JKCI Kinara Afrika upasuaji moyo

JKCI Kinara Afrika upasuaji moyo

diana chumbikino

JF-Expert Member
Joined
May 29, 2018
Posts
428
Reaction score
368
676_jakaya-kikwete-cardiac-institute_thb.jpg
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeibuka kinara kwenye hospitali za moyo barani Afrika kwa kufanya idadi kubwa ya upasuaji wa moyo . Mwaka jana imewafanyia upasuaji wagonjwa 1,356. Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji JKCI, Dk Mohamed Janabi wakati akimkaribisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipoenda kukagua wodi ya watoto iliyomalizika kujengwa kwenye hospitali hiyo. Dk Janabi amesema, idadi hiyo ni kubwa kuwahi kufanywa na hospitali yoyote ya moyo Afrika kwa mwaka jana, huku akibainisha kuwa imejipanga kwa mwaka huu na miaka ijayo kuendelea kutoa huduma bora zaidi ndani na nje ya nchi


. Amesema kwenye wagonjwa waliofanyiwa upasuaji kwa njia ya kupasua kifua ni 316 huku waliofanyiwa kwa njia ya tundu dogo ni 1,000 na kuongeza kuwa kazi hiyo imefanyika kwa ufanisi mkubwa. Alisema licha ya kuvunja rekodi hiyo lakini pia imekidhi kwa kiasi kikubwa kiwango cha kimataifa kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusiana na idadi ya vifo kwa wagonjwa wa moyo, kiwango cha kimataifa kinasema kusiwe na vifo zaidi ya asilimia 13 kwa wagonjwa ambapo JKCI imepata vifo vya asilimia 5 tu.

Akizungumzia kuhusiana na wodi hizo mpya za watoto Dk Janabi alibainisha kuwa imeiongezea hadhi JKCI ambapo imekuwa ni pekee kwa Afrika Mashariki na Kati kuwa na huduma bora za moyo kwa watoto. Alisema ujenzi wa wodi hiyo ya kuhudumia watoto peke yake ni hatua kubwa na ya kimafanikio kwenye utoaji wa huduma ya tiba ya moyo huku akibainisha kuwa kwenye nchi nyingine watoto wanachanganywa na watu wazima kwenye wodi moja na kusema kuwa hiyo sio sawa.

Dk Janabi alibainisha kuwa kwa kuwalaza watoto na watu wazima pamoja inaweza kuwaathiri watoto hao kutokana na kuwa wanahitaji ukaribu zaidi wa wazazi au walezi na hivyo kuwa kwenye wodi za pamoja na wagonjwa wakubwa wanaweza kukosa huduma hiyo kiufanisi. Alisema“mheshimiwa Waziri ninapenda kwanza kuipongeza serikali na Taasisi hii ya Baps Charities ambapo kwa pamoja wamefanikisha ujenzi wa wodi hizi za watoto za kisasa kabisa, na ni imani yangu na Taasis nzima kuwa itatoa huduma nzuri kwa watoto.” Kwa upande wake, Waziri Ummy alibainisha kuwa kutokana na harakati zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuwahudumia wagonjwa wa moyo nchini, Rais John Magufuli ameamua kuipatia Sh milioni 500.

Alisema, JKCI ni mfano wa kuigwa kwa kuwa uongozi wake umekuwa mstari wa mbele kutafuta vyanzo vya mapato na kusaidia upatikanaji wa huduma bora za moyo. Alisema awali taasisi hiyo ilikuwa ikiwafanyia upasuaji watoto 20 kwa siku na ujenzi wa wodi hiyo unaiwezesha kuwafanya upasuaji watoto hadi 40 huku akibainisha kuwa wodi hiyo itawawezesha wataalamu wengi zaidi wa tiba ya moyo kwa watoto kufanya kazi. Alisema serikali inaangalia uwezekano wa kupanua huduma ya utoaji wa tiba ya moyo kwenye hospitali ya Mloganzila kwa kuanzisha huduma za JKCI huku akibainisha kuwa inaweza huduma za moyo kwa watu wazima ikahamishiwa huko au ya watoto.

“Serikali inaona harakati mnazofanya za kutibu moyo na tena kwa ufanisi wa hali ya juu, awali ilikuwa ni lazima watoto au watu wazima wasarishwe kwenda nje ya nchi lakini kwa sasa asilimia kubwa upasuaji unafanyika hapahapa nchini, na Rais Magufuli akaona hapana ni lazima awawezeshe ili kazi iwe bora zaidi na zaidi”amesema. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasis inayosaidia tiba ya moyo kwa watoto ya Save a Child Heart, Simon Fisher alibainisha kuwa taasisi hiyo itaendelea kusaidia watoto nchini huku akimhakikishia Waziri kuwa itawaendeleza kimasomo wataalamu wa hapa nchini.
 
Kwa namna watanzania wanavyotumia mioyo yao vibaya ulikuwepo umuhimu kabisa wa kuwa na kitengo hicho.

Mtu anatumia moyo kuwaza siasa, ujue ni utumiaji mbaya wa mioyo.
 
Back
Top Bottom