Ooh! Toka lini unga uwe na bei kuliko mchele?
Wafanyabiashara waliokuwa hawalipi kodi wamebanwa kulipa kodi na wao wanakomoa wanunuzi kwa sababu wanunuzi hawajui wanalipishwa kodi asilimia ngapi. Na hakuna patamu pakuwabana wanunuzi zaidi ya kwenye ugali.
Hapo cha kufanya ni kuususia ugali, unga ukiwadodea wafanyabiashara watapunguza bei.
Lakini mbongo utamwambiaje aache kula ugali? Kama unga ni bei kubwa kuliko mchele hilo mbona ni tatizo zuri. Wali bamia, wali mbilimbi, wali mchicha, wali dagaa haviendi?
Tanzania imejaliwa vyakula vingi sana. Suburi mwezi wa Ramadhani vingine hata majina huvijui.
Ukiacha mahindi kuna mchele, mtama, ulezi, ngano, maharage, kunde, mbaazi, mbaazi, choroko, njegere, njugu mawe, magimbi, mihogo, viazi mbatata, viazi vitamu, ndizi za kila aina nakadhalika.
Kwanza ugali hauna lishe yeyote ya maana ni maji ya moto na unga tu hauna hata chumvi.
Mkulima asipolima mahindi mwaka huo anajiona hajalima. Ungekuwepo utamaduni wa kula vyakula tofauti zaidi ya ugali na wali hivi vyakula vingine pia vingelimwa kwa wingi na vingine ni rahisi kuvilima na vinavumilia hata ukame.
Watu wa nchi zilizoendelea huwezi kuwabana kwenye chakula fulani kwa sababu wanakula vyakula vya aina nyingi.
Watanzania kubadilika ni muhimu. Mabadiliko huanzia majumbani kwa watu sio kusubiri serikali ibadilishwe.