HAPO ZAMANI ZA KALE
Kulikuwa na marafiki watatu wanaopendana ambao majina yao ni Mike, Josh na Chris.
Kwa kweli hawa jamaa walikuwa ni marafiki wa kufa na kuzikana, hawakufichana jambo lolote iwe la kheri au shari.
Watu wengi waliowaonea sana wivu ikafikia hadi kutaka kuwaharibia urafiki wao lakini kwa jinsi walivyo marafiki wa kweli hakuna kilichoweza kuwatenganisha au juhudi za kuuvunja urafiki wao ziligonga mwamba kwa wale wenye vijiba vya roho.
Kuna siku marafiki hao walikuwa matembezini kwa ajili ya kujifurahisha nafsi zao ikiwemo kutembelea sehemu tofauti tofauti ikiwemo Mbuga, Mito, Maziwa, n.k. Ghafla kwa mbali wakiwa takribani umbali wa kilomita saba waliuona mlima.
Ikawabidi waliache gari lao na kuanza kutembea kuelekea mlimani sababu gari isingeweza kufika kuelekea mlimani kutokana hakukuwa na njia ya kuweza kuwafikisha kwa usafiri wa gari. Baada ya mwendo wa miguu wa takribani dakika 45 waliufikia mlima.
Na pale walipokuwa wanaanza kupanda mlima wakaliona pango kubwa sana. Bila kuleta ajizi wakaingia pangoni ile wanaingia tu wakaanza kuona madini ya Almasi na mengineyo tele aina tofauti tofauti yenye thamani ya hali ya juu. Kwa kweli walifurahi sana ikafikia hadi Mike kusema "hakika sasa sisi ni marafiki tajiri sana hapa ulimwenguni(tumetoka)".
Bila ajizi wakaanza kuzikusanya mali walizozikuta mle pangoni na kuanza kuzihifadhi kwenye mifuko yao kwa kila mmoja, wakiwa bado wapo kwenye zoezi la kujikusanyia Mali ghafla Chris na Josh wakashikwa na njaa na uchovu wa hali ya juu. Ikabidi Mike awaambie "ndugu zangu nawaona mmechoka na kubanwa na njaa ngoja niende ilipo Gari nikachukue chakula tulichokibakiza nije nacho tugonge(tule) ili tupate nguvu mpya kuendelea na zoezi letu la kujikusanyia Mali".
Chris akamjibu Mike "wazo zuri sana mimi nitaendelea kubaki na Josh hapa tukiendeleza zoezi la kujikusanyia Mali mdogo mdogo au kwa lugha nyingine tunaliendeleza libeneke taratibu" Baada ya Mike kuondoka Josh akapata wazo "Chris unaonaje tukimmaliza(tumuue) Mike ili hizi Mali zote tugawane mimi na wewe" Chris akajibu hata mimi nilikuwa nafikiria kitu kama hicho lakini ngoja kwanza arudi kisha tummalize"
Mike alifanikiwa kufika walipoliacha gari na kukichukua chakula kisha akawa anajiambia(kimoyo moyo) "kwanini nisiwawekee sumu Chris na Josh ili wapunguze idadi, na kisha Mali yote iwe yangu, hakika nikifanikisha zoezi la kuwaua Chris na Josh kwa kweli nitakuwa tajiri sana"
Alichokifanya Mike akachukua maji ya betri akayanyunyizia kwenye chakula na vinywaji vya wenzake wawili aliowaacha pangoni, bila na yeye kujua na yeye wawili aliowaacha pangoni wanamfanyia mpango wa kumuua.
Baada ya muda fulani Mike akawa na yeye amesharejea Mlimani alipowaacha marafiki zake Chris na Josh, lahaula ile Mike anafika tu akakaribishwa na visu kwa kweli walimchoma choma kifuani na kwenye tumbo kama walivyopanga mpango wao kwa kweli walifanikisha Mike alifariki dunia.
Baada ya kumuua Mike, Josh na Chris wakaanza kupata chakula(kula) kilicholetwa na Mike(marehemu) ili wapate nguvu mpya kujibebea mijifuko iliyosheheni Mali, walifakamia bila ya kufahamu kuwa chakula wanachokifakamia na vinywaji vilikuwa tayari vimeshanyunyiziwa sumu na Mike(Marehemu), Mungu si Athumani na wao(Chris na Josh) wakafariki dunia baada ya kufakamia chakula na vinywaji vyenye sumu.
Basi tena Mali zilibaki pale huku Marafiki wote watatu wakiwa wameshapoteza maisha, na hii yote sababu ya tamaa.
Kwa wengine inaweza kuwa hadithi, lakini kwa wengineo hili ni funzo tosha