DodomaTZ
Senior Member
- May 20, 2022
- 161
- 200
Kwanza ieleweke, kampeni ni nguzo muhimu katika uchaguzi wowote wa kidemokrasia. Lengo kuu ni kuwapa wananchi fursa ya kusikiliza sera na mipango ya wagombea, ili waweze kufanya maamuzi sahihi kwa msingi wa hoja na uelewa. Ni kipindi ambacho wagombea hupata nafasi ya kuwashawishi wapiga kura kuhusu sababu za wao kuaminiwa kuongoza Taifa au jamii husika.
Pamoja na mivutano ya kisiasa inayoendelea nchini Tanzania, nimefuatilia kwa ukaribu kampeni za wagombea wa urais kutoka vyama 17 vya siasa, na nimebaini mambo kadhaa muhimu kama ifuatavyo:
Kipengele kilichoonekana wazi zaidi ni utawala wa kampeni za ahadi nyingi zisizo na uhalisia. Katika jamii iliyopevuka kifkra na kidemokrasia sera la masuala upewa kipaumbele.
Wagombea wengi wamekuwa wakitoa ahadi za kuvutia wapiga kura kama kupunguza bei za bidhaa ghafla, kuongeza mishahara, kufuta baadhi ya kodi, au kujenga miradi mikubwa ya miundombinu—bila kueleza kwa kina misingi ya kiuchumi itakayowezesha utekelezaji wake.
Hali hii inaonyesha kuwa bado siasa za sera hazijakomaa, na badala yake zimegeuzwa kuwa siasa za matakwa. Sera za aina hii zinajengwa zaidi juu ya maneno matamu na si mipango yenye utafiti na takwimu sahihi. Matokeo yake ni kudhoofisha uwezo wa wapiga kura kutofautisha kati ya sera zenye uhalisia na propaganda.
2. Majukwaa Kugeuzwa Sehemu za Mizaha na Burudani
Kipindi cha kampeni kimeonyesha jinsi majukwaa ya siasa yanavyogeuzwa kuwa maeneo ya vichekesho, nyimbo na maigizo badala ya mijadala ya kisera.
Baadhi ya wagombea na wapambe wao wamekuwa wakitumia muda mwingi kwa kejeli, utani na tambo, hali inayopunguza thamani ya kampeni kama chombo cha elimu ya uraia.
3. Kukosekana kwa Udadavuzi wa Sera na Ahadi
Kampeni za mwaka huu zimekosa mjadala wa kina kuhusu sera. Vyama vingi, hususan vya upinzani, vimeonekana kukosa mikakati thabiti ya kufafanua kwa undani sera zao mbele ya umma.
Miaka iliyopita, kulikuwa na utamaduni ambapo mgombea wa chama kimoja alipotoa ahadi fulani, wapinzani wake waliichambua kwa mapana na marefu, jambo lililosaidia kuongeza uelewa kwa wananchi. Safari hii, hali hiyo imepotea.
Sera nyingi zimesalia kuwa hotuba za majukwaani badala ya mijadala ya hoja. Udadavuzi wa sera ni muhimu kwa sababu husaidia jamii kuelewa tofauti za kiuchumi, kijamii na kisiasa kati ya wagombea. Bila mjadala wa kina, wapiga kura hujikuta wakifanya maamuzi kwa hisia badala ya hoja.
4. Upendeleo wa Vyombo vya Habari
Katika ufuatiliaji wa kina wa kampeni hizi, imebainika wazi kwamba karibia asilimia 70 ya taarifa zilizorushwa na vyombo vya habari zilihusu CCM, huku vyama vingine vikibaki pembezoni.
Hali hii inaweza kuelezwa kuwa ni kutokana na nguvu ya kifedha na kimfumo ya chama tawala, lakini haiondoi wajibu wa vyombo vya habari kudumisha usawa. Mijadala huru ya kisera kupitia televisheni na redio imepungua ukilinganisha na chaguzi zilizopita, jambo linalodhoofisha uelewa wa wapiga kura.
Kwa mfumo wa vyama vingi, vyombo vya habari vinapaswa kuwa majukwaa ya usawa. Mwaka huu, vimeonekana kuelemea upande mmoja, hali inayoweza kupunguza imani ya umma katika mchakato wa uchaguzi. Vyombo vya habari vya kijamii pia havikutoa tofauti kubwa; vingi vilionekana kuunga mkono vyama fulani bila kutangaza wazi msimamo wao.
Kuna hoja zinazodai kuwa uchaguzi wa mwaka huu una ushindani mkali, lakini kwa uhalisia ushindani huo hauonekani kuwa wa kiwango cha kuipa CCM changamoto kubwa.
Mgombea wa CCM ameweza kufanya mikutano mingi zaidi nchini, akisaidiwa na mtandao mpana wa chama na viongozi wastaafu. Vyama vingine vingi vimekumbwa na changamoto za kifedha na ukosefu wa miundombinu ya kisiasa, hivyo kushindwa kufanya kampeni zenye uwiano kitaifa.
Ukosefu huu wa ushindani wa kweli unadhoofisha demokrasia kwa kupunguza hamasa ya wananchi kushiriki uchaguzi, na kuwafanya wapiga kura kutofautisha wagombea kwa hoja za kisera.
Kukosekana kwa wagombea Urais kwa tiketi ya Vyama vya Chadema na ACT Wazalendo kunaacha pengo kubwa kwenye kampeni za mwaka huu, licha ya uwepo wa wagombea 17 uenda kukawepo na kundi kubwa ambalo litakosa chaguo mbadala zaidi ya CCM.
Kuna kubwa la watu hasa maeneo ya pembezoni hawafahamu majina ya wagombea tofauti na Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea kwa tiketi ya CCM. Lakini kukosekana kwa wagombea kutoka kwenye Vyama hivyo kunaacha ombwe la taarifa ambazo zingeweza kuchochea uamuzi sahihi kwa baadhi ya wapiga kura.
Masuala nyeti kama uwajibikaji wa watumishi wa umma na viongozi, haki za binadamu, utawala bora, na vita dhidi ya rushwa hayajapewa uzito mkubwa unaostahili katika kampeni za mwaka huu licha ya kutajwa sana na wananchi kama sehemu kubwa ya mambo yanayowatatiza.
Badala yake, mjadala umejikita zaidi katika miradi mikubwa na masuala ya miundombinu, huku changamoto za msingi kama usalama wa wananchi, utawala wa sheria, na usawa katika huduma za kijamii zikishindwa kuwekwa mbele katika kampeni.
Kutotoa uzito kwa masuala haya kunadhihirisha mtazamo wa “kushinda uchaguzi” badala ya “kujenga taifa.” Wananchi walitarajia kuona mijadala yenye dira ya maendeleo jumuishi, ikiwemo mbinu za kubana matumizi ya serikali na kuhakikisha usawa wa kijamii.
Hitimisho
Kwa ujumla, kampeni za mwaka 2025 zimeonesha haja kubwa ya kuimarisha utamaduni wa mjadala wa kisera nchini. Vyombo vya habari vinapaswa kurudisha imani ya umma kwa kutoa usawa wa taarifa, huku taasisi za kiraia zikihimizwa kushiriki kikamilifu katika elimu ya uraia.
Demokrasia imara haiwezi kujengwa kwa misingi ya ahadi tamu na ushabiki pekee, bali kwa mijadala ya hoja, uwazi, na uelewa wa sera zinazogusa maisha ya wananchi.