Kama kuna wakati tunapaswa kutafakari hatima ya Nchi yetu ni sasa. Tatizo la msingi ambalo tunapita kama Taifa ni uoga , kwa maoni yangu uoga unaweza kuwa ndio dhambi kubwa na mbaya kuliko zote Duniani , hata hivyo kuwa jasiri ni kuwa na nia ya dhati kabisa ya kusimamia haki na kukataa uonevu.
Kila jambo linalotokea ktk maisha yetu ni ruksa inayotokana na hiari ya maamuzi yetu, kwani kushindwa au kushinda kwa jambo lolote hakutokani na uwezo wa maadui zetu bali maamuzi yetu na mtazamo katika mambo mbali mbali.
Sasa tuna kilio kikubwa cha demokrasia kukandamizwa , uhuru wa vyombo vya habari na mambo mengine mengi yanayofanana na haya.
Kwa sasa karibu Wabunge wote wa Upinzani wana kesi mbali mbali katika mahakama Nchini na wengine wana vitisho mbali mbali kama kuuwawa na wengine kuharibiwa mali na kufilisiwa kabisa pia Mbunge wetu Mh Tundu Lissu anauguza majeraha ya risasi Nchini Ubelgiji baada ya kukaa Nairobi takribani miezi minne.
Wakati tunapita kwenye nyakati kama hizi unaweza kusikia watu wanasema kwa kweli Chadema wanapita kwenye wakati mgumu sana , ni kweli tunapita kwenye wakati mgumu sana lakini haya ni mawazo na fikra potofu kufikiri kuanguka kwa demokrasia ni anguko la Chadema. Demokrasia na haki inaposhindwa ni Taifa linashindwa kwa hiyo wajibu wa kupigania haki ni wajibu muhimu wa kila mtu anayependa Nchi yake na wajukuu zake.
Kwa kweli kwa sasa , hatujui hatima ya maisha yetu sana kwani Siasa Nchini zimekuwa na uadui mkubwa sio kwa sababu tumevamiwa na Nchi jirani lakini ni kwa vile hadhi ya madaraka na utawala imekuwa muhimu kuliko HAKI na UTU .
Maisha yetu yamekuwa magumu sana , tunawezaje kukosa mashaka kwenye hali kama hii ya sasa,tunafundishwa uoga kila leo na tunaweza tu kushinda hali hii kwa kudharau tunavyojisikia kuhusu hofu na uoga kwani pasipo kudharau kwa ajili ya malengo ya haki ya Nchi yetu basi dhamira zetu zitapaswa kulaaniwa na vizazi vinavyokuja.
Unapoona kauli ya Jaji Mkuu kuhusu uhuru wa Mahakama , tunapoona Wabunge wanateswa kwa kutengenezewa mashitaka ya aina mbali mbali , tunapoona Mbunge anapigwa risasi mchana nyumbani kwake mioyo yetu inatazama na kulia kwa uchungu,sio fahari wala sifa kuvumilia mateso ila kwa sasa ni wajibu muhimu ambao haupaswi kukimbiwa hata kidogo , kwani thamani ya maisha yetu haijengwi na hadhi zetu na mali zetu za leo na vyeo vyetu bali msingi imara tunaoweka kwa ajili ya vizazi vinavyokuja baada yetu na msingi huo ni haki , tabia njema , usawa , kuheshimiana , utu na hadhi ya utawala wa sheria na demokrasia , kama tukifikiri hivi ni dhahiri kuwa tutakuwa tunaonyesha Upendo kwa watoto wetu na vizazi vinavyokuja.
Kwa bahati mbaya mashabiki wa mpira wamekuwa na hekima ya ushindani kuliko mashabiki wa demokrasia , hakuna Uchaguzi unaopita bila maumivu na mateso na hii inaonyesha busara mbaya ya mwekekeo wetu kama Nchi.
Tutafanya nini sasa Kurekebisha hali hii ? Ni muhimu kujua msingi wetu wa fikra katika haki na utu , kama Watanzania wataendelea kufikiri na kutenda na kuamua mambo ya Nchi yao kwa hofu na uoga basi ni wazo hata mfumo wa vyama vingi hautakuwa na maana kwetu, ni lazima Wananchi wajue Serikali inawajibika kwa ajili yao na ni lazima sana Wananchi wasiruhusu hata kidogo Nchi kuendeshwa bila utaratibu wa sheria na Katiba ,sasa ikiwa Wanamchi watafikiri kazi ya kulinda haki ni kazi ya vyama vya siasa basi Wananchi sisi tutakuwa tunafanya makosa makubwa ya kuangamiza Taifa. Ukiukwaji wa mambo ya msingi unaoendelea unasababishwa na aina ya tabia ya Wananchi katika Nchi, wakati Nchi nyingine mkate ukipanda bei watu wanaandamana huku kwetu Mbunge anapigwa risasi na wanao kusanyika kumuombea wanakamatwa na kushitakiwa na hakuna hatua yoyote inayo chukuliwa na Wananchi kuonyesha kuchukizwa na mambo haya,kipimo hiki kinathibitisha uoga wa kina kabisa ktk jamii.
Tabia hii ya uoga isipo koma nafikiri hata ikatokea Chadema kuongoza Nchi hakutakuwa na tofauti kubwa sana kati yetu na ccm kwani mlinzi wa Nchi bora sio sera na rangi ya Chama cha Siasa bali ni tabia na fikra za wanaotawaliwa (Attitude ) dhidi ya Nchi yao .
Kuishinda hofu sio tu ni faida katika Nchi bali ni msingi mzuri wa kujenga kizazi cha ubunifu sehemu mbali mbali za maisha yao ya kila siku. Hofu haiwezi kujenga uwezo ubunifu (innovations) kwa sababu hofu ni ugonjwa mbaya sana wa akili.
Kabla ya kusema kwamba Bunge letu haliko huru ni muhimu kujiuliza kama hao Wabunge wenyewe wanajua thamani ya uhuru ? Na wako huru ?
Kabla vile vile ya kusema Mahakama zetu haziko huru ni vyema tukajiuluza kama vile vile hawa watumishi wa Mahakama wanajua vyema thamani ya uhuru ? Na wanathamini haki kwa kiwango gani ? Hatuwezi kujenga Taifa imara bila kubadilisha mfumo wa fikra katika kufikiri (from Negative Mentality to Positive mentality ) huu ndio msingi mkuu wa kushinda katika Nchi.
Hivyo wajibu wa kupigania haki ni wajibu unaopaswa kuanzia kwenye familia , badala yake wajibu huu muhimu kama ibada umeachwa kwa Viongozi wa kisiasa peke yao. Hata makanisa makubwa na Misikiti zimeacha kabisa kuhubiri wajibu huu wamebaki wakipambana na uzinzi na konyagi katika ibada zao , wako wachache wanaojitahidi nao hawapaswi kupongezwa kwa kazi zao lakini kwa sababu ya fikra ya kizazi hiki kukwepa wajibu wake basi tuseme ni muhimu kuwapongeza.
Wakati naamka kuandika waraka huu, Mh Sugu yuko magereza pamoja na Kiongozi mwingine Masonga, safari yao itakuwa ndefu kidogo, uhuru wao wa kisheria kuhusu dhamana umedharauliwa na kuonewa , ninajaribu kuhisi tu ikiwa atafungwa mkakati wa Sugu kupoteza Ubunge unaweza kuwa hivi , baada ya hukumu Hakimu anaweza kuchukua likizo kwa hiyo kukataa rufaa kunaweza kuchelewa wakati huo tume itakuwa imeshaandikiwa na kutaarifiwa kuwa Jimbo liko wazi, naendelea kuona maono.... baada ya Tume kuharifiwa, Tume itaitisha Uchaguzi mara moja na Uchaguzi utafanyika na Mbunge atapatikana lakini baadaye Sugu atakuja kufanikiwa kukata rufaa au kumaliza kifungo chake na Ubunge wake utakuwa mwisho....ni nasema haya ni maono tu na sasa ni saa nane usiku sijui kwa nini naona maono haya....
Nini kifanyike kwa kweli nikiri kuwa sijui kwa sasa lakini tukitafakari na kumuomba Mungu tutapata njia..
Nimalizie kwa kusema kuwa tunapaswa kuingia kwenye wajibu mkuu sana wa kutafuta haki na kulinda haki kuliko wakati wowote wa maisha yetu.
Mungu alishasema katika vitabu vyake kuwa USIOGOPE , maana yake alijua kuwa kutakuwepo na vitisho lakini MSIOGOPE...sasa kama huu ndio msimamo wa Mungu kuhusu hofu basi nami naomba ubaki kuwa msimamo wangu na familia yangu.
MSIOGOPE....
Godbless Lema (MB )