Iran yaapa Trump atakiona chake

Iran yaapa Trump atakiona chake

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,267
IRAN inaitafsiri amri ya Rais Donald Trump wa Marekani iliyopelekea kuuliwa Meja-Jenerali Qassem Solaimani wa Iran Januari 3, 2020 kuwa ni mwanzo wa vita baina ya Marekani na Iran.

Kuna hata wasemao kwamba huo huenda ukawa ndio mwanzo wa vita vikuu vya tatu vya dunia.

Solaimani, aliyekuwa kiongozi wa kikosi maalum cha Quds cha Iran, aliuliwa kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad pamoja na vigogo wengine wa Iraq na Iran. Miongoni mwao alikuwa Jamal Ja’afar Muhammad Ali al Ibrahim, mwenye umaarufu kwa jina la Abu Mahdi al Muhandis. Kwa muda mrefu al Muhandis alikuwa kaimu kamanda wa kikosi cha al Hashd al Sha’abi, ambacho kiliongoza mapigano yaliyowashinda magaidi wa kundi liitwalo Dola la Kiislamu au Daesh, kwa ufupi wake wa Kiarabu.

Ingawa al Hashd al Sha’abi liliasisiwa likiwa jeshi la mgambo hatimaye lilikuwa sehemu ya majeshi rasmi ya Iraq.

Al Muhandis alikuwa na fungamano mahsusi na Kikosi cha Quds cha Solaimani. Mwishoni mwa Oktoba na mwanzoni mwa Novemba 2017 nilikuwa Baghdad kwa mwaliko wa ofisi ya Waziri Mkuu wa wakati huo Haider al Abadi.

Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa kuhudhuria kongamano maalum kuhusu ugaidi wa kimataifa na kuzuru baadhi ya miji ya Iraq. Siku moja tarehe 30 Oktoba al Mohandis alitualika waandishi kadhaa wa kimataifa kwa chakula cha mchana na kumsikiliza akitoa tathmini yake ya namna vita dhidi ya magaidi wa Daesh vilivyofanikiwa nchini mwake.

Ilikuwa fursa pia ya kumsaili kuhusu mambo mengi yenye kuhusika na usalama wa Iraq.

Bahati mbaya ninapoyaandika haya siko kwangu niko Ufaransa na, kwa hivyo, siwezi kuyanukuu niliyoyaandika kwenye shajara yangu ya siku hiyo.

Hata hivyo, kuna machache ninayoyakumbuka: upole wake al Mohandis, kutojitweza kwake na umahiri wake wa kuelezea mikakati ya kivita. Na huwezi kukutana naye usiuhusudu ushujaa wake wa kutokiogopa kifo.

Kuuliwa kwa al Muhandis kumewafanya Wairaqi wengi wazidi kudai kwamba majeshi yote ya kigeni na hususan ya Marekani yaondoshwe nchini mwao.

Na kwa upande wa Iran, angalau kwa sasa mauaji ya Solaimani yameuimarisha umoja wa viongozi wa Iran. Uhasama uliosemekana kuwepo, kwa mfano, baina ya Solaimani na Rais Hassan Rouhani hivi sasa umeyayuka.

Solaimani hakuwa mwanajeshi wa kawaida. Kwa muda wa miaka 22 amekuwa akikiongoza kikosi cha Quds kilichowafyeka magaidi wa Daesh kutoka Syria. Hiki pia ni kikosi maalum kilicho sehemu ya jeshi la mgambo la Walinzi wa Kimapinduzi lenye idadi ya wanamgambo wasiopungua 125,000.

Jeshi hilo lina dhima kubwa sana na kazi nyeti. Miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia mpango wa makombora ya Iran, majeshi ya wanamaji yenye kuzifuata nyendo za manowari za Kimarekani zilizo katika Ghuba na jeshi hilo la mgambo pia lina kikosi cha Basij, cha raia waliojitolea kupigana.

Jeshi la Walinzi Wakimapinduzi linawajibika kwa mtu mmoja tu: kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

Hamna shaka yoyote kwamba kifo cha Solaimani ni pigo kubwa kwa Iran. Hiyo ni sababu ya kutosha ya kuifanya Iran ilipize kisasi kwa njia ambayo Marekani haitosahau.

Ulimwengu haujawahi kushuhudia mazishi ya mtu kama ulivyoshuhudia mazishi ya Qassem Solaimani yaliyohudhuriwa na maelfu kwa maelfu ya watu katika mji wa Kerman.

Solaimani akijua kwamba atauliwa na Wamarekani na kwamba atakufa shahidi. Katika wasia aliouandika kwa mkono wake mwenyewe, Solaimani aliandika yafuatayo:

“Mke wangu, nimechagua wapi nizikwe katika Makaburi ya Mashahidi wa Kerman, Mahmoud anapajua. Nataka jiwe la kwenye kaburi langu lisiandikwe mengi. Andikeni tu ‘Mwanajeshi Qassem Solaimani’ hakuna tena vyeo na vifungu vya maneno.”

Trump anajihisi kwamba ni mwerevu kwa sababu ya uzoefu wake wa kutumia hila za vita vya kisaikolojia. Miongoni mwa hila hizo ni kuwatia ndaro mahasimu zake na kuwatisha.

Trump amekuwa na tabia hiyo tangu alipokuwa mfanyabiashara. Hila zake zimekuwa kutumia vitisho ili mahasimu zake wasalimu amri na, hatimaye, wawe wanafanya ayatakayo yeye.

Katika watu waliomshinda ni Kim Jong-un, kiongozi wa Korea ya Kaskazini, na Wairani. Trump alimkebehi na kumtisha Kim lakini Kim alisimama kidete akivijibu vitisho vya Trump kwa vitisho vyake. Mwishowe tuliona jinsi Trump alivyokuwa kama aliyempigia magoti Kim na akakubali kukutana naye.

Solaimani na al Mohandis walipata mafanikio makubwa katika kupambana na magaidi wa Daesh katika Iraq na Syria. Kuna swali tunalopaswa kujiuliza tunapozungumzia suala la magaidi wa kimataifa.

Nalo ni kwa nini magaidi hao hawakuwahi kwamwe kuishambulia Israel? Hawakuwahi kuishambulia Israel licha ya ahadi iliyowahi kutolewa na aliyekuwa kiongozi wao Abu Bakr al Baghdadi kwamba wataigeuza Israel iwe “kaburi la Wayahudi”.

Ahadi hiyo ilitolewa miaka michache iliyopita al Baghdadi alipokuwa hai na magaidi wa Daesh walipokuwa na nguvu lakini magaidi hao hawakuwahi kuugusa hata unywele wa Israel. Kwa nini?

Kwa muda sasa kumekuwa na tetesi kwamba kundi la magaidi hao limeundwa na Israel kwa ushirikiano na Marekani. Wenye kuamini hivyo wanahoji kwamba ushirikiano wa mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi — shirika la CIA (Marekani), Mossad (Israel) na MI6 (Uingereza) ndio uliowawezesha magaidi hao wa Daesh wapate kwa rahisi silaha nzito nzito.

Tetesi hizi zilithibitishwa na Jenerali Wesley Clark aliyewahi kuwa kamanda wa NATO, Umoja wa Kijeshi wa nchi za Magharibi, aliyesema waziwazi kwenye mahojiano na kituo cha Televisheni cha Marekani, CNN, kwamba marafiki wa Marekani, akimaanisha Israel, wameliunda kundi la Daesh ili lipigane na kuliangamiza vuguvugu la Hezbollah nchini Lebanon.

Mpango wa nchi za Magharibi umekuwa kuhakikisha kwamba Israel iko salama, haibughudhiwi wala haitishiwi na yoyote. Ili lengo hilo litimie ni lazima nchi zilizosimama kidete dhidi ya Israel zisambaratishwe.

Ndipo bongo la Israel lilipofanya kazi na kuandaa mkakati wa kuziangusha tawala za Libya, Iraq, Syria, Somalia, Sudan, Iran na vuguvugu la Hezbollah nchini Lebanon.

Marekani, kupitia shirika lake la Ujasusi la CIA, lina uzoefu wa kupanga njama dhidi ya Iran. Mnamo Agosti 1953 ilikula njama ambazo kwa siku nne ziliipindua demokrasia ya Iran kwa kuiangusha serikali ya waziri mkuu Mohammad Mossadegh.

Kilichomchongea Mossadegh ulikuwa mpango wake wa kuyataifisha mafuta ya Iran. Kwa muda wa miaka mingi Uingereza ndiyo iliyokuwa ikiyadhibiti mafuta ya Iran kupitia kampuni ya Anglo-Iranian Oil Company (AIOC. Uingereza ndiyo iliyokuwa na udhibiti ikiipunja Iran. Kwa mfano, mnamo 1947 kampuni hiyo ilipata faida ya pauni za Kiingereza milioni 40 lakini Iran iligaiwa pauni milioni 12 tu.

Machi 1951, bunge la Iran, Majlis, lilipiga kura kuitaifisha kampuni ya AIOC. Baada ya mashaurino ya miezi kadhaa, waziri mkuu wa Iran Mossadegh akayavunja mazungumzo hayo na akainyima Uingereza fursa ya kushiriki katika uchimbaji na uuzaji wa mafuta ya Iran.

Ndipo Uingereza ilipoomba msaada wa Marekani kuingilia kati kwa niaba yake. Na ndizo afisa mmoja mkuu wa CIA, Kermin Roosevelt Jr, mjukuu wa Rais Theodore Roosevelt, alipoandaa mpango wa kumpindua Mossadegh.

Alijaribu mara mbili. Mara ya kwanza alishindwa kumkamata Mossadegh nyumbani kwake usiku wa manane. Mara ya pili alifanikiwa na uhusiano baina ya Marekani na Iran ukaimarika wakati wa utawala wa Shah, mfalme wa Iran.

Uhusiano huo uligeuka na kuwa wa kutoaminiana baada ya Shah kupinduliwa na wafuasi wa Ayatollah Khomeini.

Baada ya kuuliwa Solaimani, kuna jemedari asiyejulikana sana nje ya Iran aliyechomoza kutoka kwenye vivuli vya nchi hiyo. Esmail Ghaani, mwenye umri wa miaka 62, ndiye aliyeteuliwa kuyarithi madaraka ya Soleimani kwa kuliongoza Jeshi la Quds.

Ghaani anamshabihi Soleimani kwa mengi. Kwa muda mrefu wamekuwa marafiki wakubwa. Usuhuba huo ulitia mizizi tangu walipokuwa vijana wakipigana dhidi ya majeshi ya Saddam Hussein huko Iraq katika miaka ya 1980.

Marekani imo gizani kwa vile haijui muelekeo wa Ghaani utakuwa upi. Inachokijua ni kwamba kwa muda mrefu amekuwa na nguvu ndani ya vyombo vya ulinzi vya Iran.

Marekani ilimuekea vikwazo 2012 ikimshutumu kuwa alikuwa akiyapa fedha makundi ya wapiganaji wa kigeni yenye kushirikiana na Kikosi cha Quds. Pia ilimhusisha na silaha zilizokamatwa 2010 kwenye bandari moja ya Lagos, Nigeria.

Wakati huo serikali ya Nigeria ilisema iliyashika makombora ya aina ya Katyusha, risasi pamoja na silaha nyingine. Raia mmoja wa Iran pamoja na mshirika wake wa Kinigeria walihukumiwa vifungo vya miaka mitano jela kwa kuhusika na kadhia hiyo. Inavyosemekana ni kwamba silaha hizo zilikuwa njiani kupelekwa Gambia.

Lakini wakuu wa Israel walidai kwamba silaha hizo zilikuwa zipelekwe kwa wanaharakati wa Gaza. Serikali ya Nigeria nayo ilidai kwamba zilikusudiwa wanasiasa wa Nigeria ili wazitumie wakati wa uchaguzi. Zote hizo zilikuwa dhana.

Inachosema sasa Marekani ni kwamba lazima Ghaani atahusika na kisasi cha kumlipizia Solaimani. Inasemekana kwamba Wairani wamekwishakipika chakula chao cha kisasi kwa mauaji hayo na wanasubiri kipoe tu walmishe Trump. Wairani wenyewe wanakubali kwamba wanao mpango wa kulipiza kisasi ingawa hawakusema bado wanafikiria kufanya nini. Nao si wapumbavu wa kubobojokwa hivyo.

PHOTO-2020-01-06-08-34-12.jpeg
PHOTO-2020-01-06-10-34-30.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aisee this pain sana kwa marekani wamezidi kujichafua kwa huu utawala wa tramp.

Machafu mengi na vitisho vyenye ishara hatarishi kwa nchi zenye kujiweza

Nadhani tramp ajitasmini upya yeye na utawala wake.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aisee this pain sana kwa marekani wamezidi kujichafua kwa huu utawala wa tramp.

Machafu mengi na vitisho vyenye ishara hatarishi kwa nchi zenye kujiweza

Nadhani tramp ajitasmini upya yeye na utawala wake.

Sent using Jamii Forums mobile app
Vingine muwe mnaacha vipite tu.
Tramp = TRUMP
 
BREAKING: Iranian official tells state television that his country can hit a hundred other American targets if the Trump Administration retaliates

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom