Mkuu fikirikwanza,
Naunga mkono hoja! Kiukweli jimbo la Busega na jirani yake Magu (kwa dr. Festus Limbu) yamekosa wawakilishi makini kwa miongo kadhaa sasa. Kibaya zaidi siasa za ndani ya ccm katika majimbo haya zimegubikwa na fitina, chuki, ushirikina na kutishiana maisha zaidi kuliko kuwatumikia wananchi waliowachagua. Kwa mara ya mwisho anglau majimbo hayo yalikuwa na wawakilishi wakati wa marehemu Ernest Kisumo Nyanda (Busega) na marehemu Malaki Levi Lupondije (Magu). Baada ya hapo kwa kweli, hatujawahi kupata wawakilishi bungeni.
Sasa ni wakati muafaka kwa wana Busega na Magu kufanya mabadiliko ya kweli kwa maendeleo ya majimbo haya, na Taifa kwa ujumla. Inasikitisha kuona rasilimali nyingi katika maeneo haya lakini wananchi wanaishi katika umaskini mkubwa huku huduma muhimu za jamii zikiwa katika hali mbaya sana. Wakati serikali inapeleka maji kutoka ziwa victoria kwenda miji ya shinyanga na kahama, wananchi wengi wa Magu na Busega hawana maji safi na salama katika vijiji vyao. Wengi wao wanakunywa na kufanya shughuli za usafi ziwani, kitu ambacho ni hatari kwa afya zao. Wakati wa kiangazi kuna wananchi wanaolazimika kutembea kilometa kadhaa kufuata ndoo moja ya maji ziwani na kufanya shughuli za usafi huko. Wabunge wetu wanaishi Dar es Salaam! Wakienda Dodoma wanadai walipwe laki 200 maana maisha yamepanda!
Uvuvi ambayo kwa miaka mingi ndiyo ilikuwa shughuli muhimu kwa vijana wa Magu na Busega, sasa sio shughuli halali tena kwa vijana hawa na imezaa msamiati mpya...wavuvi haramu!. Pamba ambayo kwa miongo kadhaa ndio lilikuwa zao kuu la biashara, sasa ni zao kuu la hasara. Kibaya zaidi mwenyekiti wa bodi ya pamba ni mbunge wa Magu (dr. Limbu) aliyesomeshwa kwa hela ya pamba kama ambavyo wengi wetu tulivyosomeshwa, lakini hajaonyesha juhudi zozote za kunusuru kilimo na soko la pamba kwa ujumla wake.
Natambua matatizo kama haya yanaikabili sehemu kubwa ya nchi yetu, ila hapa nimeaandika kizalendo zaidi kama mwananchi, mzaliwa, mpiga kura na mfuatiliaji wa karibu wa siasa za Busega na Magu, ambazo awali ilikuwa wilaya na jimbo moja la uchaguzi (Magu). Sina uhakika kama bw. Longo naye anapigia kugombea ubunge, ngoja nimtafute kwa habari zaidi.