwinyihaji angejenga kota nzima ya polisi na bwalo lake na kuambulia “Mungu bariki weye!”

Mwaka wa mwisho wa ajira yake kabla ya kustaafu, Kanjibhai akampa kandarasi ya mwisho kama kazi ya kuagana; ujenzi wa ghorofa kwenye ufukwe na bwawa la kuogelea kwenye ghorofa ya pili!

Ukweli kwamba, Mwinyihaji alikuwa anaelekea kustaafu bila chochote ulianza kumkosesha usingizi. Nafsi yake ikaanza kuhoji kuhusu uaminifu wake lakini zaidi lawama zisizoisha toka kwa mkewe zilimtesa zaidi.

Uzalendo ukamshinda Mwinyihaji, akaanza kuiba toka kwenye kambi ya ujenzi wa ghorofa mpya. Palipotakiwa mifuko 300 ya saruji ikapelekwa 200. Palipotakiwa nondo mia tano za milimita ishirini, zikawekwa 400 za milimita nane! Ujenzi ukakamilika lakini ubora na usalama wake ulimtia hofu sana kiasi kwamba aliwapiga marufuku watoto wake kucheza karibu na ghorofa lile. Si haba, kwa kudokoadokoa, Mwinyihaji naye akawa amejijengea kibanda cha kufichia aibu kule Mbagala Kizuiani!

Sherehe ya kuagwa Mwinyihaji ilifanywa maalum kiasi cha kumshangaza Mwinyihaji. Kanjibhai akihitimisha kusoma risala kwa niaba ya wafanyakazi alifanya kitu cha ajabu; alimwita Mwinyihaji mbele na kumkabidhi funguo za ghorofa ya ufukweni kama zawadi ya utumishi uliotukuka!

Kwa sababu tunazozijua mimi na wewe, Mwinyihaji akaanguka kama gunia na kuzimia!
Leo kwenye siasa zetu tunaanza kujionea kina Mwinyihaji wengi; wanasiasa tuliowajua kwa uadilifu na utetezi wa maslahi mapana ya Taifa lakini kwa sababu tu ya maslahi binafsi, wamegeuka kama usiku na mchana. Ni bahati nzuri kwamba Mwalimu Nyerere alituachia kipimo, alisema, wanasiasa waadilifu na wasema kweli tutawatambua kwa kuwatazama tu usoni. Wapo wengi tunaowatazama usoni leo tunashindwa kuwaamini.

Angalau basi, kisa hiki kiwakumbushe wote walioamua kufuata njia ya Mwinyihaji kuwa, mwisho wa siku nchi wanayoijenga leo ndimo watakamoishi!

Credit: James Gayo

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom