Baadhi yetu tunaiona Zanzibar inaweza kuwa kama SriLanka nyingine Muungano ukivunjwa. Tamil Tigers unawaona dhahiri sasa.
Na Mohammed Ghassani Nipo nje ya nyumbani kwa wiki moja na kitu sasa, lakini nafuatilia kwa karibu, kupitia mitandao, mambo yanavyoendelea kwetu. Nimeona kuwa kwa mara nyengine tena, Zanzibar imeonekana kwenye magazeti ya Tanganyika. Wenyewe, ukimtoa Mchungaji Christopher Mtikila na kaumu yake, hawataki waitwe Watanganyika. Wanajidai kwamba kuna Tanzania tu. Hata sherehe za jana za uhuru wa Disemba 9, wanaziita ni za uhuru wa Tanzania. Unafiki mtupu! Alaakullihali, turudi kwenye nukta. Zanzibar imetajwa katika magazeti ya Tanganyika
kwa matukio mawili: moja ni lile linalohusiana na kadhia ya Jumuiya ya Kiislam (OIC) na la pili ni la uchimbwaji wa mafuta. Yote mawili yamezishirikisha
serikali, wawakilishi, wanasiasa na wananchi wa kawaida. La kukumbushia Zanzibar kurejesha uanachama wake OIC, liliibuliwa, kama kawaida, na Chama cha Wananchi (CUF). Nasema kama kawaida, maana imekuwa ni ishara ya CUF kuipigania Zanzibar pahala popote pale wanapopata nafasi. Mimi ni katika watu wanaoamini kwamba miongoni mwa mambo makubwa ambayo yamewafanya CUF wafanikiwe Zanzibar, ni kujinasibisha kwao na usemaji na utetezi wa Zanzibar, eneo ambalo wenzao wa Chama cha Mapinduzi (CCM), labda kwa woga na hisia za kulipa fadhila, wako ziro kabisa. Katika semina ya kujadili Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliyofanyika Zanzibar mwishoni mwa mwezi uliopita, wawakilishi Said Ali Mbarouk na Rashid Saleh walisema kwamba umeshafika wakati wa Zanzibar kurudi katika jumuiya hiyo ya Kiislam, kwa hoja kwamba sasa sera ya nchi imebadilika kutoka ile ya kuzingatia siasa tu kwenye mahusiano na kuwa ile inayozingatia uchumi. Economic diplomacy, wasemavyo
Waingereza. Kwenye semina hiyo, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alihudhuria, jibu la Serikali ya Muungano (SMT), kupitia kwake Waziri Membe, lilikuwa kwamba jambo hilo linajadilika, na akatoa matumaini kana kwamba litajadiliwa kweli. Lakini alikuwa anacheza siasa tu kwa kuwa alikuwa kwenye jukwaa la Zanzibar, mbele ya watu wanaojinasibisha na Uzanzibari wao. Kwa mtu kama yeye, ambaye ametokea kwenye system, anajuwa namna ya kucheza na akili za watu. Na akacheza nazo. Jibu hilo halikuipendeza kaumu ya Mchungaji Mtikila. Na kwa kuwa Makamo wa Rais, Ali Mohammed Shein (mwenyewe Mzanzibari na Muislam), alikuwa ndio kwanza amerudi ziara ya nchi za Misri na Iran, Mtikila akaunganisha yote mawili kuongelea kitu kimoja: chuki binafsi dhidi ya Uislam na Uzanzibari. Halafu, kama mchezo wa kuigiza, Wazanzibari nao wakaingia kichwa kichwa kuelekeza hasira
zao kwa Mtikila kama kwamba ni yeye ndiye anayeizuia Zanzibar kupata haki zake katika kizungumkuti hiki cha Muungano. Kwenye mtandao wa zanzinet.org, jukwaa la Wazanzibari linalojadili mausala mbali mbali kuhusu nchi yao, nilisoma maoni ya wachangiaji wengi wakimtaka Mtikila afumbe mdomo wake panapohusika masuala ya Zanzibar. Akosaye la kufanya, azinge mwana akalee, mchango mmoja ulimwambia hivyo Mtikila ukimfananisha na mtu ambaye hana kazi ya kufanya. Lakini huko kulikuwa, na kumeendelea kuwa, sehemu ya mikakati ya SMT kupindisha hoja muhimu, hasa panapohusika hizi za Zanzibar. Nimesema kwamba Waziri Membe alikuwa akicheza politiki tu kule Zanzibar kuonesha kuwa eti kuna uwezekano wa kulijadili suala la Zanzibar na OIC. Ukweli hasa amekuja kuutoa Hussein Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo Rais (Muungano), aliyesema wazi, Alhamis iliyopita, kwamba hakuna suala la mjadala katika hilo. Kwamba inayoweza kujiunga na OIC ni Tanzania, ikitaka, maana ndiyo nchi. Kwamba chini ya Katiba, si sawa kwa Zanzibar kuingia mashirikiano kama hayo. Huo ndio ukweli mkavu kutoka kwenye kinywa cha SMT yenyewe. Lakini katika aliyoyasema Waziri Mwinyi siku hiyo hiyo ni
kwamba mafuta ya Zanzibar hayajaweza kuchimbika kwa kuwa kwenye Tume ya Pamoja wa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri Kiongozi Shamsi Nahodha hakujakuwa na makubaliano. Hakusema, hata hivyo, ikiwa kilichokuwa hakijaafikiwa
kinatokana na kukataa kwa nani, ingawa dhana inatwambia kwamba wanaokataa ni
akina Waziri Kiongozi Nahodha. Huku nako kulikuwa ni kuweka mizani baina ya
mambo mawili tete. Upande mmoja wa mizani kuna ukweli kwamba suala la Zanzibar na OIC ndio limekwisha,
vyenginevyo Katiba ibadilishwe. Uzoefu unaonesha hakuna kitu kama hicho, yaani kuibadilisha Katiba kwa kufuata matakwa ya Zanzibar, bali kilichopo ni kinyume chake, yaani kuibadilisha Katiba kwa kuikandamiza Zanzibar. Wamefanya hivyo takribani mara 14 tangu
mwaka 1964. Upande huo wa mizani unatwambia wazi kuwa Wazanzibari tumepoteza. Upande mwengine wa mizani umetengenezwa
utuoneshe kuwa eti tuko madhubuti. Si akina Waziri Kiongozi Shamsi, Wazanzibari, wameweka ngumu na akina Waziri Mkuu Lowassa,
Watanganyika,
wameshindwa
kuyachimba? Si umadhubuti wa viongozi wetu huo? Lakini ukweli, hata kwa hili uko tafauti na hapo. Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa Watanganyika
wameshindwa
kuyachimba mafuta ya Wazanzibari ati kwa kuwa Wazanzibari hao wameonesha ukaidi wa kuelewa (kama wanavyotwambia).
Siamini ikiwa kweli hawa jamaa wamedhamiria
kuyachimba mafuta yetu, watahitaji ridhaa yoyote kutoka kwetu. Hakuna uzoefu huo, na hauwezi kuwepo sasa. Hawa jamaa wakitaka kufanya leo kwetu hulifanya tu bila ya kujali hisia wala hasira zetu. Hoja ninayojaribu kuiwasilisha mbele yako hapa ni kwamba, panapohusika
Muungano na nguvu za Tanganyika kwa Zanzibar, chini ya utawala wa CCM, hakuna kitu kama hiari. Ni kile kinachoamuliwa na Tanganyika ndicho kizuri na kinachofanyika
Zanzibar, kutoka kuamua nani awe raisi wetu hadi vipi raisi huyo aiongoze Zanzibar yetu. Na huo nao ndio ukweli mkavu. Siku watakayoamua,
watayachimba. Sababu wanazo, uwezo wanao na nguvu za kufanya hivyo wanazo. Naomba nieleweke, kwamba sizungumzii uhalali wa Tanganyika kuyachimba mafuta ya Wazanzibari, bali nazungumzia kwamba uwezekano wa kufanya hivyo kuwa upo. Labda kwa kuandika hivi kuna watu watakaonichukulia
kuwa ni Mzanzibari niliyekwishavunjika
moyo na hatima ya nchi yangu ndani ya kizungumkuti cha Muungano huu, kwa upande mmoja, na wale watakaonichukulia
nanuka ubaguzi, kwa upande mwengine. Wa mwanzo ni Wazanzibari wenzangu, naamini, na wa pili ni Watanganyika au kaumu yao, nadhani. Kwa makundi yote mawili, mimi si mtu wa kuvunjika moyo kiasi hicho. Nimezaliwa miaka 13 baada ya Muungano wa 1964 ulioichukua Zanzibar kimzobezobe, na tayari nilifumbua macho nikikuta kwamba natakiwa kuisahau Zanzibar. Ndivyo mfumo
unavyotutayarisha sote. Lakini, kama ilivyo kwa mamia ya maelfu ya Wazanzibari wengine, nimegoma kuisahau nchi yangu na kuuzika Uzanzibari wangu. Tunawaachia wanaokaa
madarakani kuifanya kazi hiyo ya kuizika Zanzibar, lakini sisi tulio nje ya madaraka tumekataa kuhudhuria maziko wala kukaa matanga ya kifo cha Mama yetu, Zanzibar. Bado tuna moyo. Moyo wa kwamba Zanzibar ipo daima, ilikuwepo jana, ipo leo na itakuwepo kesho
na milele. Akina Mtikila wanatwambia tuache kabisa kufikiria OIC ndani ya Muungano. Kwamba ikiwa tunataka kufanya hilo, labda tujitoe kwenye Muungano. Pamoja na ukweli kwamba hata pale Julius Nyerere alipomlazimisha Salmin Amour kujitoa kwenye jumuiya hiyo kwa kuwa alikiuka Katiba, alikuwa,
yeye mwenyewe Nyerere, anavunja Katiba, maana hadi hapo ushirikiano wa kimataifa haikuwa sehemu ya mambo ya Muungano, bado akina Mtikila wasidhani kwamba ni Wazanzibari wenye shida ya Muungano katika kiwango hicho cha kutwambia, ama tubakie au tutoke. Ni kiwango cha mwisho cha matusi kwetu, Wazanzibari. Hata kama tunajuwa kuwa watawala wetu wanaungangania
Muungano huu na mfumo wake kwa kuwa ndio wanaoutumilia
kujiweka na kujirejesha madarakani, hilo halitujumuishi sote katika kundi moja. Waingereza
walimwambia Tony Blair alipoamua kushirikiana na George Bush kwenda kuivamia Iraq: Not in our name. Vivyo ni kwa sisi, Wazanzibari. Ni kosa kudhani kwamba udhalilifu wote unaofanywa na utawala wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar mbele ya macho ya hao waitwao viongozi wa Zanzibar, hufanyika kwa baraka zetu. Hapana. Na kwa uelewa huo, basi tusipeane ultimatum