Idadi ya waliokufa yaongezeka

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
KATIKA kujibu hoja ya Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha aliyetaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Mapinduzi (CCM) vikae kuzungumza namna ya kumaliza mfarakano ulioleta maafa jijini Arusha, CHADEMA kimekataa pendekezo hilo kwa maelezo kuwa CCM na serikali yake ni katili na ya kihuni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika hospitali ya Mount Meru alikokwenda kuwajulia hali majeruhi wa vurugu hizo, akiwamo mchumba wake Josephine, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilibrod Slaa alisema: ”Hatuwezi kukaa meza moja na serikali ya kihuni. Tumepigwa, tumedhalilishwa huku tukiwa na vibali vyote halali vya kuturuhusu kufanya mkutano na maandamano, halafu haohao wanasema tukae meza moja kujadili nini?”

Alisema pendekezo la Waziri Nahodha limechelewa na kwamba chama hicho kwa hivi sasa hakiwezi tena kukaa meza moja na CCM kujadili mvutano uliojitokeza kwani wakati serikali ilipoungana na CCM kuhujumu uchaguzi wa meya ilikuwa inajua matokeo yake.

Alisema pendekezo la mazungumzo sasa hivi ni ghiliba ya serikali kuhujumu harakati za mabadiliko ya Watanzania wakiongozwa na CHADEMA.

Alisema kitendo cha serikali kushambulia, kupiga na kuua waandamanaji badala ya kuwalinda ni uhuni usioweza kuvumiliwa; na kwamba CHADEMA haiwezi ’kununuliwa’ kwa mazungumzo ya mezani.

Akizungumzia mchakato mzima wa kufanya mkutano na maandamano, alisema mchakato huo ulianzia mwaka jana ambapo yeye kama katibu aliwasiliana hadi na Msajili wa Vyama kuhusu suala hilo, tena kwa maandishi.

Alisema kuwa Desemba 22 mwaka jana alimuandikia barua Msajili John Tendwa kumjulisha suala hilo na yeye akaahidi kulifanyia kazi kwa kuwasiliana na mkuu wa jeshi la polisi na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Mkuchika ili kuona uwezekano wa kuitishwa uchaguzi mpya katika maeneo yaliyokumbwa na matatizo.

Januari 3 mwaka huu Msajili aliwasiliana naye kwa simu kutaka kujua makubaliano ya awali, akaahidi kuwa kabla ya Januari 4 angekutanisha pande zote kujadiliana suala hilo.

Jioni ya Januari 3 Tendwa alimpigia (Dk. Slaa) simu na kumwambia kuwa waendelee na taratibu zote za maandamano pamoja na mkutano wa hadhara na akashauri katika mkutano huo wazungumze kiistaarabu na wasitoe kashfa kwa yeyote ili chama kiendelee kupata heshima kwa jamii.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa akiwa njiani kuelekea Arusha Januari 4, Tendwa tena akampigia na kumuuliza alikuwa wapi na alipomjibu kuwa yuko njiani kuelekea Arusha akamuuliza kama walikuwa tayari kuahirisha mkutano endapo waziri wa TAMISEMI angetangaza kurudiwa kwa chaguzi zote za mameya katika maeneo yaliyokumbwa na vurugu. Dk Slaa akamjibu kuwa ni vigumu kuahirisha mkutano kwa kuwa umeishaandaliwa kwa gharama kubwa.

”Baada ya kuwasiliana na kuelezana hayo nilimtania kidogo Tendwa nikamuuliza kwa kuwa alikuwa nyumbani Same ’niambie wapi ntakuta mahindi yangu ya kuchoma ili nikifika Arusha nikayachome nile’ kwa kuwa huwa mara nyingine nataniana naye,” alisema Slaa.

Alisema kuwa simu za Tendwa hazikuishia hapo na baadaye siku hiyo hiyo saa 12 jioni alinipigia na barua kadhalika alituma.

“Na mimi bahati nzuri nikafahamishwa na watumishi ofisini kuwa imeishafika, na hivyo Tendwa tena, akaniambia anawasiliana na Mkuchika kujua kama ameishatoa tangazo la kufanyika kwa chaguzi,” alisema.

Katika hilo Slaa alisema kutokana na hayo yote aliyoyafuata kitaratibu kufanikisha mkutano huo na barua ya mkuu wa polisi wilaya (OCD) kuruhusu kibali cha maandamano na mkutano na kuambulia kupigwa sasa, hawaoni sababu za kukutana na serikali ya aina hiyo kujadiliana nayo.

Maaskofu walaani polisi, wamkataa meya Arusha

Katika hatua nyingine, umoja wa maaskofu wa Kikristo Mkoa wa Arusha wametoa tamko kulaani ubabe na ukatili wa polisi kupiga na kuua waandamanaji.

Akisoma tamko hilo la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake wanaounda umoja huo jana katika hoteli ya Korridor Spring, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu, alisema Jeshi la Polisi ndilo chanzo cha ghasia na mauaji hayo na ndilo linapaswa kubeba lawama.

Alisema machafuko hayo kwa kiasi kikubwa, yalisababishwa na polisi iliyotoa maamuzi mkanganyiko yaliyowachanganya wananchi.

“Wao walitoa kibali cha kufanya mkutano na maandamano, halafu mara ghafla, dakika za mwisho, wanakataza maandamano; na kama hiyo haitoshi wanatumia nguvu kubwa kuwatawanya watu kwa mabomu na risasi. Kwa nini wanasababisha vurugu badala ya kuzuia?” alisema Askofu Lebulu.

Askofu huyo alitamka wazi kuwa maaskofu hao, wakiwa sehemu ya wananchi, hawamtambui Meya Gaudensi Lyimo aliyechaguliwa kinyemela kwa kuwa hakupatikana kihalali; akasisitiza kuwa hawako tayari kufanya kazi naye.

Alisema kuwa wao kama umoja wa viongozi wa dini mkoa wa Arusha wanaitaka serikali kuchukua tukio la Arusha kama jambo la kitaifa kwa kutoa maelezo ya kutosha na ya kuridhisha kwa Watanzania wote na jamii ya kimataifa ili kurejesha na kujenga upya imani ya wananchi kwa serikali yao.

“Sisi tunataka haki itendeke na haki ionekane imetendeka. Uchaguzi haukuwa huru wala wa haki, maana hata vyombo vya habari vilituhabarisha kuwa wengine hawakupiga kura na wengine wasiokuwa wakazi wa Arusha walipiga kura. Hili jambo linatakiwa nalo lifanyiwe uchunguzi,” alisema Askofu Lebulu.

Alisema njia pekee ya serikali kuifanya nchi iwe na amani na kuongozwa kidemokrasia, ni kwa serikali kutenda haki kwa kufanya uchaguzi mwingine ambao utakuwa huru na wa haki.

Idadi ya waliokufa yaongezeka

Wakati huo huo, idadi ya raia waliokufa katika vurugu hizo imeongezeka kutoka watatu hadi wanne, huku polisi wakibainika kumuua pia raia mmoja wa Kenya, aliyefariki katika Hospitali ya Mount Meru.

Awali, polisi walikuwa wametangaza kifo cha raia aliyetambulika kwa jina la George Waitara, lakini baadaye imegundulika kuwa marehemu hakuwa Mtanzania na jina lake halisi si Waitara bali Paulo Njuguna Kaiyela.

Njuguna amefahamika baada ya kupatikana kwa vitambulisho vyake ambapo kitambulisho chake kinamtambulisha kama raia wa Kenya kina namba 25066938 na sirio namba yake ni 218733089.

Hadi jana kulikuwa na majeruhi 17 katika hospitali za Mount Meru na St. Theresa. Miongoni mwao, 11 walijeruhiwa kwa risasi na wawili miongoni mwao ndio waliotolewa vipande vya mabomu. Baadhi ya majeruhi bado wana risasi mwilini na wamelalamikia kuchelewa kutolewa risasi hizo.

Kati ya majeruhi hao, yumo mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito, ambaye kutokana na kipigo alichopewa na polisi mimba yake imeharibika na kutoka.

Majeruhi mwingine ambaye ni dereva wa Mbunge wa CHADEMA, Grace Kiwelu, amepoteza uwezo wa kuhisi, na pia miguu imekufa ngazi.

Madaktari waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa wanaogopa kumpeleka hata kwenye chumba cha X-ray kwa sababu hali yake inaweza kuwa mbaya zaidi.

Akizungumzia malalamiko ya majeruhi hao Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Mount Meru Salash Toure alisema majeruhi wameishapata huduma ya awali mpaka sasa.

Alisema wale ambao bado wana risasi mwilini wamepatiwa dawa za kupunguza maumivu ili kusubiri uchunguzi zaidi juu ya risasi walizonazo mwilini kuona kama kuna uwezekano wa kuzitoa.

Hata hivyo, bado hazijapatikana taarifa sahihi za waliojeruhiwa katika tukio hilo la Jumatano kufuatia kuwepo kwa majeruhi wengine wanaotibiwa katika hospitali binafsi za Seliani na AICC ambapo miongoni mwao ni askari polisi.
 
Back
Top Bottom