JPM Agusa Jipu BoT-Source Mtanzania

Shebbydo

JF-Expert Member
Feb 12, 2015
1,174
1,937
JPM agusa jipu BoT
SHARE THIS

TAGS
* Azuia hundi bil. 900/- zilizokuwa katika hatua ya Mwisho kuchotwa

* Fedha hizo ni karibu ya mukusanyo ya kodi ya mwezi mzima ya TRA

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amesitisha utoaji wa Sh. bilioni 925 zilizokuwa zimeidhishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni ya Serikali.

Mbali na hilo, Rais Magufuli ameagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho awali kilikuwa chini ya BoT na baadaye kupelekwa wizarani, kirejeshwe mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.

Rais Magufuli alitoa uamuzi huo jana Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kushtukiza BoT na kusitisha ulipaji huo wa fedha ambazo tayari zilikwishaidhinishwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari jana, ilisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo katika kikao chake na watendaji wakuu wa benki hiyo, wakiwamo Gavana Mkuu Profesa Benno Ndulu, naibu wake, Julian Banzi, wakurugenzi na mameneja wa BoT.

Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa malipo hayo yalikuwa yameidhinishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali ambapo rais aliagiza fedha hizo zirejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki upya.

“Rais Magufuli alifanya ziara hiyo jana ambapo hadi anatoa agizo hilo, BoT ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo hayo ya Sh. bilioni 925 ambazo wizara ilitoa idhini ya kufanyika malipo.

“Ameagiza yarejeshwe katika wizara ili ifanye upya uhakiki wa malipo hayo kubaini walengwa walioidhinishiwa kulipwa iwapo wanastahili kulipwa ama vinginevyo,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.

Kiasi hicho cha fedha kilichozuiwa na rais kinakaribia kufikia makusanyo ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kilichokusanywa Februari, mwaka huu – Sh. trilioni 1.040.



HABARI ZA NDANI

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata jana jioni kutoka kwenye chanzo chake, zinasema fedha hizo zilikuwa zimeelekezwa kulipa madeni mbalimbali ya taasisi za Serikali na binafsi.

“Malipo mengi yapo kwenye taasisi ambazo zinatoa huduma serikalini na cheki zao zimerundikana pale wizarani, jambo la kujiuliza kwanini wizara iidhinishe malipo wakati hayako kwenye bajeti.

“Hivi tujiulize wote kama tunaipenda nchi yetu, hivi kweli kwa mtindo huu mwananchi wa kawaida atapata huduma za kijamii,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema BoT na wizara wametakiwa kufuata waraka uliotolewa mwaka 2004 unaotoa mwongozo wa malipo.



AGIZO KWA GAVANA

Aidha taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli pia amemuagiza Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa benki hiyo na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwapo.

“Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati kazi wanazofanya hazijulikani.

“Maswali ninayoyauliza ni ‘very technical’, yapo mengine siwezi kuyataja hapa ‘and I know what iam doing’. Myafute majina yote ya watu ambao si wafanyakazi wa BoT ili mshahara uende kwa watu wanaofanya kazi hapa,” alinukuliwa Rais Magufuli katika taarifa hiyo, huku ikiweka wazi kwamba hadi jana BoT ilikuwa na jumla ya wafanyakazi 1,391.

Ziara ya jana ni ya pili tangu Dk. Magufuli alipoapishwa kuwa rais Novemba mwaka jana ambapo alitembelea ofisi hizo akitokea Ikulu kwa miguu na kubaini kuwapo utoro ofisini kwa baadhi ya wafanyakazi wa Hazina.

Ziara kama hiyo pia aliifanya Novemba 9 mwaka jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alijionea idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wamelala chini kutokana na ukosefu wa vitanda ambapo alifanya mabadiliko ya uongozi kwa kumuhamisha aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dk. Hussein Kidanto na kumteua Profesa Lawrence Museru kusimamia nafasi hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alielezwa na baadhi ya wagonjwa adha wanazozipata wakati wanasubiri vipimo vya MRI na CT-Scan ambavyo vilikuwa vimeharibika tangu mwishoni mwa Agosti mwaka jana.

Hadi sasa Serikali yake imewasimamisha kazi zaidi ya watumishi 700 na kuagiza vyombo vya dola na usalama kuwafanyia uchunguzi ambapo baadhi wanadaiwa kuikosesha mapato Serikali na kuisababishia hasara.

Katika mlolongo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye amekuwa akifanya ziara za ghafla katika maeneo mbalimbali ambako amekuwa akiibua ufisadi mkubwa.

Mapema Desemba mwaka jana, Majaliwa aliibua upotevu wa makontena 2,431 yaliyokuwa yametolewa Bandari ya Dar es Salaam na kupelekwa katika Bandari Kavu bila kulipiwa kodi.

Katika sakata hilo watumishi wapatao 15 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kukamatwa kwa watumishi hao kulitokana na ukaguzi uliobaini upotevu wa makontena 11,884 katika bandari kavu saba, ambapo pia magari 2,019 yalitolewa bila kulipiwa ushuru.

Wakati makontena hayo ushuru wake ni zaidi ya Sh. bilioni 47, ushuru wa magari uliokwepa ni zaidi ya Sh. bilioni 1.072.

Tangu alipoapishwa, Rais Magufuli amekuwa akishikilia msimamo kwamba atasimamia katika kupunguza matumizi ya Serikali, kubana mianya ya rushwa na ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo vyake vya ndani.

Ahadi ya utumbuaji majipu, Rais Magufuli aliitoa katika hotuba yake ya kwanza kwa Bunge la 11 mjini Dodoma mwanzoni mwa huu.

Hivi karibuni Rais Magufuli alinukuliwa akisema kwamba iwapo atashindwa kusimamia masuala hayo kwa kuhakikisha kuwa ‘anatumbua majipu’, ni bora akaenda kulala nyumbani kwake kwani atakuwa hastahili kuitwa rais.
 
Back
Top Bottom