Je, tatizo la kutokupata watoto ni tatizo la mwanamke tu?

chuuma

JF-Expert Member
May 19, 2015
363
557
JE, TATIZO LA KUTOKUPATA WATOTO NI TATIZO LA MWANAMKE TU?

Na Kilawa the Iron

Tatizo la kutokupata watoto limeonekana kuwa ni kitendawili katika ndoa nyingi licha ya wapendano hawa kukutana kimwili yaani kufanya tendo la ndoa (kujamiana) kwa wakati muafaka na unaotakiwa pia unaojitosheleza (mara nne au zaidi kwa wiki). Tatizo hili limesababisha ndoa nyingi kuvunjika na hata kupelekea wanawake na wanaume wengi kuwa na msongo wa mawazo ambao pia unaweza kuliongezea tatizo la utasa/ugumba.

Kila binadamu aliyekamilika anatamani au anapenda kuwa na familia yake mwenyewe. Anatamani kuwa na watoto bila kujali ni ndani ya ndoa au nje ya ndoa. Katika jamii nyingi hasa nchi za kiafrica zimekuwa zikiamini kwamba kutokupata watoto ni tatizo la mwanamke na sio mwanaume.

Napenda kuwatoa matongotongo ndugu zangu wengi wanaopotoshwa na watu wengine aidha kwa makusudi au kwa kutokujua lipi ni lipi?.

Awali ya yote niaze kwa kufafanua kwa ufupi maana halisi ya Ugumba/Utasa (Infertility), hali hii ni pale mwanamke anaposhindwa kupata ujauzito na kuweza kuzaa mtoto licha ya kufanya tendo la ndoa kwa mpangilio sahawia ndani ya mienzi 12. Tatizo hili linaweza kusababishwa na mwanaume au mwanamke.
Tafiti nyingi zinaonesha tatizo hili linachangiwa na mwanamke kwa asilimia 20 hadi 35,mwanaume kwa asilimia 20 hadi 30 pia linaweza kuchangiwa na wote kwa pamoja kwa asilimia 25 hadi 40. Watafiti wengine wanasema kwamba tatizo hili linachangiwa na mwanamke kwa asilimia 40 hadi 55,huku mwanaume akichangia asilimia 30 hadi 40.

Tatizo hili linaweza kuwa la kuzaliwa nalo(Primary infertility) au laweza kutokea baada ya kuzaa mtoto mmoja au zaidi. (Secondary infertility).Kiujumla watu wanaokutuna kimwili(kufanya tendo la ndoa) wanauwezekano wa asilimia 85% au zaidi kupata mtoto ndani ya mwaka mmoja.

Tatizo la ugumba/utasa linaweza kuwa la mwanake, mwanaume au wote kwa pamoja. Hivyo kukosa watoto si swala la kumkurupukia na kumlaumu mwanamke pekee moja kwa moja. Ni dhahiri imekuwa desturi yetu tuliowengi, kuwafukuza wake zetu kwa kukosa watoto na hata kuwadharirisha katika jamii zetu lakini pia watu wasiozaa wakati mwingine hutengwa na jamii zao na kuonelewa sana.

Tuangazie kwa ufupi kwanini tatizo la ugumba linatokea, tutajadili sababu hizi kwa kugusia kwa ufupi upande wa mwanamke ikifuatiwa na sababu zinazopelekea mwanaume kukosa watoto.

Sababu gani zinapelekea tatizo la kukosa watoto kwa mwanamke?
Kuna sababu nyingi sana zinaweza kupelekea mwanamke kukosa watoto, nitaelezea kwa ufupi sababu kadhaa kama ifuatavyo.

1.Tatizo la mfumo wa fahamu unaoratibu utengenezaji wa homoni(vichochezi vya mwili kama vile Follicle stimulating hormone FSH na Luteinizing hormone LH). Kama homoni hizi hazitatengenezwa au zikipungua zinaweza kusababisha mwanamke kukosa uwezo wa kutengeneza mayai au kutengeneza mayai yasiyo na uwezo hali inayompelekea kukosa uwezo wa kuzaa mtoto. Tatizo hili linaweza kuwepo kwenye tezi za pituitari au hypothalamus au kwenye ovari zenyewe. Utengenezaji wa homoni hizi zinategemeana sana kutoka tezi moja na nyingine ikiwa kati ya tezi hizo moja wapo imeathirika basi mfumo huo unakuwa umeathiriwa na kukosa uwezo wa kusaidia kulitengeneza yai na kukosa mtoto.

2.Kuziba kwa mirija ya kupitisha mayai(Oviduct/Fallopian tube). Mwanamke huyu anaweza kuwa uwezo wa kutengeneza mayai vizuri lakini kwakuwa mirija imeziba yai lilokomaa haliwezi kupita ili likakutane na mbegu ya kiume na kuweza kurutubishwa ili kupata mtoto. Tatizo hili la mirija kuzibwa linaweza kusababishwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kaswende na kisonono n.k au maumbikizi ya wadudu wengine wanaoathiri mfumo wa uzazi (Pelvic inflammatory disease PID).
Pia mirija hiyo inaweza ikawa imeziba kwa upasuaji uliofanyika kipindi cha nyuma.

3.Uvimbe wa kwenye nyumba ya uzazi (Uterine fibroids) na kwenye kiwanda cha kuzalishia mayai yaan kwenye ovari (Ovarian cyst and tumour). Tatizo la uvimbe kwenye mfuko wa uzazi likiwa kubwa linaweza kuzuia mbigu ya kiume kwenda kukutana na yai la kike au yai lilorutubishwa kuziuwa kujishikiza kwenye nyumba ya uzazi au hata lile yai lilobahatika kujishikiza linaweza kutolewa kabla ya wakati(Miscarriage). Sio uvimbe pekee unaoweza kuleta matatizo bali pia kama maumbile ya mfumo wa uzazi kama hayapo sawa linaweza kumfanya mwanamke huyo kukosa mtoto.

4.Umri mkubwa wa mwanamke (>35), kikawaida tunashauri mwanamke kupata ujauzito wako wa kwanza kati ya miaka 18 hadi 30 akichelewa sana asizidi miaka 35.kadri umri unavyozidi mayai ya mwanamke hupungua uwezo wake na hupungua idadi yake, ikumbukwe kila mwenzi mwanamke anatoa yai moja au zaidi na mayai yaohazidi 450 katika maisha yao. Pia watu hawa wakifika miaka 45 au zaidi wakosa kabisa uwezo wa kuzaa.

5. Matumizi ya baadhi ya madawa na pia kuathiriwa na magonjwa sugu kama vile ugonjwa wa Inni, Figo, kisukari, magonjwa ya akili n.k. Sambamba na hayo kama mtu ana historia ya matumizi ya Diethylstillbestrol humpelekea kuwa mgumba/tasa. Hivyo kabla ya kutumia dawa yoyote ile lazima ujue kwa ufasaha kama inaweza kuleta shida yoyote katika mfumo wa uzazi.

Sababu zinazoweza kumsababishia mwanaume kuwa Mgumba/Tasa ni zipi?

1.Kuzalisha mbegu zisizo na uwezo wa kurutubisha yai la kike.
Kama mwanaume atazalisha mbegu zisizo na uwezo wa kusafiri kwa kukosa mkia,au zenye muonekano usio sahawiya kwa kurutubisha yai au kuzalisha mbegu zenye ujazo mdogo (chache) au zilizokosa chemikali inayosaidia kupenya kwenye yai ni lazima atakosa watoto kabisa. Mke wake anaweza kushirikiana naye tendo la ndoa bila mafanikio kwa mwaka mmoja lakini mwanamke huyo akifanya tendo la ndoa na mwanaume mwingine mwenye mbegu zenye uwezo ni lazima atapata ujauzito na kuzaa.

2.Matatizo ya kimaumbile kwa mwanaume.
Kama korodani zinazozalisha mbegu za kiume hazijashuka na kukaa kwenye mfuko unaohifadhi mbigu hizo ni lazima mwanaume huyu atakuwa tasa, ikumbukwe mbegu za kiume huzalishwa kwenye nyuzi joto 2°C chini ya joto halisi la mwili na ndio maana mbegu za kiume ni hubembea chini. Lakini pia kama viungo vya mfumo wa uzazi havijakamilika au mirija ya kutolea mbegu imeziba humsababishia ugumba. Sambamba na hii kama njia ya kupitia mbegu imefunguka chini(Hypospadius) inaweza kusababisha mbegu hizo kutokuingia ukeni na kuishia nje ya uke na kusababisha ugumba.

3.Matatizo ya mfumo wa homoni(Endocrine system). Kama mwanaume atakuwa na tatizo linaloathiri utengenezaji wa homoni zinazoweza kuchochea utengenezaji wa mbegu za kiume basi ni lazima mtu huyo atakuwa tasa, tatizo hili linaweza kuwa kwenye tezi ya pituitari, au kwenye korodani kwenye. Ambapo tezi hizo zinaweza kuwa hazifanyi kazi kabisa au zinafanya kwa kiasi kidogo. Inaweza kuwa imesababishwa na saratani, maambukizi na matumizi ya baadhi ya madawa kwa mfano madawa ya kupunguza shinikizo la damu kama vile dawa aina ya methyldopa.

4.Maambukizi ya magonjwa ya zinaa na magonjwa mengine ambayo yanaweza kushambulia kwa kubwa mfumo wa uzazi wa mwanaume hali inayoweza kuzuia utengenezaji wa mbegu au kuziba mirija ya kupitisha mbegu za kiume.

5.Kukosa uwezo wa kusimamisha uume, watoto wa uswahilini wanasema kuangukiwa na kabati. Hali ya mwanaume kutokusimamisha uume inathiri sana ndoa nyingi hali hiyo inaweza kusababishwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya mfumo wa fahamu na ni hali inayowatokea wanaume wengi sana duniani. Tatizo hili limekuwa kikwazo kikubwa kwa wanaume wengi hali inayopelekea watu hawa kukosa amani na kujihisi sio wanaume kabisa, tatizo hili linaweza kupelekea mwanaume kukosa watoto kabisa.

Yapo matatizo mengi yanayoweza kusababisha ugumba kwa mwananume au kwa mwanamke. Tunaweza kuyajadili hata siku nzima na tusiyamalize.
Tutajadili kwa kina kadili Mungu atakavyotujaalia siku za mbeleni. Usikose kufuatilia kwa ukaribu kuona ni jinsi gani tunaweza kutatua tatizo hili kitaalamu....
Itaendelea..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom