Je, Safari ya kuelekea Ethiopia imeanza?

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279

upload_2018-3-5_11-28-25.jpeg


Katika nchi ambazo zina historia ya kukandamiza haki za binadamu, uhuru wa raia, demokrasia na uhuru vyama vya siasa Baran Africa Ethiopia ni miongoni mwa nchi hizo. Tokea kipindi cha Utawala wa Kijeshi wa Mengitsu Haile Mariam na badaye Utawala wa Melas Zenawi toka mwaka 1991 hadi 2012 Ethiopia imepitia kipindi kigumu cha uongozi wa mabavu, ubaguzi, ukatili na mauaji ya wapinzani au wakosoaji wa serikali.

Darubini hii ya kichambuzi inachambua hali ya sasa hapa chini Tanzania kwa kurejea mwenendo mzima wa kisiasa na kiutawala nchini Ethiopia kuanzia 2005 hadi hivi karibuni Waziri Mariam Desaley alipojiuzulu.

Tanzania na Ethiopia ni nchi kubwa zenye idadi kubwa ya watu ( Ethiopia zaidi ya million 100 na Tanzania zaidi ya 50 Milion) na eneo kubwa kijiografia na wanachi wake ni wakulima na wafugaji. Tanzania na Ethiopia zina mfumo wa vyama vingi na ufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Kiongozi Mkuu wa Ethiopia ni Waziri Mkuu na Tanzania ni Rais, tofouti ni majina ya uongozi lakini mamlaka ni sawa kabisa. Chama Tawala nchini Ethiopia ( Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kinatawala toka 1991 kwa Muungano wa vyama vingine vidogo.

Melas Zenawi kiuchumi amefanya Taifa hilo lionekane ni Taifa lenye uchumi mzuri kimataifa, lakini watu wake wakiwa na umaskini mkubwa na wakiogelea katika uongozi unaonuka damu, uliokiuka haki na uhuru wa raia. Maelfu wamekufa, maelfu wanashikiliwa katika magereza na kambi za kijeshi na wengine wapo uamishoni kwa uthubutu wao wa kudai haki na usawa.

Ubaguzi na Ukabila

upload_2018-3-5_11-28-25.jpeg


Ubaguzi na Ukabila katika nchi ya Ethiopia upo kwa asilimia kubwa na ndiyo msingi wa migogoro ya Ethiopia kwa sasa. Ethiopia ina zaidi ya watu million 100 na makabila makubwa kama yafuatayo; Oromo 35% ya wananchi, Amhara 27 ya Wananchi, Somali 6% ya wananchi, Sidoma 4% ya wananchi, Gurage 2.5% na wengine 19%. Oromo ambalo ndo kabila kubwa limekuwa lilkilalamika kubaguliwa na kutengwa kuazia kwenye uongozi hadi maendeleo.

Tanzania hatuna ubaguzi wala ukabila wa aina ya Ethiopia, ila kuna kila dalili za kuelekea huku kama kusipochukuliwa hatua za haraka. Tanzania ina makabila zaidi ya 120. Huko Zanzibar wananchi na wanachama wa chama fulani wamekuwa wakibaguliwa kutokana na itikadi yao na asili yao, na baadhi ya wanasiasa kudiriki kuwaita majina ya kibaguzi wazanzibari wenzao.

Wiki ijayo kamati kuu ya Chama Tawala inchini Ethiopia inakutana ili kumchagua waziri mkuu mpya ,na safari hii ili kutuliza hali nchini humo wanategemea kumpata toka vyama vya wana Oromo kinachaunda umoja wa chama Tawala. Mvutano huu ndani ya Umoja huu ni moja ya sababu ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Desaley.

Mauaji, Kuteswa na Kutoweka kwa watu
Maelfu wameuwa, wengine kutoweka na kuteswa na vyombo vya usalama kuhusishwa moja kwa moja. Serikali ya Melis Zenawi iliyodumu toka 1991 hadi 2012 imeshutumiwa kwa muda mwingi kuwa ya Kidikteta na kuhusika na ukandamizaji huu wa makundi yaliyokuwa yanampinga pamoja na wakosoaji wakiwepo waandishi wa habari na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Mamia ya wanasiasa wamekufa, maelfu ya wananchi wamekufa na wengine wengi kupoteza wakiwemo waandishi wa habari na wakosoaji wengine. Wanaharakati, wanasiasa na waandishi wengi wanaishi uamishoni katika nchi mbalimbali duniani. Mauaji, kutoweka kwa makundi tajwa kunazidi kushika kasi Tanzania lakini bado wanaotajwa kuhusika ni watu “wasiojulikana”. Kuna baadhi ya matukio Jeshi la Polisi limetuhumiwa moja kwa moja kama mauji ya Binti Akwliina.

Kwa sasa hatuna watu waliokombia Tanzania na kufanya kazi zao wakiwa nje, lakini tusipokaa kama Taifa na kudhibiti viashiria vya sasa hapo mbeleni tunaweza ona makundi ya watu wakikimbilia nchi mbalimbali na kufanya harakati wakiwa nje kwani tayari kuna watu wameshaitwa wasaliti, sio raia, wachochezi na maadui wa Taifa.

Historia ya Ethiopia inaoyesha pia walianza kwa utaratibu huu na wengine kuitwa magaidi na kufungwa maisha. Ili kuepuka hii safari ya kuelekea Ethiopia nashauri kama Tafa tukae chini na kufanyia kazi viashiria hivi.

Kukamatwa kiholela, kutiwa kuzuini na kufungwa
Makundi ya wanahabari, wanaharakati, wanasiasa wa upinzani maelefu wamekamatwa na kufunguliwa kesi nyingi kuanzia 2005 hasa kesi za kubambikizwa kama za kufanya matukio ya uchochezi na kigaidi. Kulitengwa eneo maalum na makambi ya kijeshi kwa ajili wa wafungwa hawa walionekana kukosoa uongozi usiojali haki za watu wa Mels Zenawi.

Mels Zenawi ndio aliepindua serikali ya kimabavu na ya Kijeshi 1991 ya Mengstu Haile Mariam na kuingia madarakani toka kabila dogo la Tigray ambalo limekuwa likilalamikiwa kupendelewa na Rais Zenawi. Wafungwa wa kisiasa kama kina Merena Gudina wa vyama vyama vya Oromo na wengine 6000 na zaidi waliachiwa huru na Waziri Mkuu aliejiuzulu baada ya shinikizo la maandamano nchi nzima.

Katika vitu ambavyo vimechangia kuondoka kwa Waziri Mkuu ni suala la kutaka kuanza kuzingatia haki na demokrasia nchini humo ampapo bado kulikuwa na mvutano ndani ya chama chake. Hadi sasa Taifa hilo lipo kwenye hali ya hatari.

upload_2018-3-5_11-28-25.jpeg


Gudina alikamatwa mwaka 2016, baada ya kukosoa rekodi mbaya ya haki za binadamu ya serikali ya Addis Ababa na hali ya kisiasa nchini Ethiopia. Kwa mujibu wa BBC, Askari usalama wa serikali ya Ethiopia wamekamata makumi ya maelfu ya watu na kuua waandamanaji zaidi ya 900 tangu yalipoanza maandamano ya watu wa Oromo 2014 waliokuwa wakipinga unyakuzi wa ardhi zao, ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya dola.

Uhuru wa Mashirika ya Haki za Binadamu
Mashirika yote ya ndani na Nje yalipigwa marufuku kufanya kazi zao. Mashirika mengi yalifungwa na wengi kukimbilia nchi zingine na kufanya kazi wakiwa kama wakimbizi. Yamewekewa mazingira magumu kwa asasi za kiraia ikiwemo kutakiwa kupata pesa asilimia 10 tu toka nje. Tanzania bado tuna hali ambayo siyo kama ya Ethiopia kwa sasa.

Ingawa kuna watu wanatamani tufike huko kama Ethiopia. Viashiria vidogogo vya kubana uhuru wa AZAKi kufanya kazi kwa uhuru umeanza kuonekana katika maeneo kadhaa. Sasa hivi hata matangazo ya AZAKI kwenda kwa vyombo vya habari yanahitaji kibali cha serikali. Kwenda mikoani kufanya kazi vibali vinahitajika toka TAMISEMI, kufungua akaunti ya shirika lazima upate kibali,kutoa taarifa ya uangalizi wa uchaguzi unahitaji kwanza kupeleka taarifa kwa Tume ndipo kutoa kwa umma.

Mashirika yakijaribu kukosoa na kushauri baadhi ya mambo kwa maslahi ya umma yanaanza kutishiwa hasa yale yaliyopo nje ya usimamizi wa sheria ya NGOs ya 2002 na Brela. Narudia Tanzania bado tupo vizuri kiasi ila kuna watu kwa sasa hawalali wanatafuta nauli za kutufikisha Ethiopia, nashauri baada ya muda rejeeni andiko hili.

Uhuru wa Kujieleza na Vyombo vya Habari
Kwa Ujumla Ethiopia hawan vyombo huru vya habari na waandishi wengi wamekatwa na wapo jela, wengine kuuwawa huku wengine wakifanya kazi wakiwa nje kama kin Solomon , Kiflu nk. Hali yao ni mbaya zaidi. Zaidi ya Waandishi 100 wanatumikia vifungo, wengine wanafanyia kazi nje na wengine wamekufa.

Vyombo vya habari zaidi ya 15 vimefungiwa na vingine kufa venyewe kwa kuwa viongozi wao wanatumikia vifungo. Serikali ndio inasimamia na control media zote hata binafsi. Internet inatolewa na Serikali pekee na Mitandao yote ya Kijamii iko restricted hata zinazoendeshwa na wakimbizi wa Ethiopia. Tanzania hapa tuna afadhali, tunaonekana kuwa na vyombo vingi vya habari lakini havina uhuru , vyombo vingi hadi sasa zaidi ya vitano vimefungiwa na vikwazo vingi kuzidi kuongezeka kwa vyombo vya habari hasa kipindi cha uchaguzi.

Waandishi kupigwa, kukamatwa na kutekwa kwa Mwandishi Azori hadi leo. Kwa sasa tuna afadhali ukilinganisha na Ethiopia, ila kuna watu wanahangaika usiku kucha ili kuhakikisha tunapata nauli ya kuelekea Ethiopia. Baada ya muda mnaweza rejea andiko hili.

Wafanyakazi hawakuwa na uhuru wa kudai maslahi na vyama vya wafanyakazi vilifutwa. Wafanyakazi walilazimishwa kuwa wanachama wa chama tawala na wale waliokutwa wakiwa wanaunga mkono vyama vya upinzani walifukuzwa na wengi wao toka kabila la Oromo. Mfano Jimbo la Oromia walimu wengi sana wamefukuzwa kwa kunga mkono upinzani.

Tanzania tuna vyama vya wafanyakazi lakini ni kama havipo na mbaya zaidi wanatumia pesa za wafanyakazi wanazokatwa kuziendesha bila kusimami maslahi na haki za wafanyakazi hasa dhidi ya udhalishaji. Pia tumeshaanza kuona kauli zikiwataka wafanyakazi wa umma kuwa wafuasi wa chama chatawala. Kwenye hili nadhani nauli ishapatikana na tayari baadhi wameshaingia kwenye ndege kuelekea Ethiopia. Rejeeni matamko ya hivi karibuni kuhusu wafanyakazi na siasa.

Makundi ya Waasi
Kumekuwa na Makundi ya Waasi hasa katika Kanda za Wahoromo na Somali. Haya ni makundi yaliyobaguliwa na kuonewa kwa muda mrefu hadi kuamua kuingia katika makundi ya kuasi. Hatuna kwa sasa makundi haya, ila taifa linakundi linalohisi kuonewa na kubaguliwa ambalo ni kundi la wapinzani na wale wakosoaji hadi kufikia kuitwa wachochezi, maadui wa Taifa na bila kuchukuliwa hatua zozote kwa aliejitokeza kuwaita watanzania wenzake maadui wa Taifa.

Huko Zanzibar kuna watu wananungunikia moyoni kwa kubaguliwa kisiasa na kutengwa katika mambo mengi kutokana itikadi na asili yao. Nashauri Taifa langu tusiruhusu hali ya kubaguana na kuoneana kwani mwisho wake ni mbaya.

Mikutano ya Kisiasa na Maandamano
Katiba ya Ethiopia inaruhusu Maandamano lakini Serikali ilipiga marufuku maandamano mara baada ya uchaguzi wa 2005 ambao upinzani ulipata wabunge wengi zaidi ya 200 kati ya wabunge 570. Kupatikana wa wabunge na madiwani wengi wa Upinzani kulimstua sana Mels Zenawi na kuanza mkakati wa kuumaliza upinzani kabla ya uchaguzi wa 2010.

Mabadiliko ya sharia nyingi yalifanyika ili kuvibana vyama vya siasa na taasisi zingine huru mwaka 2007. Wanasiasa wengi na wafuasi wao waliuwa na Polisi wakati wa kupambana na waandamanaji. Hapa Tanzania pia Maandamano yameruhusiwa kikatiba lakini mara baada ya uchaguzi wa 2015 kiongozi mkuu alipiga marufuku maandamano nchi nzima na baadhi ya watu wameumizwa na wengine kupoteza maisha wakati wa purukushani na polisi waliokuwa wakizuia maandamano. Kipindi hich ndipo Upinzani ulipata madiwani wengi na wabunge wengi karibu 150 kati ya wabunge 300+ wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Wanasiasa walipigwa marufuku kutembea katika maeneo mbalimbali ya nchi kufanya siasa na wengine hata kwenye majimbo yao walizuiliwa mara baada ya uchaguzi wa 2005 inchini Ethiopia , waliojaribu walikamatwa na kufungwa. Hali hii ilifanya katika uchaguzi wa 2010 Bunge kuwa na Mbunge Mmoja wa Upinzani. Hapa Tanzania, Wabunge na wanasiasa wamezuiliwa kufanya mikutano na maandamano nje ya majimbo yao.

Na hata wengine ambao ni viongozi wa Upinzani wamekuwa wakikamatwa kwa kufanya mikutano ya siasa. Wengi wana kesi za kufanya mikutano isiyo halali. Hali hii ni kama nauli ya kuelekea uchaguzi wa Ethiopia wa 2010, na isipozibitiwa pia inaweza kufanya Bunge la 2020 tukawa na Mbunge mmoja wa Upinzani na madiwani wote wa chama tawala. Hii ni darubini yangu huru kama mchambuzi huru wa sera na siasa za Africa.

Uchaguzi na Demokrasia

upload_2018-3-5_11-28-25.jpeg


Chaguzi za Ethiopia zimekuwa na matukio mengi ya mauaji , kutoweka, vurugu, kukamatwa watu na wanasiasa kiholela na mawakala wa vyama vya upinzani kuzuiwa. Mwaka 2005 Muungano wa Chama Tawala kilipata wabunge 372 kati ya wabunge 574 na Upinzani wabunge 202. Tume (NEB) yao ya Uchaguzi imelalamikiwa kuwa chombo cha Chama Tawala.

Kutokana na vitisho, mauaji, na mkakati wa kuwahamisha wanachama wa upinzania upinzani uliambulia kiti kimoja cha ubunge katika uchaguzi wa 2010. Jumla ya wabunge 2010 walikuwa ni 547, mmoja ametokana na nafasi ya mgombea huru, 545 kutona na Muunganiko wa Chama Tawala na mmoja toka chama cha upinzani. Katika uchaguzi huu wapinzani hawakupata hata kiti kimoja cha udiwani.

Kuporomoka kwa upinzani katika uchaguzi wa 2010 Ethiopia kumetokana na vitisho kwa vyama vya upinzani hasa kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa kwao ni Federal Goverments , hali hii ilipelekea mamilion ya wanachama wa upinzani kujiunga na chama tawala. Mfano, kabla ya uchaguzi wa 2010 chama Tawala kiliweza kwa njia mbalimbali kuchukua wanachama zaidi ya milio 7 wa upinzani, huku viongozi wakifungwa na wengine kukimbia uamishioni. Kwa mujibu wa EU kama watazamaji wa uchaguzi na siasa wa nje wanasema vitisho na kukamatwa kiholela kwa wapinzani kumechangia sana kuanguka kwa upinzani katika uchaguzi wa 2010.

Surah hii ya siasa za Ethiopia ni kama inatunyemelea hapa Tanzania. Chaguzi zimeanza kuwa za matukio ya uvunjifu wa Amani, vitisho na umwagaji damu. Hali hii japo inaweza onekana ni ya chini bado, inadhirisha wazi kuwa vyama vina hali mbaya na wanasiasa wao hasa viogozi , wabunge na madiwani wanapata vitisho vingi na ubaguzi toka kwa viongozi wa serikali za mitaa hadi wengi wao kuamua kuhama vyama vya upinzani.

Wabunge wengi wa Upinzani wana kesi mahakamani na wawili tayari wameshafungwa, hadi ifike 2020 huenda idadi ikaongezeka. Mwaka 2015 Wabunge wa Upinzani Tanzania walikwa karibu 150. Idadi hii ya wabunge wa upinzani ina mawili (kwa uchambuzi wangu) aidha waishe wote kabla ya 2020 au baada ya uchaguzi wa 2020, au waongezeke maradufu katika uchaguzi wa 2020 kulingana na hali itakavyokuwa kati ya leo na 2020.

Huu ni uchambuzi wangu huru unaoleta tafakari kwa Taifa ili kuepuka kuelekea katika maisha ya nchi kama Ethiopia. Ushauri wangu kwa viongozi wangu ni kuwa waende Ethiopia wakajifunze madhara ya kubinya uhuru wa wananchi, demokrasia na haki za binadamu. Maendeleo yoyote bila uhuru si kitu kwa raia. Kuna faida kubwåa sana kama Taifa litaheshimu utawala wa sharia, demokrasia, haki za binadamu na usawa.

Maendeleo endelevu yanakwenda sambasamba na uhuru na haki za binadamu. Taifa lango bado lipo vizuri na kamwe tusikubali kuanza safari yoyote ya kwenåda Ethiopia. Tujenge utaratibu wa mazungunzo pale tunapoona viashiria vibaya kwa Amani ya Taifa badala ya kutumia nguvu na mabavu ziaidi. Mungu Ibariki Tanzania, watu wake na viongozi wake.



Comrade Onesmo Paul Olengurumwa Kasale, ni mtetezi wa haki za binadamu, mchambuzi huru wa sera na siasa za Africa na asiefungamana na chama chochote barani Africa na Tanzania na wala si muumini wa mrengo (Ideology) wowote wa siasa duniani zaidi ya ule wa Mwalimu Julius Nyerere. opngurumwa@gmail.com
 
Umeeleweka vizuri Olengurumwa. Mimi nazani Mtawala akiwa kwenye kiti anaona wengine wote ni bure kabisa,
 
Alikuja wa Ethiopia
akaja wa Burundi
then Rwanda
Then Uganda
Then Turkey

Nadhani macho hayadanganyi
Tumuombee mama Tanzania abaki salama
 
Back
Top Bottom