Jaji Warioba: Namshangaa Sitta

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
Ahoji haraka ya kupata rasimu inatoka wapi, asikitishwa na kitendo cha Bunge kunyofoa vipengele muhimu katika rasimu, Asema Katiba itakayopatikana itakuwa sawa na iliyopo, ataka maoni ya wananchi yaheshimiwe

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema anashangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kung'ang'ania kuendelea na Bunge hilo licha ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia lifikie kikomo Oktoba 4 mwaka huu.

Hivi karibuni, Rais Kikwete alikutana na viongozi wa vyama vya siasa vilivyo chini ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na kukubaliana kusitisha mchakato wa Katiba hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalumu wiki hii jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ameshangazwa na uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao wakati uwezekano wa kukamilisha mchakato haupo.

"Hivi kuna haraka gani ya kuwa na rasimu katika Bunge hili? Mimi nilivyoelewa makubaliano ya Rais na TCD ni kama walikuwa wanasema kwa ustaarabu hebu twende polepole. Nimeambiwa kuwa Rais alitoa muda mpaka Oktoba 4, lakini uongozi wa Bunge ukapanga mpaka mwisho wa Oktoba," alisema Jaji Warioba na kuongeza:

"Mimi nafikiri makubaliano kati ya Rais na viongozi wa vyama ni kukataa kuongeza muda. Hiyo kwangu ni lugha ya kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki," alisema Jaji Warioba.

Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa kuhusu Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume yake, badala ya kujihami.

"Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate maoni ya watu ya kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema vibaya. Nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja," alisema na kuongeza:

"Sitta asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro."

Aliongeza: "Nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii tena. Ni wakati fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema…."

Alisema hatua ya uongozi wa Bunge kung'ang'ania kuendelea na mchakato ni kupingana na Rais Kikwete.

"Lakini mimi inanishangaza ilikuwaje Rais anatoa nyongeza ya hadi Oktoba 4, uongozi wa Bunge unaongeza hadi mwisho wa mwezi? Rais anasema hivi na Bunge linasema hivi. Mimi naomba uongozi wa Bunge utafakari tena," alisema na kuongeza:

"Kinachofanywa na uongozi wa Bunge la Katiba hakina shinikizo la CCM , bali ni uamuzi ambao unatokana na matakwa yao.

"Kama ni makubaliano ya viongozi wa vyama vya siasa na CCM walikuwapo, sasa kama chama kimeona hatuwezi kupata Katiba bora kwa nini tena uendelee?"

"Sheria ilisema Bunge lile litapewa siku 70, lisipomaliza litapewa nyingine 20, wakafanya tafsiri zao, kwani hizo siku 90 hazijaisha? Walipofikia wakati wakasema sasa tunakutana na Bunge la Bajeti tuahirishe, wakaahirisha. Kama mara ya kwanza liliwafanya wasitishe, nini kinawazuia kwa sasa?"

Alisema mbali ya tamko hilo, uongozi wa Bunge hilo umetangaza kuendelea na mchakato wakisema kuwa rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu.

"Nasikia wanaendelea, nasikia wanasema rasimu itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu. Hivi katika hali hii wanaweza?" alihoji Jaji Warioba huku akionyesha sura ya mshangao.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema ahadi iliyotolewa na Sitta ya kupatikana kwa rasimu ndani ya Septemba haitekelezeki.

"Sina tatizo na kuahirisha Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa waliona haiwezekani kupata Katiba kabla ya uchaguzi, lakini sioni uwezekano wa kumaliza kazi zote kwa wakati huu," alisema na kuongeza:

"Sioni kama wana muda wa kamati kuandika rasimu mpya ya kupigia kura, kwa sababu suala siyo kupiga kura tu, kuna mambo ambayo lazima kuwe na maridhiano na itachukua muda."

Akitoa mfano wa suala la Muungano, Warioba alisema ni kati ya mambo yanayohitaji maridhiano badala ya kuishia kwenye kupiga kura tu.

"Kwa mfano suala la muungano halitakwisha hivihivi bila maridhiano. Kuna mengine, nimesikia wanajadili Mahakama ya Kadhi, limejitokeza sana.

Litakapofika kwenye uamuzi, lazima kuwe na maridhiano. Wasipokuwa na maridhiano inawezekana wakaleta rasimu ambayo haina Mahakama ya Kadhi.

Je, wale wanaoitaka wakikataa una uhakika wa kupata theluthi mbili? Wale wanaopinga wakikubali utapata theluthi mbili?" alihoji.

Kupiga kura

Akizungumzia kauli ya Sitta ya kuwasiliana na balozi za nje ili kuhakikisha wajumbe waliosafiri huko wapige kura hukohuko, Warioba alisema kupiga kura peke yake hakutoshi kutoa uhalali wa Katiba bali maridhiano ndiyo msingi.

Aliongeza: "Mimi sielewi uongozi wa Bunge unafanya nini! Kwa sababu ukipitisha kitu kwa siri, hata kabla ya kufika kwenye kura ya maoni kikakataliwa na wananchi. Ni vizuri kutulia na kushauriana, wasiwe na haraka."

Amewashauri viongozi wa Bunge hilo kutafakari upya uamuzi wa kuendelea na vikao wakati Rais ameonyesha nia ya kuvisitisha.

Misimamo ya vyama imeharibu


Akieleza sababu za Bunge hilo kuyumba, Jaji Warioba alisema licha ya Tume yake kuwapa viongozi wa vyama vya siasa na wajumbe wengine nyaraka 10, lakini wameingiza misimamo ya vyama vyao:

"Mchakato ulipoanza kwa wale ambao tulikabidhiwa kazi hii, tuliamini tunaelekea kupata Katiba bora itakayotokana na maoni ya wananchi.

Sisi kwenye Tume hilo ndilo lilikuwa lengo letu. Tulijipanga tulivyoweza mpaka tukatoa rasimu ambayo kwa kiwango kikubwa ilizingatia maoni ya wananchi," alisema.

Jaji Warioba alisema mwanzo wa Bunge waliamini kuwa maoni ya wananchi yatazingatiwa, lakini baadaye walishangaa kuona maoni ya vyama ndiyo yanazingatiwa badala ya wananchi.
"Lazima nikiri kwamba mwanzo wa Bunge hilo haukuwa mzuri. Sisi tuliamini kwamba chochote kinachokuja kitaangalia tulichofanya kwa msingi wa kuona wananchi wamesema nini….

"Lakini walivyoanza ikabidilika kabisa ikawa ni kwa msimamo wa vyama. Tukatoka kwenye msingi wa maoni ya wananchi tukaingia kwenye maoni ya vyama."

Aliendelea kusisitza kuwa misimamo ya vyama ndiyo imeua matumaini ya kupata Katiba Mpya licha ya Tume hiyo kutoa nyaraka 10 za randama zinazoonyesha maoni ya wananchi na sababu ya mapendekezo ya rasimu hiyo.

"Nimewasikiliza kwa kirefu wajumbe wa Bunge la Katiba, inaonekana wengi hawakusoma taarifa tulizowapelekea. Tuliwapelekea nyaraka 10. Tuliwapelekea Rasimu, Randama inayoelezea kila ibara, maoni ya wananchi kisha sababu za mapendekezo," alisema na kuongeza:

"Baada ya hapo kuna vitabu vikubwa viwili vinavyoeleza maoni ya wananchi. Kuna kitabu kingine cha maoni ya mabaraza. Kuna kile cha takwimu na kitabu cha utafiti. Sasa pamoja na vitabu vyote hivyo, bado watu wanazungumza bila kuzingatia yaliyoandikwa."

Alisisitiza kuwa wajumbe wengi hawakusoma vitabu hivyo kwa sababu walikwenda bungeni na misimamo ya vyama vyao.

"CCM wana misimamo yao, Chadema yao, CUF na NCCR-Mageuzi nao wana yao."
Kufutwa kwa vipengele muhimu.

Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa mambo muhimu katika rasimu hiyo ya Katiba, Warioba alisema hali hiyo inatishia kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa.

Alisema baada ya kuondolewa kwa vipengele muhimu katika Rasimu ya Katiba ni wazi kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa tofauti na iliyopo sasa.

"Katiba Mpya siyo kuandika waraka mpya, ni kuona kuna tofauti gani kati ya katiba hiyo na ile ya zamani. Kuna maeneo fulani ambayo ndiyo yaliyofanyiwa mabadiliko. Lakini kutokana na mambo yanavyokwenda yale mabadiliko makubwa hayapo tena," alisema.

Aliyataja maeneo makubwa yaliyobadilishwa katika rasimu hiyo ni suala la maadili akisema kuwa wananchi walisisitiza kuporomoka kwake na kupendekeza njia za kudhibiti.

"Wananchi walikuwa wanataka lazima tuwe na mwongozo kwenye Katiba utakaowezesha kujenga utamaduni na maadili. Kwa hiyo katika rasimu tukaona kwenye utangulizi unaobeba misingi mikuu ya utaifa. Tukaona lazima kuimarisha misingi mikuu," alisema.

Alisema katiba ya sasa inasema misingi mikuu ni uhuru, haki, udugu na amani na kwamba wananchi walitaka yaimarishwe hayo.

Jaji Warioba alisema wananchi walisema huwezi kuzungumzia haki bila usawa, huwezi kuzungumzia amani bila umoja na katika umoja lazima kuwe na mshikamano.

"Lakini wakasema msingi wa kwanza ni utu, kwa hiyo Tume ikazingatia misingi yote ya utu na maadili ikafika misingi minane badala ya minne."

Alisema eneo lingine lililofanyiwa mabadiliko ni tunu ya taifa, akieleza kuwa wananchi walitaka ziwekwe kwenye Katiba kutokana na maelezo kwamba ndizo zinazojenga utamaduni wa Taifa.

Maadili ya Viongozi

Kuhusu maadili kwa viongozi, alisema walipendekeza, madaraka ya viongozi yawe ni dhamana, hivyo yawekewe kanuni, lakini Bunge badala ya kuheshimu maoni ya wananchi yamefanyiwa mabadiliko.

Alisema Tume yake iliangalia sheria ya maadili wakaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja.

Jaji Warioba alitoa mfano wa nchi ambazo hazikuwa na maadili ya viongozi madhubuti na kujikuta zipo katika matatizo makubwa kuwa ni Ufilipino.

Alisema katika nchi hiyo maadili ya viongozi yalikuwa yameshuka sana, rushwa imezidi, hivyo walipomwondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Ferdnand Marcos, maadili ya viongozi wakayaweka kwenye katiba.

Alitaja nchi nyingine ambazo zimeweka maadili ya viongozi kwenye katiba ni Afrika Kusini, Namibia na Kenya.

Aliendelea kusema kuwa hata zawadi wanazopewa viongozi zinapaswa kuwa za Taifa ili kuepusha kuchanganya masilahi ya Taifa na masilahi yao binafsi hasa pale viongozi wanapopewa zawadi wakati wa kutia saini kwenye mikataba ya Serikali.

"Kwanza wananchi walisema zawadi anayopewa kiongozi inakuwa ni mali ya Taifa. Wakasema viongozi wanaingia mikataba na wanajifikiria wenyewe.

Pili, katika kuimarisha maadili kwa viongozi Tume ilipendekeza kiongozi asiwe na akaunti nje kinyume cha sheria.

Tatu, iwe ni wajibu wa kiongozi kutangaza mali zake, kiongozi lazima atofautishe kati ya masilahi yake na masilahi ya umma, na kiongozi aepuke kutumia mali ya umma kwa masiahi yake.

Hata hivyo, alisema mwelekeo wa Katiba Mpya umebadilika hasa baada ya mambo hayo kuondolewa na kuyafanya kuwa sheria za kawaida.

"Wenzetu yaliwashinda wakayaweka kwenye katiba, sisi tunayaondoa. Nimeshangaa hata waliposema uwazi na uwajibikaji siyo tunu. Lakini katika nchi yoyote lazima uzingatie uwazi na uwajibikaji ili kuepuka ufisadi na wizi," alisema.

Kuhusu madaraka ya wananchi katika Katiba alifafanua haja ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao wakiwamo wabunge akisema kuwa mamlaka hayo yameporwa na kupewa vyama vya siasa.

"Wananchi walisema sisi ndiyo wenye madaraka ya katiba, sasa tunataka mbunge wetu asiwe waziri. Pili tunataka ubunge uwe na kikomo.

"Uchaguzi siku hizi siyo kitu ni kama mnada tu. Walisema kama mbunge ameshindwa tuwe na madaraka ya kumwondoa hata kama muda haujafika, kwa sasa hawawezi kuwaondoa kwa sababu ya rushwa," alisema na kuongeza:

"Lakini wamesema haiwezekani kumwondoa mbunge na watu watafanya mbinu za kuwaondoa wabunge. Lakini vyama vya siasa vimepewa mamlaka ya kuwaondoa wabunge na vimefanya hivyo. Wananchi wanaomchagua wanasema italeta matatizo."

Kuhusu wabunge kutokuwa mawaziri, alisema walifanya utafiti na kuona ugumu wa kutenganisha madaraka ya Serikali na madaraka ya Bunge kwa sababu Serikali iko ndani ya Bunge.

Alisema kwa mabadiliko waliyopendekeza wao rais aondolewe bungeni abaki kuwa mtendaji na amiri jeshi mkuu na mawaziri wake wasiwe wabunge.

Alisema hata hivyo mapendekezo hayo yamekataliwa kwa madai kuwa mfumo wa sasa waliouzoea ni wa kibunge ambao Waziri Mkuu anakuwa mbunge na anakaa bungeni.

"Kuna nchi zenye mfumo huo kama vile Uingereza, Canada, Australia, ni nchi za Jumuiya ya Madola, mkuu wa nchi siyo mtendaji mkuu, bali waziri mkuu ndiyo anakuwa mbunge. Lakini hapa unakuwa na rais katika Bunge ambaye haingii bungeni. Kunakuwa na mkanganyiko," alisema na kuongeza:

"Kinachofanyika ni Serikali inalibana Bunge ama Bunge linaingia katika mambo ya Serikali," alisema.

Muungano

Kuhusu suala la muungano alisema Bunge la Katiba limekuwa likijadili udhaifu wa Serikali tatu badala ya kuangalia udhaifu wa Serikali mbili, huku wakipanga kupunguza mambo ya muungano.

"Sasa hivi nasikia wanataka kuondoa mambo mengi zaidi ya muungano. Sisi tuliyaondoa kwa kuwa na Serikali tatu. Lakini kwa sasa watayaondoa bila kuweka utaratibu," alisema na kuongeza:

"Serikali ya muungano inashughulikia tu mambo ya Bara. Huoni Waziri wa muungano akivuka maji na kwenda kufanya kazi Zanzibar. Hiyo imeleta matatizo makubwa. Kwa kuwa Serikali ya Muungano inashughulikia zaidi mambo ya Bara," alisema.

Alitoa mfano wa mikopo akisema kuwa Zanzibar haiwezi kukopa kwa kuwa haitambuliki kama nchi kimataifa bali ni lazima ije bara na ipate dhamana.
Huku akitoa mifano ya dira na mikakati ya maendeleo, Warioba aliendelea kufafanua kasoro za muungano.

"Chukua mfano wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ni ya Bara maana Zanzibar wao wana Dira ya Maendeleo ya 2020.

Mikakati ya maendeleo kama Mkukuta ni wa Bara, Zanzibar kuna Mkuza. Kama ni hivyo, Wazanzibari wanakuja Bara kufanya nini? Kwa nini wanakuja kushiriki katika maamuzi ya bara? Hilo limekuwa ni tatizo la kisiasa na yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu."

Aliongeza suala la kuwapo kwa migongano ya Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar huku moja ikisema nchi ni moja na nyingine ikisema nchi mbili zilizoungana.
Jaji Warioba alisema kutokana na mabadiliko muhimu yaliyopendekezwa na Tume yao kuondolewa, huenda kukawa na Katiba yenye mabadiliko kidogo.

"Wamechukulia yale mambo ya uongozi tu, uwe na muundo mpya wa Tume ya uchaguzi, uchaguzi wa rais, Rais achaguliwe kwa asilimia 50 na zaidi, uchaguzi wa rais unaweza kuhojiwa mahakamani. Lakini yale ya wananchi yameachwa.

Haki za binadamu

Kuhusu haki za binadamu, Warioba alisema kuwa wananchi walitaka vikwazo vilivyokuwapo viondolewe, hivyo tume ilifanya marekebisho ikiwamo kuweka mgombea binafsi.

Baada ya uchaguzi Katiba itapatikana?


Kuhusu suala la kuahirisha mchakato hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Jaji Warioba alisema rais ajaye atalazimika kufuata sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kumalizia mchakato huo.

"Sheria ipo, sidhani kwamba akija atapingana nayo. Tumekusanya maoni, tumekwenda bungeni na tunangoja kura za maoni, kwa nini avunje sheria? Labda kwa kuwa sheria inasema wajumbe wa Bunge la Katiba ni pamoja na wabunge wa muungano, sasa kama hawakurudi sijui atafanyaje? Je, waendelee hao hao au wateuliwe wengine?" Alihoji.

Ardhi na Maliasili


Jaji Warioba pia ameshangazwa na Bunge hilo kuingiza masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa kwa siri akisema huko ni kuvuruga mchakato.

Alisema mambo hayo si ya Muungano na yanahitaji na yalipaswa kutolewa hadharani ili wananchi waone kwanza.

"Kuna mambo ambayo Bunge limeyafanya kwa siri. Wameingiza sura mpya kwenye rasimu, kuhusu ardhi na maliasili na Serikali za Mitaa," alisema .

Alisema kuziingiza kwenye rasimu lazima muwe na uhakika kwamba yatatumika pande zote, na kwamba bara wana utaratibu wao wa Serikali za Mitaa na Zanzibar wana utaratibu wao wa ardhi na maliasili ambao ni tofauti kabisa na ule wa Bara.

Alisema kuweka kwenye Katiba ya Muungano mambo hayo ni kuvuruga. Huku akitoa angalizo kuhusu umiliki wa ardhi na rasilimali zake, Warioba alisema kuwa hilo ni suala linalopaswa kujadiliwa na kila upande wa muungano:

"Sisi tuliliona suala la ardhi na maliasili, lakini kwa kuwa siyo suala la muungano tukaliacha. Wananchi walisema Serikali haithamini ardhi yao, mtu anahamishwa kwa lengo zuri tu la kujenga shule au barabara, lakini fidia anayopewa hailingani na thamani ya ardhi yake. Wanahesabu miti tu, hatuwezi kumletea maisha mtu huyu," alisema na kuongeza:

"Wanasema kama Serikali inapendelea wawekezaji wa nje na wa ndani. Hata hapa mjini matatizo yanatokea, watu wanahamishwa mtu mwenye uwezo akishatokea. Kwa mfano, mahali kuna madini wanaondolewa anapewa mwekezaji, mwananchi anaendelea kuwa masikini.

Ilitakiwa kuwe na utaratibu ambao mwananchi mwenye ardhi awe anapewa asilimia tano, Serikali za Mitaa asilimia 10 na Serikali Kuu asilimia 25, wanataka wafaidi. Ndiyo siri ya mambo ya Mtwara."

Jaji Warioba ambaye amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza rushwa ya mwaka 1996, alisema kuwa anafarijika kuona kuwa anaaminiwa na Serikali na matokeo ya kazi zake yanafanyiwa kazi ndani na nje ya nchi.

Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa katika kazi zake.

"Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate mrejesho wa kila aina. Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema na nilisemwa mengi sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja mmoja.

"Alivyosema Sitta nakubaliana naye, kazi ya binadamu haikosi kasoro na sisi hatukuamini kwamba kazi yetu haikuwa na kasoro. Ilikuwa nazo, kulikuwa na mambo labda tulipitiwa.

Ningefikiri, hayo anayosema angeyatumia na kwake, asifanye mambo kama hivi anavyofanya… Asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.

Lakini mimi nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii… ni kweli.

"Ni wakati fulani fulani mtu anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema. Bado nina matumaini, wananchi hawa wametoa mawazo ya msingi, tukiyazingatia tutapata Katiba bora, tusipoyazingatia tutapata Katiba itakayoanzisha mgogoro," alisema Jaji Warioba.

Chanzo:
Mwananchi
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi
 
Mzee wetu Warioba u did ur job better na hata hilo mungu ana kushuhudia ila huyu mungu mtu 6 ipo siku yake
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi
Kama kazi yake inachezewa aache kusema pambaf mkubwa wewe
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi

Humu jf huwa kuna Dr hivi atibu vichaa. Maana utakuwa umerukwa na akili
 
Kwa ujumla haya ndiyo maoni ya walio wengi nje ya BMK, na mambo yako wazi sana lakini Nchi hii ubinafsi ndiyo umetawala hakuna uzalendo tena, sasa kwa mtu kama Sitta kwa umri wake, uzoefu na yote ambayo nchi hii imemfanyia sikutarajia kwenye suala kama hili nyeti la Kitafa kulisimamia akiwa ametawaliwa na ubinfsi wa hali ya juu kama hivi ilivyo sasa.
Hata hivyo kwa hali yoyote katiba hii hata ikipita haitamaliza hata miaka 5 kwani ndiyo inaenda kuwa chanzo cha migogoro mikubwa katika nchi hii, na waliosababisha hili lazima historia iwahukumu.
 
kuna siku watanzania mtamkumbuka Mzee Warioba kwa busara na hekima zake
 
Warioba bado tunakuitaji kwa 92% MUNGU ATUVUSHE VEMA 2015 kitaelewaka tuu

Tanganyika kwanza………………
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi
wewe ni punguani au? kwani yeye siyo Mtanzania? Umetumwa na nani wewe? eti anavuruga amani! hiyo amani na kupewa katiba mbovu itatufaa nini? acha ushamba, mzee wa watu ana haki ya kusema kwani naye ni Mtanzaniia.
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi


wanaokusanya maoni kipindi hiki wanazeeka vizuri?
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi
Kwanini usijielekeze kujibu Hoja za Jaji Warioba. Unaposema anazeeka vibaya unamaanisha nini? Au wewe ndio unakuwa vibaya.
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi

mtu alopoteza muda wake usingizi wake familia yake nguvu zake leo unakuja najis kama ww mb..w...aa wa kufugwa unamtukana ww kweli umepatikana ohio street
 
Mzee wetu Warioba siyo peke yako unayemshangaa Sitta. Hatushangazwi na kuwa Mwenyekiti au kuliendesha Bunge bali kauli anazosema au kuruhusu kusema ndani ya Bunge hilo. Kwa hiyo farijika na ukweli huu.
 
Babu Warioba kazi mliyotumwa kuifanya na Rais mliifanya kwa weledi mkubwa. Cha kushangaza wabunge wabunge maalumu la katiba wanajifanya wanajua kuliko nyie mliojitahidi kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi na kuyachambua, mkapitia na yaliyojiri kipindi cha nyuma mkatupatia rasimu yenye muelekeo mzuri, wapi na wapi? Huyo mkiti wao ana agenda gani kwa nchi yetu? Je atakuwa tayari kuwajibika kama katiba wanayotaka kutupatia itatuletea matatizo ndani ya kipindi kifupi? Hivi nyi wabunge mlioko mjengoni kwa sasa mnaona mnatutendea haki kwa mnayojadili au lengo lenu ni posho tu? Hayo mambo ya msingi kwenye Rasimu ya Warioba mbona mmeyatoa?
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi

Wewe ndiye unazeeka mazuri!!?
 
Huyu mzee naye anazeeka vibaya. Ametengeneza rasmu, kazi yake imeisha. Mambo mengine ayaachie vyombo vingine. Huyu naona anataka kuvuruga amani na utulivu uliopo kwa uchochezi
Kageuza Tanzania Kama familia yake anayoweza kusema lolote wakati wowote. Ashindwe na alegee.
 
Back
Top Bottom