Jamal Khashoggi: kufa kufaana...

Jamal Khashoggi: kufa kufaana...

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,263
BARAZANI KWA RAJAB

Jamal Khashoggi: kufa kufaana

Na Ahmed Rajab

KAMA nilivyoeleza katika makala ya mwanzo niliyoandika kuhusu mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi (“Sema unayotaka kusema ujiendee zako”, Raia Mwema, Oktoba 17, 2018) nilikutana naye mara moja tu katika maisha yangu. Kadhalika, kama nilivyoeleza humo sikukubaliana na mengi ya msingi katika uchambuzi wake wa Mashariki ya Kati na wa siasa za kwao Saudi Arabia.

Tulikuwa na mitazamo tofauti kabisa. Juu ya hayo, ninamheshimu kwa msimamo wake wa kusema kweli na kupigania uwazi katika serikali ya kwao. Ni msimamo huo uliomfanya adhulumiwe maisha yake, tena kwa njia za kikatili kabisa.

Kwa sababu hiyo kila mpenda haki hana budi ila kuendelea kumkumbuka na kumuenzi. Na hivyo ndivyo wengi wetu tulivyofanya Jumatatu ya wiki iliyopita.

Jioni ya siku hiyo nilikuwa mmoja wa waalikwa kwenye kikao cha kumkumbuka. Kikao hicho kiliandaliwa na taasisi mbili zinazojihusisha na Mashariki ya Kati, Middle East Monitor (MEMO) yenye makao yake London na Al Sharq Forum yenye makao yake Istanbul.

Tulikutana kwenye ukumbi mmoja ulio katika mtaa wa Westminster, London, karibu na Bunge la Uingereza.

Khashoggi alikuwa na mahusiano na taasisi zote mbili. Mara kwa mara akitoa hotuba au akishiriki kwenye mijadala iliyokuwa ikiandaliwa na MEMO au na Al Sharq Forum, taasisi iliyoanzishwa na Wadah Khanfar, mkurugenzi mkuu wa zamani wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera. Siku chache kabla hajauliwa Khashoggi alizungumza katika taasisi zote hizo mbili.

Wote waliozungumza katika huo usiku wa “Kumkumbuka Jamal Khashoggi” walimwagia sifa kwa ujasiri wake wa kuthubutu kuwakosoa watawala wa Saudi Arabia na juhudi zake za kupigania mfumo wa siasa za Saudi Arabia ufunguke.

Maneno ya kusisimua na mazito yalitamkwa na mchumba wake Khashoggi, Hatice (Khadija) Cengiz, aliyeomba wafiwa wapewe maiti yao ili waisalie na kuizika mjini Madinah, Saudi Arabia, alikozaliwa na alikokuwa akiishi Khashoggi.

Kuna aliyetoa wito wa kuanzisha kampeni ya kuzitaka serikali za mitaa duniani kote zibadili majina ya barabara zilipo balozi za Saudi Arabia. Alitaka barabara hizo zipewe jina la Khashoggi.

Baadhi ya wasemaji walimtaja wazi mwana wa mfalme Mohamed Bin Salman kuwa ndiye aliyeamuru Khashoggi auawe. Hawakulibania jina hilo kama wafanyavyo wengineo wenye kumpiga vijembe Bin Salman au wenye kumtaja kwa mafumbo.

Kuna msemaji mmoja aliyemtaka mrithi huyo wa ufalme wa Saudi Arabia abadili jina na asijiite “Mohamed” na kulichafua jina tukufu la Mtume wa Rehma.

Tuhuma kwamba Bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kuuawa Khashoggi zimekuwa zikizurura Uturuki, Saudi Arabia na katika nchi za Magharibi mara tu baada ya kubainika kwamba mwandishi huyo ameuliwa.

Tuhuma hizo zilizidi kupata nguvu hasa baada ya Saudi Arabia kubadilibadili maelezo yake juu ya kilichomkuta Khashoggi na hatimaye kukiri kwamba waliomuua walikuwa Wasaudi na mpango wa kumuua ulikuwa umeandaliwa kabla.

Wakati shutuma dhidi ya Bin Salman zikizidi kupamba moto kuna “nzi” waliojitokeza kumtetetea. “Nzi” hao ni jeshi la wanamitandao wanaotumiwa kusambaza habari za uongo za kumuosha Bin Salman na kumpaka tope Khashoggi. Walikuwa wakiendesha shughuli zao wakiongozwa na Saud Al Qahtani, mshauri mkuu wa Bin Salman ambaye sasa kafutwa kazi, ingawa hatuna hakika iwapo yuko huru akiendelea kula unyunyu.

Kwa mujibu wa yaliyoachiwa yavuje na serikali ya Uturuki ni kwamba Qahtani, akiwa Riyadh, alikuwa akiwapa amri ya nini cha kufanya Wasaudi 15 waliosafiri kwenda kwenye ubalozi wao mdogo Istanbul, Uturuki.

Waturuki wanasema kwamba wakati mmoja akiwasiliana na wenzake kwa njia ya Skype Qahtani alianza kumtukana Khashoggi na Khashoggi akimjibu tusi kwa tusi. Mwishowe Qahtani aliwaambia wenzake: “Nileteeni kichwa cha huyo mbwa!”

Waturuki wanasema kuwa Wasaudi hao ndio waliomkaba roho na kumyonga Khashoggi mpaka akafa. Halafu walifanya unyama kwa kumkata mapande mapande mithili ya mnyama (kama tulivyoeleza wiki mbili zilizopita) na kuyatia mapande ya maiti yake katika masanduku matano.

Kuna tetesi zaidi kwamba baada ya kukatwa katwa baadhi ya mapande ya maiti ya Khashoggi yaliyayushwa katika asidi.

Tumesikia pia, ingawa bado hatujapata ithibati kwamba kichwa chake pamoja na kiganja cha mkono alipelekewa Mohamed Bin Salman. Ikiwa taarifa hii ni ya kweli hilo halitokuwa jambo geni Arabuni.

Historia ya huko ina visa vingi vya watawala wa kale waliotaka wapelekewe vichwa vya adui zao wakishauliwa.

Ama kuhusu kiganja chake cha mkono kinanikumbusha yaliyomfika Salim Al-Lawzi, mwandishi mahiri wa Lebanon na aliyekuwa mhariri wa gazeti la Al Hawadeth. Lawzi akiishi uhamishoni London baada ya kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe kwao 1975. Akiishi uhamishoni kwa sababu akihisi kwamba maisha yake yalikuwa hatarini Lebanon.

Bahati mbaya mama yake alifariki dunia Lebanon Februari, 1980 na akaamua kwenda kwao. Rafiki na jamaa zake walimsihi asende. “E bwana we, usende!” Waliokuwa karibu naye walimwambia.

Hakuwasikiliza. Mauti yalikuwa yakimwita. Yalimjongolea alipowasili uwanja wa ndege wa Beirut Februari 25, 1980. Watu wasiojulikana waliokuwa na bunduki walimteka nyara. Maiti yake ilikutikana siku tisa baadaye mahali panapoitwa Aramoun, kwenye viunga vya Beirut.

Maiti yake ilionesha ishara za kuteswa vibaya sana. Mkono wake wa kulia ulivunjika, kiganja cha mkono wake wa kuandikia kilivunjwa, vidole vyake viliunguzwa, vilikuwa vyeusi kama mashizi kwa kutumbukizwa kwenye asidi, kalamu zilichomwa na kuachwa tumboni mwake na ndani ya matumbo. Isitoshe, alipigwa risasi kichwani.

Inasemekana kuwa waliomtesa walikuwa watu wa usalama wa serikali ya Syria na mateso na mauaji yake yalikuwa ni onyo kwa wakosoaji wengine wa serikali ya Syria.

Khashoggi naye alikuwa mkosoaji; hakuwa mpinzani. Katika miaka miwili mitatu hii iliyopita alikuwa mkosoaji mkubwa wa baadhi ya sera za Mohamed Bin Salman, aliye mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia.

Mauaji ya Khashoggi yamesababisha jambo ambulo ni nadra kutokea katika siasa za Marekani. Nalo ni wabunge wa vyama vyote viwili vikuu, vya Republican na Democrat, kuwa na msimamo mmoja kuhusu suala moja.

Wote wamekirihishwa na kushtushwa na mauaji hayo. Wabunge hao hawayaamini maelezo yanayotolewa na serikali ya Saudi Arabia kuhusu kadhia hiyo. Wanaiona serikali ya Saudi Arabia kuwa isiyoaminika.

Hamna shaka kwamba mauaji ya Khashoggi yameuchafua uhusiano baina ya Marekani na Saudi Arabia, uhusiano ulioanzishwa na muasisi wa ufalme wa Saudi Arabia Abdulaziz Al Saud na Rais Franklin D. Roosevelt wa Marekani walipokutana kuanzia Februari 14, 1945.

Walikutana ndani ya manuwari ya Kimarekani, USS Quincy iliyokuwa imetia nanga katika Mfereji wa Suez, nchini Misri. Roosevelt alikuwa njiani akirudi Marekani kutoka mkutano wa Yalta uliojadili mustakbali wa bara la Ulaya baada ya Vita Vikuu vya Pili ya Dunia.

