kama ulienda shule pita hapa

Kashindi

JF-Expert Member
Oct 28, 2011
349
250
Shule zafunguliwa watoto kuhudhuria
Wakubwa kwa wadogo maarifa kujipatia
Pekupeku twaenda na kamasi zikitutoka
Yeye atukumbatia bila kujali twamchafua
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

La pili tumefika na nyimbo atuimbisha
Adabu atufundisha wakubwa kuwaamkia
Methali atuambia vitendawili kutegua
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

La saba twamaliza sherehe kutufanyia
Wengi twamuudhi tabasamu atupatia
Chini atuweka mengi kutushauria
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Kidato cha nne twamaliza rabana atujalia
Juhudi kaonesha maarifa katuzawadia
Si mchoyo asilani ya kwake katugawia
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Twamaliza cha sita kidato nakuambia
Usiku akesha masomo kutuandalia
Aamka mapema darasani anaingia
Atusisitiza tusome marks kujipatia
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Mlimani nimefika msomi nimekua
Udaktari nasomea ualimu pia sheria
Bado anipenda na madesa kunipatia
Bega yuko na mimi njia kunisafishia
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Sasa mtawala mshahara nampangia
Nampa kisichoridhisha na masimango pia
Apigwa na wamkoa wa wilaya simwachi nyuma.
Wengi wafurahia kumwona mwalimu alia
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Afuta machozi darasani mapema kuingia
Nyumba anayolalia hata ndege amsikitikia kampeni aambiwa kompyuta atampatia
Waacha ya msingi mishahara kumbania
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Mengi nimesema naamini mwanisikia
Taifa alijenga kwa nguvu na maarifa pia
Heshima tumpatie kwa mola kumuombea
Hakuna kama mwalimu jamii yote yajua.

Mtunzi..
.Mwalimu Emanuel Kashindi
Mhitimu chuo kikuu UDSM.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom