KAGERA: Waziri wa Ardhi,William Lukuvu apokewa na mabango kila kona

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepokewa kwa mabango na wakazi wa kijiji cha Rwakalemela Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, huku wakimuomba kutatua migogoro ya ardhi unaowakabili.

Wananchi hao walitoa ombi hilo jana baada ya waziri huyo kufika wilayani hapa akitokea Karagwe, akiwa katika ziara ya utendaji mkoani Kagera.

Lukuvi baada ya kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya, alianza kusikiliza kero za wananchi kuhusu migogoro ya ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Rwakalemela.

Wananchi hao waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kutaka migogoro ya ardhi itatuliwe, wengi walimuomba waziri huyo kuwafutia hati miliki wenye mashamba makubwa walioyapata bila kufuata utaratibu.

Mmoja wa wananchi hao, Amiri Rashidi alisema baadhi ya wananchi waliowahi kuwa viongozi wa chama, Serikali na wenye uwezo wa fedha walijimilikisha maeneo makubwa katika kata za Kasulo, Kabanga na Rulenge na kusababisha wananchi wengi kukosa mashamba.

Kitendo cha Rashidi kuzungumza huku akitokwa na machozi, kilimwamsha kwenye kiti ofisa ardhi Wilaya ya Ngara, Betty Munuo kutoa maelezo.

Munuo alisema mzee huyo eneo lake alilimiliki mwaka 1969 lakini ilipofika 1985, lilichukuliwa na kuwa kituo cha kuegesha magari.

“Huyu anastahili kulipwa tangu mwaka 1985 na ofisi ya mkurugenzi ambayo haijatekeleza maagizo ya mahakama,” alisema Munuo.

Baadhi ya wananchi waliwataja vigogo waliojimilikisha mashamba, ambao kutokana na kutowapata kusikiliza upande wao yamehifadhiwa.

Awali mbunge wa Ngara, Alex Gashaza alisema migogoro ya ardhi wilayani hapa ni mingi na wenye uwezo ndiyo wanaowanyanyasa maskini.

Katika ufafanuzi wake, Lukuvi alisema Serikali inafanya mpango wa kurekebisha utaratibu wa kutatua migogoro ya ardhi kwa kubadilisha mfumo wa mabaraza ya ardhi kila kata.

“Migogoro ya ardhi ambayo imefikishwa mahakamani waziri hana mamlaka ya kuingilia, lakini naagiza mwanasheria wa halmashauri hakikisha wajumbe wa mabaraza ya ardhi ambao siyo waaminifu wanaondolewa ili haki iweze kutendeka,” aliagiza Lukuvi.

Alisema Ngara haina ofisa wa kutoa hati ya ardhi hivyo Serikali itahakikisha anapelekwa ili kusimamia mipango ya upimaji viwanja na kutatua migogoro inayojitokeza.

Lukuvi alisema katika utaratibu aliouanzisha wa ‘Funguka kwa Waziri’ wilayani Ngara amepokea kero 101 na atasikiliza kila mmoja apate haki anayostahili.

Katika hatua nyingine, Lukuvi aliagiza mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara kufanya uchunguzi wa ardhi ilipojengwa Shule ya Msingi Murugwanza ili aliyekuwa akimiliki eneo hilo, Zedeki Kadyamasaka alipwe fidia.


pic+lukuvi.jpg


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom