SoC03 Jicho la karibu linahitajika kunusuru Elimu yetu

Stories of Change - 2023 Competition

Mfimbo

Member
May 10, 2015
5
11
Kwa miongo kadhaa sasa suala la elimu limekuwa likishika hatamu katika mijadala mbalimbali nchini. Maoni mengi yamekuwa yakilenga kuishauri serikali kufanya mabadiliko ya mitaala ikihusisha uhuishaji wa mambo yanayopaswa kufundishwa katika zama hizi zilizotawaliwa na ushindani katika kila Kona ya maendeleo. Binafsi naamini mabadiliko tunayoyalilia kuinusuru elimu yetu hayatakuwa na tija kama serikali na wadau mbalimbali wa elimu hawatakua tayari kuwajibika vile ipasavyo katika nafasi zao. Natamani kuona mabadiliko ya kiuwajibikaji katika maeoneo yafuatayo ili kuipa ubora elimu yetu:

Kuhusu elimu inayogharimiwa na serikali: Serikali inatumia kiasi kikubwa sana cha pesa kuwezesha elimu bila malipo nchini. Mpaka sasa ni dhahiri kuwa mpango wa elimu bure umefanikiwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule ila sio kwenye eneo la kuboresha elimu. Mpango wa elimu bure ulipaswa kutanguliwa na ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu za kutosha, kuajiri walimu wa kutosha na wenye weledi na kuboresha maslahi ya walimu. Bora tuwe na wahitimu 10 walio vizuri kitaaluma kuliko kuwa na wahitimu 1000 wasiojua hata stadi za KKK. Kwa mustakabari wa maendeleo yetu, serikali haina budi kuacha kufanya maamuzi kwa minajili ya kuwafurahisha wapiga kura wake bila kujali athari zake kwa taifa kwa ujumla.

Kuhusu sifa za kitaaluma kwa wahitimu wanaotarajia kujiunga na mafunzo ya ualimu: Elimu ni eneo nyeti sana kwa maendeleo ya taifa. Hakuna nyaja ya maendeleo inayoweza kufanya vizuri kama itakosa wataalumu katika eneo husika. Vivyo hivyo pia katika elimu. Ubora wa walimu waliopo ndio utatoa taswira ya wahitimu wetu. Si rahisi kwa mwalimu anayefundisha kitu asichokijua kumtengeneza mhitimu bora.

Hapa namaanisha serikali inapaswa kuja na vigezo vipya juu ya sifa za kitaaluma anazopaswa kuwa nazo yeyote anayekusudia kusomea taaluma ya ualimu. Na hapa ni daraja la I na II ndio wanapaswa kupewa nafasi ya kujiandikisha na mafunzo ya ualimu. Natambua kuwa uamzi huu unaweza usipokelewe kwa furaha na bashasha lakini siku zote maamzi magumu ndio yaletayo tija kwa taifa. Tukishakuwa na walimu wenye weledi katika vile wanavyovifundisha itakuwa ni rahisi sana kuwapata wahitimu wenye ubora wa hali ya juu na ambao watakuwa chachu ya maendeleo kwa taifa letu.

Kuhusu suala la mitihani ya taifa: Ni ukweli usiopingika kuwa serikali hutumia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya zoezi zima la mitihani ya taifa. Uwepo wa mitihani ni jambo lenye afya kwenye elimu kwani hutumika kama kichocheo kwa wanafunzi kujituma katika masomo yao na hata kutengeneza msingi wa kuwapata wataalamu katika fani mbalimbali. Kwa sasa mitihani hii ya taifa inachezewa sana na baadhi ya watu. Kuna baadhi ya taasisi (za serikali na binafsi) zimekuwa zikihujumu zoezi la mitihani ya taifa na hivyo, kupelekea watu wasio na sifa fulani waonekane wenye sifa hizo. Kama mchakato wa usimamizi wa mitihani ya taifa ungekuwa unafanyika kama vile ulivyokusudiwa basi kwa hakika ingesaidia kuwapata wale wanaostahili ambao baadae ingekuwa rahisi kwao kutumia maarifa yao katika kuleta mabadiliko chanya maeneo mbalimbali.

Kuhusu mfumo mzuri wa kuwasimamia wakuu wa idara mpaka walimu wakuu na wakuu wa shule: Serikali imekuwa ikipokea takwimu mbalimbali kutoka kwa wakuu wa idara zake ambao nao wamezipokea kutoka kwa wanaohusika chini yao. Kwa kiasi kikubwa takwimu hizi huwa ni za kupikwa katika maeneo mengi. Jambo ni hatarishi sana kwa maendeleo ya elimu. Imefikia hatua sasa mpaka mahudhurio ya wanafunzi yanapikwa. Serikali inapokusanya takwimu za mahudhurio lengo ni kujua hali utoro ilivyo katika eneo husika ili kuweza kuja na mikakati mbalimbali ya namna ya kukabiliana na utoro huo. Lakini viongozi wengi kwa sasa hususani walimu wakuu na wakuu wa shule wanaona si vyema kusema ukweli kuwa wanafunzi 10 kati ya 100 ndio waliohudhuria na kuamua kutoa takwimu feki kuwa wanafunzi 95/100 ndio waliohudhuria. Unafanya hivi maana yake umekwamisha jitihada zinazopaswa kuchukuliwa na serikali ili kuhakikisha tatizo la utoro linapatiwa ufumbuzi.

Kuhusu kuheshimu mikataba na makubaliano yaliyowekwa baina ya serikali (mwajiri) na watumishi: Kiukweli ukiukwaji wa mikataba ni jambo linalowakatisha tamaa wafanyakazi hususani walimu nchini. Nyongeza ya mshahara na upandaji wa madaraja ni mambo ambayo yapo kwa mujibu wa sheria lakini serikali imeyageuza masuala hayo kama hisani kwa walimu. Ualimu ni kada ambayo bado maslahi yake yapo chini na hivyo kitendo cha serikali kuendelea kukiuka vipengele vinavyolenga kuwapa ahueni walimu ni kuwakosea sana. Serikali iwajibike ipasavyo kuhakikisha haki za mwalimu zilizopo kisheria zinapatikana kwa wakati ili kukuza hali ya kuipenda kazi na hatimae kuleta ufanisi.

Kuhusu kuajiri wataalamu wengine wasio walimu shuleni: Kwa muda mrefu sana serikali imeshindwa kutambua umuhimu wa kuajiri wataalamu wengine wasio walimu katika shule zake. Kuna haja kubwa kwa shule zetu kupelekewa wataalamu kama wahasibu, wanaohusika na dawati la jinsia na hata nesi kwa kila shule. Uwepo wa wataalamu hawa utaongeza ufanisi kwenye elimu yetu kwani walimu wataachwa na jukumu mama la kuwafundisha wanafunzi pia kuhakikisha pesa inayotolewa shuleni inasimamiwa vizuri kadri ilivyokusudiwa. Pia uwepo wa mtaalamu anayeshughulikia dawati la kijinsia kutasaidia kufichua vitendo vya kikatiri wanavyofanyiwa watoto wetu.

Kwa kumalizia nipende kusema maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho katika elimu ni mengi ila sio mbaya serikali ikaanza na hayo machache niliyoyabainisha.
 
Back
Top Bottom