Kamati za Rais kuhusu makanikia: Uchambuzi wa Luqman Maloto

Mbase1970

JF-Expert Member
Jun 11, 2015
6,056
2,000
Report ya Kwanza:

HONGERA RAIS MAGUFULI ILA SISHANGILII GOLI LA KUONGOZA
Taifa linashangilia matokeo ya Kamati Maalum ya Rais ambayo Rais John Magufuli aliiunda kuchunguza mchanga kutoka kwenye migodi ya Tanzania ili kubaini kiasi cha madini kinachokuwemo.
Kamati imecheua leo! Uchunguzi wa Kamati umeonesha kuwa kwa takriban miaka 19 Tanzania imekuwa ikipigwa na wawekezaji wanaochimba madini.
Mabilioni mpaka trilioni kila mwezi taifa linaibiwa na wawekezaji kupitia sababu kwamba nchi haina uwezo wa kufunga mashine za uchenjuaji wa mchanga kutoka migodini.
Kwa sababu hiyo basi, makontena ya mchanga husafirishwa kwenda nje kwa ajili ya kuchenjuliwa. Matokeo yake idadi ya madini ambayo hutangazwa kupatikana baada ya uchenjuaji nje ya nchi ni kidogo mno ukilinganisha kilichoelezwa na ripoti ya Kamati ya Rais.
Matokeo ya jumla ni kwamba nchi inakosa mapato mengi. Hili la nchi kukosa mapato linapaswa kumshtua kila mmoja. Wawekezaji wamekuwa wakifanya udanganyifu mwingi kuinyima nchi mapato.
HONGERA RAIS MAGUFULI
Ni hapa sasa ni lazima kumpongeza Rais Magufuli kwa nia yake njema. Kuteua kamati ya kuchunguza mchanga unaosafirishwa nje ni jambo ambalo limefichua ambayo wengi walikuwa hawajui kwa usahihi.
Rais Magufuli anastahili pongezi zaidi kwa sababu mchanga kutoka kwenye migodi yetu imekuwa ikisafirishwa kwenda nje tangu mwaka 1998. Miaka yote 19 nchi ina wataalam na viongozi lakini hakuna hatua iliyochukuliwa kujua kiasi mwafaka cha madini yanayokuwemo ndani ya mchanga (makanikia).
Alichokifanya Rais Magufuli, kilipaswa kufanywa na mamlaka za usimamizi wa uchimbaji wa madini nchini amabazo zimekuwepo miaka yote hiyo. Hata hivyo, hakukuwa na utashi.
Rais Magufuli anao utashi na amejaliwa ujasiri wa kuthubutu. Rais Magufuli si mpokea maneno, bali hujitahidi kufuatilia mwenyewe. Anapotaka lake, atalihangaikia mpaka aone mwisho wake.
Ni hulka hiyo ya Rais Magufuli ambayo leo hii imewezesha majibu kupitia Kamati aliyoiunda, juu ya idadi ya madini na aina zake ambayo nchi ilikuwa inaporwa na wawekezaji wa sekta ya madini kupitia sababu ya nchi kutokuwa na uwezo wa kuchenjua.
Mwanamke mjasiriamali wa Marekani, Amy Rees Anderson, husema: “A person who feels appreciated will always do more than what is expected.”
Kiswahili: Mtu anayejiskia kuthaminiwa kwa anachofanya mara zote hufanya zaidi ya matarajio.
Hivyo, pongezi zielekezwe kwa Rais Magufuli kuonesha kuthamini kile anachokifanya kwa nchi. Bila shaka naye anapoona Watanzania wenzake wanathamini yale mema anayofanya, basi atafanya zaidi kuliko matarajio ya wananchi kwa wingi wao.
TUSIUVUKE UKWELI
Ukweli ubaki kwenye vipimo vyake! Ni kwamba malalamiko ya mchanga kusafirishwa kwenda nje hayajaibuliwa wakati wa Rais Magufuli. Yalikuwepo na watu wengi walipiga kelele kuwa dhahabu nyingi inaibiwa kupitia mchanga unaosafirishwa kwenda nje kwa ajili ya kuchenjuliwa.
Kwa mantiki hiyo, ushujaa wa Kamati Maalum ya Rais haupo kwenye kubaini kama wawekezaji walikuwa wanaiba au la! Ushujaa upo kwenye kubaini kiasi cha madini na mapato ambayo taifa lilikuwa linapoteza.
Kwa sasa, angalau yapo makisio kuwa kati ya Sh600 bilioni mpaka zaidi ya Sh1 trilioni, nchi ilikuwa inapoteza kupitia kuwaamini wawekezaji wanaosafirisha mchanga kwenda kuuchenjua kisha wao wenyewe kutamka kiasi na aina ya madini ambayo hupatikana.
Tena, hasara kubwa kwa nchi ipo kwenye dhahabu, maana thamani yake ni kubwa na kwa mujibu wa ripoti ya Kamati Maalum ya Rais, kiasi kilichokuwa kikitajwa na wawekezaji ni pungufu zaidi kwa mara 10 ya kile ambacho wamekibaini ndani ya kila tani moja ya mchanga.
Kwa miaka mingi Watanzania walikuwa wanaambiwa kama wimbo kuwa dhahabu yao na madini mengine wanaibiwa kupitia mchanga, lakini hawakuwa wakijua ni kiasi gani hicho.
Hivi sasa wanaelewa japo kwa tarakimu za makadirio kuwa mabilioni mpaka trilioni zimekuwa zikiwanufaisha wawekezaji wakati madini ni mali ya Watanzania. Wenye mali yao hawanufaiki inavyotakiwa.
SIWEZI KUSHANGILIA
Wengi wanashangilia, lakini mimi siwezi kufanya hivyo. Nampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake lakini najiweka kando na ushangiliaji wa mapema. Maana wapo wengi walishangilia mwanzoni lakini mwisho wakabaki wanaduwaa.
Binafsi naisubiri kwanza ripoti ya Kamati ya pili ambayo iliundwa na Rais Magufuli kwa ajili ya kufuatilia masuala ya mikataba na mambo ya kisheria. Hiyo ndiyo naitaka.
Suala la usafirishaji wa mchanga kwenda nje lipo kisheria na nchi ilisaini mikataba kuridhia mchanga uwe unasafirishwa.
Kuzuia jambo hilo inatakiwa sheria zifuatwe. Siyo tu kwa sababu umebaini kuwa wawekezaji wanaiba ndiyo utoe uamuzi wa kuzuia mchanga usisafirishwe bila kufuata utaratibu. Hapana, sheria lazima zifuatwe!
Ukiwa na nyumba, ukapangisha wapangaji halafu wakawa wanakulipa fedha ambazo mmekubaliana kwenye mkataba, kisha baadaye ukagundua kiasi wanachokulipa ni kidogo kulinganisha na thamani ya nyumba yako, hutakiwi kufika na kuwatolea wapangaji vifaa vyao nje.
Kuna mawili, ama kuvumilia mikataba iishe ili baada ya hapo usifanye makosa mengine au kuwaita wapangaji wako mezani mjadili na kukubaliana waongeze fedha kulingana na thamani halisi. Hilo la pili linategemea uungwana na utashi wa mpangaji.
Kama utaamua kuvunja mkataba, unaweza kujikuta unawalipa wapangaji wako fedha nyingi na kuingia hasara kubwa kuliko ambayo ungeivumilia. Nyumba yako, kodi unapunjwa wewe lakini fidia utalipa wewe. Hiyo ndiyo tabia ya mkataba.
Ni vizuri kutambua kuwa Watanzania waliosaini mikataba inayowapa upendeleo mkubwa wawekezaji katika rasilimali za Watanzania, hao ndiyo wasaliti wakubwa. Mfanyabiashara yake ni faida, akiona upenyo wa kukuibia ili atengeneze faida kubwa atakuibia tu!
Kwa maana hiyo, wataalamu wa Kitanzania ambao wamekuwa wakipewa dhamana ya kuchunguza na kushauri kabla ya nchi kuingia mikataba, hao ndiyo wasaliti. Wataalamu ambao wana dhamana ya kuhakiki kiwango cha madini yanayochimbwa nchini na kuhakikisha nchi inapata mapato stahiki, hao ndiyo wasliti.
Hata hivyo, kushughulika na usaliti wa Watanzania wanaoihujumu nchi kwa maslahi ya wawekezaji, inahitaji akili kuliko hisia, inahitaji subira kuliko pupa, vinginevyo ni hasara kubwa.
Hii ndiyo sababu nimesema kuwa nasubiri ile Kamati ya pili ambayo Rais Magufuli aliiunda. Je, itakuja na mapendekezo gani ya kisheria? Hapo ndipo tutapata mwanga.
Mimi nitakuwa wa mwisho kushangilia. Maana nitashangilia baada ya kulimaliza suala hili salama, bila kuingia kwenye mzigo wa madeni. Nitashangilia nitakapoona kuwa mwanga umepatikana na nchi inakwenda kupata kile ambacho inastahili kupitia madini yake.
Hali ni mbaya, tuendako nchi inaweza kubaki mashimo matupu na madini yote yatakuwa yamekwisha. Wawekezaji hawana huruma, wao wanavuna Tanzania kisha wanakwenda kujenga kwenye mataifa yao. Wasaliti ni wataalamu wa Kitanzania ambao wamekuwa daraja la wawekezaji kuwanyonya Watanzania.
KWA NINI SISHANGILII?
End justifies the means! Ndivyo wenye Kiingereza chao husema, wakiwa na maana kuwa mwisho ndiyo huhalalisha njia. Je, njia inayotumika ni sahihi? Matokeo ya mwisho hutoa majibu kamili.
Nami nasubiri nione mwisho wa hili suala la mchanga ili nipate mantiki. Ikiwa chanya nitashangilia kama zuzu, lakini mambo yakiwa hasi, nitakuwa nimetunza heshima yangu kwa kutoshangilia goli la kuongoza na kuamini ushindi tayari, wakati ndiyo kwanza dakika ya 15 kipindi cha kwanza, bado dakika 75.
Tunakubaliana wote kuwa Rais Magufuli anastahili pongezi kwa kutoa mwanga. Sasa tuone ripoti ya wanasheria. Kama upo uwezekano wa kuvunja mikataba na kubaki salama, basi ivunjiliwe mbali. Kama ni vigumu, subira na hekima vichukue mkodo wake.
Huko nyuma taifa limewahi kushangilia goli la kuongoza pale Rais Magufuli akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alipokamata wavuvi kutoka China na meli ya samaki waliogawiwa bure. Kuna walioshangilia kitoweo kupitia Samaki wa Magufuli.
Watu walishangilia hasa kana kwamba ushindi tayari, kumbe lilikuwa tu goli la kuongoza. Dakika 90 zilipowadia, Serikali ya Tanzania ikajikuta kwenye deni kubwa la kulipa samaki, meli ya Wachina iliyokosa uangalizi na kuzama Dar es Salaam pamoja na faini.
Ukifuatilia unaona kuwa dhamira ilikuwa njema kabisa, maana wale wavuvi walikuwa wanavua Tanzania sehemu ya maji ya kina kirefu. Mambo yalipokwenda kwenye sheria, hali ikawa mbaya kwa nchi.
Unakumbuka mkataba wa Richmond Development LLC mwaka 2006? Taarifa zote zilionesha kuwa nchi ilipigwa na wajanja. Mkataba huo ukahamishiwa kwa Kampuni ya Dowans Holding kinyemela.
Mkataba ulikuwa mbaya na ilithibitishwa kuwa wataalamu wa Kitanzania walitumika kusaidia upigaji. Ushauri ukawa kwamba mkataba uvunjwe. Kweli ukavunjwa.
Matokeo ya kuvunja mkataba huo yakawa Tanzania kudaiwa fedha karibu Sh100 bilioni baada ya kushindwa kesi mahakamani. Na zililipwa!
Hii ndiyo sababu katika suala hili la mchanga najiweka kando kushangilia goli la kuongoza. Mpaka sasa kweli nchi ipo kifua mbele dhidi ya wawekezaji. Rais Magufuli anatakata. Watanzania wapo juu kwa hoihoi na vifijo.
Je, dakika 90 za sakata la mchanga zitakapokamilika tutakuwa salama? Je, tutakuwa tunaendelea kushangilia? Maswali hayo mawili ndiyo ambayo yananifanya ninyamaze kwanza. Niishie tu kumpongeza Rais Magufuli na wajumbe wote wa kamati waliofanya kazi kubwa. Kushangilia hapana!
Tatizo naogopa sana mikataba, iwe imeingiwa kimakosa au kiusahihi lakini mwisho inabaki kuwa mikataba. Hivyo kushughulika nayo, inatakiwa hekima na weledi wa hali ya juu.
Mchanga ni wa Watanzania na wanaobiwa ni Watanzania lakini umakini ukikosekana katika suala hili, watakaodaiwa ni haohao Watanzania, kama walivyolipishwa samaki na meli wakati ni wao waliokuwa wanaibiwa au walivyolipa Dowans, huku ni wao walioibiwa.
Ndimi Luqman MALOTO

Report ya Pili


WELEDI
Nilichokishuhudia wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya pili ya tume ya wataalamu wa sheria na uchumi kuhusu suala la mchanga wa madini (makanikia), nakiweka katika neno moja tu; Weledi.
