Imani za miujiza

Almagedoni

Member
Aug 1, 2022
10
8
Imani ni hakika na bayana ya mambo yatarajiwayo, ni kuwa na hakika na jambo kutokea au kutimilika pasipo shaka. Kila mtu amekuwa na kile anachokiamini, japo kuwa sote tunaamini uwepo wa Mungu. Ni nadra sana kusikia mtu haamini uwepo wa Mungu. Hii yote imetokana na hitaji la mwanadamu katika kutafuta furaha na hitaji la moyo wake, ikiwemo utajiri, uponyaji, mali pengine umaarufu. Hali hii imepelekea kuibuka kwa madhehebu mengi yanayoambatana na kampeni ya miujiza ya uponyaji. Naiita kampeni kwa sababu ya utitiri wa matangazo kwenye vyombo vya habari na vipindi vya kuhamasisha imani ya miujiza zinazoendeshwa na wanaojiita manabii.

Ni vizuri kuwa na mawazo chanya kwenye kila kitu mtu anachokifanya, hayo hupelekea kukua kwa Imani juu ya kitu hicho. Na mafanikio huhitaji imani inayoambatana na utendaji yaani vitendo. Pasipo matendo sote tunatambua kuwa hakuna Imani. Kinachosikitisha ni Imani za uponyaji zimejikita kuhamasisha watu kuamini kwenye vitu na siyo kwenye kiini cha Imani hiyo yaani MUUMBA WA MBINGU NA NCHI NA VYOTE VILIVYOMO. Imekuwa kawaida kuona umati mkubwa wa watu wakiwa wamebeba vitu kama vile chumvi, picha, maji, kalamu, daftari, sahani na masufuria kupeleka sehemu za ibada hizo za maombezi.

Huduma hizi huambatana na kupanda mbegu yaani utoaji wa pesa, mtu hulipishwa tozo ili kupata miujiza. Hivyo imeripotiwa kuwepo kwa athari mbalimbali kutokana na imani hizo, miongoni mwa athari hizo ni kwenye ndoa na uchumi.

Athari za Imani ya Miujiza
Kwa upande wa ndoa, imejitokeza changamoto kubwa leo pale wanandoa wanapokuwa na mitazamo tofauti ya kiimani. Imeleta migongano ya mara kwa mara na hatimaye kuvunjika kabisa. Watu wamekuwa kama waliopagawa kwa sababu ya hali zao za ufahamu zinakuwa kama zimefungwa wasisikilize kitu au jambo lolote kutoka kwa mtu mwingine. Hivyo si ajabu ukakuta mwanandoa mmoja akawa hamsikilizi tena mwenzi wake. Muda mwingi huutumia kwenye majumba ya hao wajitao manabii akiwahudumia kwa kila jambo kuliko anavyomhudumia mwenzi wake. Mwishoe, hujikita katika mahusiano kwa kisingizio cha kupata maono ya huduma iweze kuendelea.

Visa hivyo ni vingi sana, watu hutumia vibaya imani kwa kisingizio cha kupata miujiza. Mnamo mwaka (2017), huko kagera iliripotiwa Mchungaji kumuoa mke wa muumini wake kwa madai ameoteshwa na Mungu. Unaweza pata habari kamili kwenye hii link-https://millardayo.com/kg9/. Mwaka ( 2013), pia nabii mmoja Jijini Dar es salaam alituhumiwa kuzaa na mke wa mtu, hii ilipelekea mume wa mke huyo kumfungulia nabii mashtaka. Unaweza ipata habari hii Tuhuma za Kuzaa na Mke wa Mtu, MWINGIRA aburuzwa Kortini. Hayo ni baadhi tu ya matukio yaliyokwisha ripotiwa hadharani, kiuhalisia ni mengi ambayo hayajawekwa wazi. Familia ambayo mke au mume ni muumini wa hizi Imani za miujiza zimekuwa na migongano isiyokwisha hasa zikihusiana na wivu wa kimapenzi.

Kisaikolojia, mtaji wa mtu kufanikiwa ni afya njema ya akili. Na uwepo wa imani yake kwa kile anachokiamini humletea faraja na amani. Inapotokea mvurugano basi imani huathirika na akili kwa ujumla. Imani za miujiza imekuwa ikiwajengea wanadamu hofu ambayo huathiri akili kwa kiasi kikubwa. Watu huaminishwa kuwa wamerogwa au wamefungamanishwa kwenye mizimu yao. Mambo hayo husababisha hofu kwa mtu na kupelekea kutojiamini mwishoe hupatwa na uoga.

Kiuchumi, hitaji la kila mwanadamu kufanikiwa kiuchumi, kuwa na uwezo wa kifedha ili kumudu gharama za maisha. Kupitia mtego huu imani ya miujiza imewavuta wengi kuamini mafanikio ya utajiri kwa njia ya maombezi pasipo kufanya kazi. Unakuta familia inafilisika kwa sababu ya kupanda mbegu kwenye huduma za miujiza. Pia kutumia muda mwingi kwenye huduma hizo zimepelekea anguko la kiuchumi.

Mambo ya kufanya ili kuepuka athari hizo;
Kila muumini kwa imani yake ajidhatiti kufahamu misingi ya imani ya dini yake, hii itasaidia kuepuka udanganyifu kutoka kwa baadhi ya watu wanaotumia vazi la kidini kulaghai na kujipatia kipato. Kila muumini asiwe mtu wa kusubiri kuambiwa ,bali kila mtu awe mfuatiliaji, mdadisi na msomaji wa maandiko matakatifu ili kuweza kupima mafundisho kabla ya kuchukua hatua ya kuamini.

Kila familia itoe mafunzo kwa watoto wao kuwa hakuna mafanikio yanayokuja kwa kutegemea miujiza, ni wajibu wa kila mmoja kuwajibika na kujituma ili kupata mafanikio. Kazi ifanywe kwa bidii pasipo ulegevu, akili ijazwe mawazo chanya na imani kwa kile kinachofanyika.

Waumini wafundishwe kuamini neno la Mungu na sio kuamini mtu au watu (nabii au mchungaji), Mungu ndiye mpaji wa vitu vyote kwahiyo tunapaswa kujenga imani kwake. Tukijenga imani kwa vitu au watu tunakosea na inakuwa rahisi kudanganyika.

Mwisho, Ndoa iheshimiwe na watu wote, waliomo na wasio kwenye ndoa hainabudi kuheshimu maaganao. Ewe ndugu usiruhusu mtu yeyote kuingilia ndoa yako kwa kigezo cha kidini. Hakuna dini au imani yoyote inayokubali kuingilia ndoa ya mtu mwingine.

Hitimisho
Kwa kuwa mambo haya yako wazi mbele zetu nitoe rai kwa kila mmoja wetu kupinga imani zote zinazopotosha na kuleta sintofahamu kwenye jamii. Tuhimizane kufanya kazi kwa bidii. huku tukiomba amani katika maisha yetu ya kila siku.
 
Back
Top Bottom