PreGE2025 Janeth Ritte:Tupo tayari kumpigania na kumuunga mkono Dorothy Semu

PreGE2025 Janeth Ritte:Tupo tayari kumpigania na kumuunga mkono Dorothy Semu

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla)

DuaZaMama

JF-Expert Member
Joined
Jun 2, 2025
Posts
1,882
Reaction score
4,129
Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo, Janeth Ritte, ametangaza kwa msisitizo kuwa wanawake wa chama hicho wako tayari kumpigania na kumuunga mkono Dorothy Semu, Kiongozi wa Chama, kupeperusha bendera ya ACT katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza tarehe 28 Juni 2025 wakati wa hafla ya mapokezi ya Mbunge wa Viti Maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2020-2025), Nagy Livingstone Kaboyoka, aliyejiunga rasmi na ACT Wazalendo, Ritte amejibu vikali kauli zinazodai kuwa wanawake wameshindwa kuongoza.

Akiwa mbele ya viongozi wa chama hicho akiwemo Dorothy Semu na wanachama wa Ngome ya Wanawake, Ritte amesisitiza kuwa safari ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao imeanza rasmi kwao, na watahakikisha wanampigania Dorothy apate nafasi ya kugombea urais kupitia ACT Wazalendo.

Ameongeza kuwa kampeni ya mabadiliko ya kweli inaanza ndani ya chama chao, na kwamba wanawake wa ACT wako tayari kuonesha kuwa wanaweza kuongoza nchi kwa mafanikio makubwa.

Mbunge Nagy Kaboyoka amekaribishwa kwa heshima kubwa na viongozi mbalimbali wa chama, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya ACT Wazalendo, Magomeni, Dar es Salaam.
 
Back
Top Bottom