Alipokuwa katika safari hiyo, Roosevelt alitaka kuonana na baadhi ya viongozi muhimu wa Mashariki ya Kati na Afrika. Nao walikuwa Mfalme Farouk wa Misri, Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia na Abdulaziz al Saud, mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia.

Al Saud na Roosevelt walikutana kwa siku kadhaa wakizungumza kwa Kifaransa. Inasemekana kwamba Al Saud alikwenda kwenye manowari akiwa na kondoo wanane. Kila siku akichinjwa mmoja kwa chakula cha usiku.

Viongozi hao walisikilizana sana lakini Roosevelt alifariki miezi miwili baada ya mkutano wao. Rais aliyemfuatia Roosevelt yaani Harry Truman, hakuwa na usuhuba mkubwa na Al Saud kama aliokuwa nao Roosevelt.

Hata hivyo, waliyokubaliana baina ya Roosevelt na Al Saud, yaani masuala ya ulinzi na mafuta, ndio msingi mkuu wa uhusiano wa mataifa hayo mawili. Mauaji ya Khashoggi yameutikisa uhusiano huo na kuuingiza mashakani. Hivi sasa kumechomoza vigogo katika siasa za Marekani wenye kusema kuwa kuna haja ya kuutathmini upya uhusiano baina ya nchi yao na Saudi Arabia.

Lakini kama tujuavyo katika siasa za kimataifa na za uhusiano wa nchi moja na nchi nyingine kuna mambo fulani ambayo huzingatiwa hasa pale inapoonekana kwamba wakati umefika wa kuufumua uhusiano uliopo na kuufuma uhusiano mpya. Kuna ajenda, maslahi na mikakati ya kuzingatiwa.

Yaliyokuwa hayasemwi au yaliyokuwa yakinong’onwa tu, siku hizi yanasemwa wazi. Kuna wenye kutaka viongozi wakuu katika ufalme wa Saudi Arabia wabadilishwe.

Wasaudi wenyewe, hata miongoni mwa ukoo wa kifalme, wanataka pawepo mageuzi.

Bin Salman alimuondoa binamu yake Mohamed Bin Nayef aliyekuwa kiungo muhimu katika ushirikiano baina ya Marekani na Saudi Arabia. Ukoo mzima wa Al Saud umeelemea juu ya mgongo wa Marekani na unaitegemea serikali ya huko. Lakini Bin Nayef ndiye hasa mtu wao.

Wakati mmoja yeye ndiye aliyekuwa mrithi wa ufalme lakini 2017, Mfalme Salman alimuondoa kwenye wadhifa huo na akamteua mwanawe badala yake.

Siku hizi Bin Nayef hasikiki na wala jina lake halitajwi. Watu wanaogopa kuuliza yu wapi pakiwa na uvumi kwamba huenda akawa amewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani.

Hali ya Bin Nayef inaweza ikabadilika kutokana na mauaji ya Khashoggi kama ilivyobadilika ile ya Ahmed Abdulaziz Al Saud, ami yao Bin Nayef na Bin Salman.

Wiki iliyopita Ahmed alirudi Saudi Arabia kutoka London alikokuwa akiishi uhamishoni. Tangu arudi amekutana na nduguze pamoja na jamaa zake wengine. . Inasemekana kwamba wamezungumza kinagaubaga kuhusu namna ya kuuzima huu moto aliouwasha Mohamed Bin Salman na wenye kuutishia ufalme wa Al Saud.

Tukio jingine lisilotarajiwa ni kufunguliwa kutoka gerezani wiki iliyopita Khaled bin Talal Al Saud, mdogo wake bilionea Alwaleed bin Talal.

Waswahili tuna usemi: kufa kufaana. Asaa kifo cha Jamal Khashoggi hakitokuwa cha bure. Asaa kitasaidia kuleta mageuzi ya kimsingi Saudi Arabia na pengine hata kunusuru mauaji ya wengine nchini Yemen. Ndo maana tunaomba kifo chake kiwe na maisha marefu.
 
Siku zote uwezi kuelewa kitu ambacho utaki kuelewa ndio kanuni ya maisha ipo hivyo
Ndefu sana. Nimesoma naielewa lakini ndefu sana kwa jamii forums. Tawala zenye kunyamazisha watu Africa ndiko nyumbani kwake.

Sisi hapo hata ile kauli ya bring back Azory haisikiki tena.
 
naaam muandishi mkongwe ahmed rajabu kwa makala za midle east hana mpinzani.
 
Back
Top Bottom