Naam, weledi katika hasi na chanya.
CHANYA
Tume ya pili imebainisha masuala yenye kuhusu sakata la makanikia kwa weledi wa hali ya juu.
Uwasilishaji wake ni wa kitaalamu na hata ushauri (mapendekezo), umetolewa kisomi.
Jukumu lililobaki ni Serikali kufanyia kazi kisha tuone matokeo.
Pamoja na hayo yote, jazba iwekwe kando kisha weledi uchukue nafasi wakati wote wa kushughulikia suala la makanikia.
Ni kweli tumeibiwa sana ila tuwakabili wezi kwa akili na utaalamu wa kutosha. Tusije kuwapa nafasi ya kupumua, wakapata eneo la kutubana. Tutakuja kuwatambua.
Majibu ya Rais Magufuli kwa ripoti yamekuwa mazuri sana. Alionesha weledi kama mkuu wa utawala.
Rais Magufuli ameridhia mapendekezo ya kufanyika mabadiliko ya sheria ya madini. Amekubali sheria kupelekwa bungeni ili Bunge lifanye mabadikiko. Jambo jema sana.
HASI
Uwepo wa Spika wa Bunge wakati wa kupokea ripoti haukuwa na afya. Nchi ipo kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017-2018, Spika wa Bunge yupo Dar kushuhudia Rais akikabidhiwa ripoti.
Spika wa Bunge anapaswa kuwepo Dodoma, kuongoza Bunge ili lifanye kazi yake vizuri ya ama kupitisha au kuikataa Bajeti, Spika yupo Dar kushuhudia tu ripoti ikikabidhiwa kwa Rais. Hii siyo sawa.
Kauli ya Rais kumtaka Spika alisimamie Bunge kufanya mabadiliko ya sheria ni njema kwa nchi lakini haikuzingatia weledi wa dola.
Rais hapaswi kuonekana analiagiza Bunge, maana Bunge ni mhimili huru na jukumu lake ni kuisimamia Serikali. Tafsiri yake ni kuwa Spika anaongoza chombo kinachopaswa kuisimamia kazi ya Rais Magufuli.
Upo utaratibu wa Serikali kuwasilisha muswada bungeni, siyo Rais aseme kumwambia Spika kuwa waongeze wiki moja. Hiyo ni rushwa ya dola.
Kauli ya Rais Magufuli kumtaka Spika atimue wabunge 'wakosoaji' ili wakiropoka nje washughulikiwe na Serikali haikuzingatia weledi wa dola.
Uwepo wa Waziri wa Fedha katika makabidhiano ya ripoti, wakati Bunge lipo kwenye mjadala wa Bajeti, haukuwa uamuzi sahihi. Waziri anapaswa kuwepo bungeni kusikiliza michango ya wabunge. Ripoti ya Makanikia pamoja na umuhimu wake mkubwa, lakini haipaswi kuzuia shughuli nyingine nyeti kwa nchi.
Uwepo wa Kaimu Jaji Mkuu pia haukuzingatia weledi wa mgawanyiko wa mihimili ya dola. Sakata la makanikia linahusu masuala ya sheria za mikataba.
Ikiwa wawekezaji wataona hawajatendewa haki na kuishitaki Serikali kwa mahakama ya hapa nchini, maana yake hiyo kesi itakuwa chini ya Kaimu Jaji Mkuu ambaye naye alikuwepo kupokea ripoti hiyo.
Hakukuwa na ulazima wowote wa Kaimu Jaji Mkuu kuwepo. Angeshuhudia kwenye TV na hakuna ambacho kingepungua. Uwepo wa Kaimu Jaji Mkuu unaathiri mazingira ya Mahakama kutenda haki ikiwa watuhumiwa watakimbilia mahakama ya nchini.
Rais Magufuli ametaka yawepo mazungumzo kati ya Serikali na Acacia, kwamba Acacia wakikubali makosa ndipo wapewe masharti ya kuendelea na kazi.
Hilo ni kosa. Serikali inatakiwa kuwapeleka Acacia mahakamani ili Mahakama itafsiri sheria na kutoa haki, siyo tena kufanyika mazungumzo pembeni.
HITIMISHO
Pongezi kwa kamati, kazi nzuri imefanyika. Pongezi kwa Rais Magufuli, ameonesha dhamira njema ya kuitetea nchi dhidi ya wizi wa rasilimali zetu.
Ndimi Luqman MALOTO

Kutoka facebook page ya mchambuzi na mwandishi Luqman Maloto.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom