PISTO LERO
JF-Expert Member
- Mar 8, 2011
- 2,819
- 1,455
HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, MHE. JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA, AKIWASILISHA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA, MACHI 2014 ________________ UTANGULIZI Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, 1. Kwa mujibu wa kifungu 20 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 na Tangazo la Serikali Na. 30 la tarehe 14 Februari, 2014, naomba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba. Rasimu ya Katiba ninayoiwasilisha imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kukamilisha kazi ya kuratibu, kukusanya, kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. Mwanzo kabisa, nieleze kwamba, Maelezo haya ninayoyatoa, ni sehemu ya Randama (Memorandum) iliyoandaliwa na Tume kwa lengo la kufafanua kwa kina, maudhui ya kila Ibara iliyomo katika Rasimu ya Katiba na sababu za mapendekezo ya Ibara hizo. Hivyo, naomba maelezo yote yaliyomo katika Randama yawe sehemu ya maelezo yangu na yaingizwe katika kumbukumbu za Bunge hili. Rasimu ya Katiba ni miongoni mwa Nyaraka zilizoambatanishwa katika Ripoti ya Tume kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyowakabidhi Waheshimiwa Marais tarehe 30 Desemba, 2013. Nyaraka nyingine ni: 2. 3. 1 (a) Taarifa ya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba. Taarifa hii ina maoni ya Wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya kikatiba ambayo ndio msingi wa uandishi wa Rasimu ya Katiba; (b)Taarifa ya Mabaraza ya Katiba ambayo inaainisha maoni ya Wananchi kuhusu Ibara zilizokuwemo katika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba na jinsi zilivyofanyiwa kazi; (c) Taarifa ya maoni ya Wananchi kuhusu Sera, Sheria na Utekelezaji. Taarifa hii ina maoni ya wananchi kuhusu mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa uamuzi wa kisera, kutunga au kurekebisha sheria zilizopo au utekelezaji wa kiutendaji; (d)Taarifa ya Utafiti Kuhusu Masuala Mbalimbali ya Kikatiba, ambayo ina taarifa nne ambazo ni: (i) (ii) (iii) (iv) Utafiti Kuhusu Madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Utafiti Kuhusu Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji; Utafiti Kuhusu Masuala Yanayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar; na Ushauri Elekezi Kuhusu Mifumo ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, Tanzania (Final Report on the Review of Various Aspects of Electoral Systems and the Electoral Commission in Tanzania). (e) Taarifa ya maeneo makuu yaliyotolewa maoni, jinsi, elimu na kazi za watoaji maoni; na Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi ambayo inaainisha (f) Viambatisho vya Ripoti ambavyo vinaainisha hatua mbalimbali za mchakato, uamuzi, hotuba za viongozi na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Tume. 4. Ripoti ya Tume na baadhi ya Taarifa zimegawiwa kwa kila Mjumbe na Taarifa nyingine zimewekwa katika Maktaba ya Bunge ili kuwawezesha Wajumbe kufanya marejeo. Tume inaamini kwamba Ripoti na Taarifa zinazowasilishwa pamoja na maelezo haya zitawasaidia Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kujadili na kufanya uamuzi sahihi kwa kila Ibara iliyopendekezwa kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na Taifa kwa jumla. 2 Shukrani kwa Uteuzi na Kuchaguliwa Mheshimiwa Mwenyekiti,
5. Naomba kutumia fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha Tume kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba na kuiwasilisha katika Bunge lako. 6. Mwenyezi Mungu alitulinda katika mchakato mzima wa kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi hadi kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu. Kwa huzuni kubwa tulimpoteza mmoja wetu, Dkt. Adrian Sengondo Mvungi katika hatua za mwisho za kazi yetu. Mchango wa Dkt. Mvungi ulikuwa mkubwa sana na ingawa hatuko naye, Rasimu ya Katiba ninayoiwasilisha imesheheni maoni yake mengi. Kazi ya Mungu haina makosa na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 7. Napenda kukupongeza wewe mwenyewe na Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu ili kuongoza Bunge hili ambalo lina jukumu kubwa la kujadili na kupitisha masharti ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Bunge hili Maalum la Katiba litapendekeza Katiba Mpya itakayopigiwa kura ya maoni na wananchi. Kuchaguliwa kwenu ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wajumbe wa Bunge Maalum juu yenu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awawezeshe kuifanya kazi hiyo kwa weledi, hekima, busara, uzalendo na uadilifu mkubwa ili kukamilisha jukumu la Bunge Maalum la Katiba. Tunawapongeza pia wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba na tunawatakia kila la kheri katika kutimiza jukumu ambalo taifa limewakabidhi. 3 Shukrani kwa Marais, Watendaji Mheshimiwa Mwenyekiti,
8. Kwa niaba ya Wajumbe, na Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa niaba yangu mwenyewe, ninawashukuru kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, kwa mambo yafuatayo:
Kwanza, kwa uamuzi wao wa busara wa kusikiliza matakwa ya Wananchi ya kutaka Katiba Mpya. Pili, kwa kututeua kuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutuwezesha kuifanya na kuikamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba kwa wakati uliowekwa kisheria. Tatu, kwa kuipatia Tume, Watumishi wa Sekretarieti walio makini, wenye ujuzi, utaalamu na uelewa katika fani zao walioiwezesha Tume kukamilisha kazi yake kwa ufanisi. Nne kuheshimu, kuisimamia na kuipa Tume nyenzo za kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na bila ya kuiingilia. Mwisho kwa mujibu wa sheria, kuunda Bunge Maalum la Katiba lililojaa wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali ya jamii za watanzania.
9. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Mawaziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Serikali; Makatibu Wakuu Viongozi, Watendaji Wakuu wa Wizara za Katiba na Sheria; Wakuu wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Wakurugenzi na Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Watendaji wa Tarafa, Kata, Shehia,
4 Vijiji na Mitaa kwa ushirikiano mzuri waliotoa kwa Tume wakati wote wa mchakato wa kupata maoni ya wananchi. 10.Tume pia inatoa shukrani maalum kwa Jeshi la Polisi la Tanzania na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kuhakikisha mchakato mzima unaenda kwa usalama. Aidha, Tume inatoa shukrani kwa Vyama vya Siasa, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia, Vyombo vya Habari, Taasisi na Makundi mengine kwa mchango wao mkubwa wakati wote wa mchakato wa kupata maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. Shukrani kwa Wananchi Mheshimiwa Mwenyekiti, 11.Kwa namna na kwa uzito wa pekee, Tume inawashukuru sana Wananchi wote kwa ushiriki, na kwa mchango wao mkubwa wa mawazo, maoni na mapendekezo yaliyowezesha kupatikana kwa Rasimu ya Katiba. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kwa wananchi wa kawaida kushiriki katika kutoa maoni kwa uhuru na uwazi kuhusu aina ya katiba wanayoitaka, na wamefanya hivyo kwa wingi, uhuru, uwazi, umakini na kwa uzito unaostahili. Mheshimiwa Mwenyekiti; 12.Baada ya kutoa shukrani sasa naomba nitoe maelezo marefu kidogo kuhusu Rasimu ya Katiba. Maeneo yote ya Rasimu ni muhimu lakini kwanza nitayazungumzia machache kwa ujumla kutokana na umuhimu wake. Baadaye nitaizungumzia Rasimu ya Katiba kwa kupitia maudhui ya kila Sura. Maelezo kwa kina ya kila Ibara na sababu za mapendekezo zinaelezwa kwenye Randama 5 ambayo tayari imekabidhiwa kwa Katibu wa Bunge Maalum la Katiba na wabunge wote watapata nakala. Dhana ya Katiba Mheshimiwa Mwenyekiti, 13.Katika nchi yoyote, msingi wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba. Katiba ni sheria kuu au sheria mama katika nchi yoyote. Sheria nyingine zote zinategemea au zinatungwa kwa mujibu wa Katiba. Wakati mwingine Katiba hutafsiriwa kuwa ni mkataba wa Kijamii kati ya Viongozi na Wananchi. Ni makubaliano ya wananchi kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao. Katiba ni muafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi. 14.Katiba ni Sheria ya msingi ambayo inaweka mfumo wa uendeshaji wa nchi. Katiba inafanya hivyo kwa kuainisha misingi ya taifa, mgawanyo wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola. Mheshimiwa Mwenyekiti, 15.Katika nchi ambazo zimefanya mabadiliko ya katiba, njia kuu zifuatazo huwa zinatumika: (i) (ii) (iii) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya kikatiba; Kuundwa Tume ya kuandaa Katiba kwa kupitia sheria zilizopo; na Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya Katiba. 6 16.Nchi yetu imetumia utaratibu wa Bunge kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayoelezea utaratibu wa mchakato mzima wa kupata katiba mpya ambao unawashirikisha wananchi kisheria katika hatua zote muhimu za uandikaji wa katiba yao. 17.Sheria imeanzisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ikaweka Hadidu za Rejea na kuipa Tume jukumu la kuratibu, kukusanya maoni ya wananchi, kuchambua na kutathmini maoni na kuandaa Ripoti na Rasimu ya Katiba. Baadaye wananchi, kupitia Mabaraza ya Katiba, walipewa fursa tena ya kutoa maoni yao kabla ya Tume kufanya maboresho na kuiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba; hatua ambayo ndipo tulipofikia hivi sasa. 18.Baada ya Bunge Maalum kutoa Katiba inayopendekezwa, wananchi watapata fursa ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba Mpya kupitia kura ya maoni. Si nia yangu kutoa maelezo kuhusu historia ya katiba nchini, kwa kuonyesha tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi. Maelezo ya kina kuhusu suala hilo yamo kwenye Sura ya Tatu ya Ripoti ya Tume kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utangulizi wa Rasimu ya Katiba 19.Rasimu ya Katiba inaanza na utangulizi. Utangulizi ni sehemu muhimu ya Katiba ya nchi. Katika hali ya sasa ya mwelekeo wa taaluma ya sheria duniani, na kwa mujibu wa Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 ya Sheria za Tanzania, Utangulizi ni sehemu ya Katiba. Utangulizi ndio kioo kinachoonyesha dhamira ya Katiba kwa kutoa tafsiri ya jumla ya Katiba. Sehemu hii inatoa taswira na picha halisi ya 7 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake, historia yao, matarajio yao, misingi na masuala muhimu ambayo wanataka kuyaendeleza katika jamii, kizazi hadi kizazi. 20.Utangulizi wa Rasimu ya Katiba unatamka rasmi kwamba Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetungwa na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuthibitishwa na wananchi kupitia kura ya maoni. Eneo la Jamhuri 21.Tume imependekeza eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lijumuishe eneo lote la iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari, kama ilivyoainishwa katika Katiba za Uhuru za nchi mbili hizi. 22.Madhumuni ya kubainisha eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kukubaliana na maoni ya wananchi waliotaka kuwepo kwa ufafanuzi thabiti kuhusu eneo na mipaka ya nchi. Kufanya hivi, kutatunza historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuondoa utata na hisia kwamba mipaka ya nchi hizi mbili inabadilika. 23.Lengo pia la sehemu hii ni kuainisha mipaka ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotambulika na mikataba mbalimbali ya kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Bahari wa mwaka 1982. 8 Misingi Mikuu ya Taifa 24.Rasimu ya Katiba, kama ilivyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeorodhesha misingi mikuu ya Taifa inayojenga Taifa la Tanzania na kusimamia ustawi wa wananchi wake. Katiba ya sasa ina misingi mikuu minne, yaani, uhuru, haki, udugu na amani. Wananchi walipendekeza misingi mingine minne iongezwe, yaani utu, usawa, umoja na mshikamano. Kwa hiyo, misingi inayopendekezwa ni Utu, Uhuru, Haki, Udugu, Amani, Usawa, Umoja na Mshikamano. Tunu za Taifa 25.Tunu za Taifa ni mambo muhimu ya kujivunia kwa jamii yoyote ile. Tunu ndio msingi wa maadili na utamaduni wa jamii. Tume inapendekeza tunu zifuatazo zitajwe ndani ya Katiba: Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa. 26.Madhumuni ya kupendekeza Tunu hizi kuingizwa katika Katiba ni kuheshimu na kuzingatia maoni na mapendekezo ya wananchi kuwa Katiba itaje Tunu za Taifa ili kuifanya jamii kuzitambua, kuzithamini na kuzitekeleza. Malengo Muhimu 27.Sura ya Pili ya Rasimu inaelezea Malengo Muhimu na Misingi ya Shughuli za Serikali na Sera za Kitaifa. Wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi, hasa wale wanaoishi vijijini, walizungumzia sana dira ya taifa kuhusu maendeleo yao. 9 28.Moja ya mambo ambayo wananchi waliyatolea maoni kwa msisitizo mkubwa ni ardhi. Wananchi wengi walilalamika kwamba wanayo matatizo kutokana na ugumu wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine lakini wawekezaji wakubwa wanapewa upendeleo wa kupata ardhi kwa urahisi. Pia, kuna migongano isiyokwisha ya makundi mbalimbali, wakulima na wafugaji, wananchi na mamlaka za hifadhi za taifa na kadhalika. Kuna malalamiko mengi kuhusu huduma za kilimo kama vile zana za kilimo, pembejeo na mizania ya bei. 29.Mkulima mmoja wa pamba, wilaya ya Kahama, alilalamika kwamba ingawa wanaambiwa na Serikali kwamba watajiondoa kwenye lindi la umaskini kupitia kilimo bora, lakini haoni dalili hizo. Alisema wakulima wana matatizo ya mbegu, dawa za kuuwa wadudu na bei ndogo ya mazao. Alisema mwaka 2012 alikuwa ametumia shilingi mia nane kupata kilo moja ya pamba, lakini bei aliyopewa ilikuwa shilingi mia sita. Katika mazingira haya, badala ya kupata maisha bora, anazidi kuwa maskini. 30.Wakulima wa mazao ya chakula wana matatizo ya aina hiyo, na hivyo hivyo kwa wakulima wa mazao ya biashara. Wafugaji nao wana matatizo ya ardhi ya malisho, maji, madawa ya mifugo na bei ya mifugo yao. Wavuvi wana matatizo ya maeneo ya uvuvi, zana za uvuvi bei na kadhalika. 31.Wananchi pia walizumgumzia hifadhi ya jamii, hasa kwa wazee. Wanasema wafanyakazi wana mifumo ya hifadhi ya jamii na mishahara yao inaongezwa kila wakati. Kwa Wakulima, mapato yao ni madogo na wakizeeka hawana hifadhi yoyote. Hata matibabu ya wazee siyo bure kama utaratibu wa Serikali 10 unavyoelekeza, kwani sharti wanunue dawa wakati uwezo wao wa kifedha ni mdogo. 32.Wananchi pia walizungumzia elimu na huduma za afya. Kwa maoni yao, elimu bora na huduma za afya bora zinatolewa kwa watu wa tabaka la juu. Wao wanabaki na shule zenye huduma hafifu na zahanati zenye kutoa huduma hafifu. 33.Tume imezingatia maoni ya wananchi na imependekeza mambo kadhaa. Kubwa ni kuweka dira ya taifa. Sura ya Pili yote ya Rasimu ya Katiba inazungumzia dira ya taifa. Madhumuni ya kuweka Malengo Muhimu na Misingi ya Shughuli za Serikali ni kuhakikisha kuwa Serikali na mamlaka zake zinapewa mwongozo wa kisera na mwelekeo wa kiutendaji. Pamoja na mambo mengine malengo yafuatayo yamewekwa kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi:
(i) Kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi; (ii) Kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao; (iii) Kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya mazao yao; (iv) Kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa mizania ya bei za mazao na pembejeo.
34.Haki ya kumiliki mali imejumuishwa kwenye haki za binadamu, na vivyo hivyo, haki ya elimu bora ya msingi ipatikanayo bila malipo. 11 Maadili 35.Wananchi walio wengi walionyesha kufadhaishwa sana na kuporomoka kwa maadili ndani ya jamii na ndani ya Uongozi wa Umma kwa kiwango kikubwa. Aidha, wananchi walitoa maoni yao kuwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi iliyopo haina mamlaka ya kutosha ya kuchukua hatua zinazostahiki kwa viongozi wanaovunja na kukiuka maadili ya uongozi. 36.Katika kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu maadili ya viongozi wa umma na uwajibikaji, Tume ilifanya utafiti kuhusu dhana ya uwajibikaji. Aidha, Maoni ya Mabaraza ya Katiba yamesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa Maadili na miiko ya Viongozi wa Umma ndani ya Katiba. 37.Kwa kuzingatia maoni ya wananchi na Taarifa ya utafiti, Tume inapendekeza Maadili ya Viongozi wa Umma na Miiko ya Uongozi yawekwe katika Katiba. Aidha, inapendekezwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi ibadilishwe kuwa Tume kamili ya kikatiba yenye mamlaka na uwezo mkubwa wa kusimamia maadili ya viongozi. Haki za Binadamu 38.Kwa kiwango kikubwa Haki za Binadamu zilizoainishwa kwenye Rasimu ya Katiba zinafanana sana na namna zilivyo kwenye katiba ya sasa. Kwa kuzingatia maoni ya wananchi ya kutaka kuimarishwa kwa Haki za Binadamu, Tume inapendekeza kuimarishwa kwa Haki hizo kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima. Kwa mfano, kuimarisha ushiriki wa wananchi kwenye uongozi kwa kuruhusu mgombea huru kikatiba. 12 39.Tume kwa kuzingatia maoni ya wananchi na mikataba ya kimataifa inapendekeza kuongezwa kwa haki mpya kwa kuzingatia maadili ya watanzania. Miongoni mwa haki hizo ni Haki za Wafanyakazi, Haki ya Mtoto, Haki za Watu wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Vijana, Haki za Kupata Habari, Haki na Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari. Baadhi ya haki hizi zimo kwenye sheria mahususi za nchi. Hata hivyo, Tume imeona ni vyema zikawekwa kwenye katiba ili kuweka msingi wa wananchi kuweza kuhoji na kudai utekelezaji wake kikatiba. 40.Pamoja na haki hizo, haki ya kumiliki mali, ilitolewa maoni na wananchi kwa msisitizo wa kipekee. Maoni ya wananchi wengi yanahusu upungufu katika utekelezaji na usimamizi wa sheria za ardhi kuhusu umiliki, uchukuaji wa maeneo ya ardhi yao na ulipaji wa fidia stahiki. Aidha, wananchi walilalamika kuwa Serikali imekuwa ikichukua mali zao bila fidia stahiki. Hivyo, Tume inapendekeza kuwa mtu yeyote ana haki ya kumiliki na kupata hifadhi ya mali ambayo ameipata kwa njia ya halali na kwamba, asinyanganywe mali hiyo kwa madhumuni yoyote, bila ya kupata malipo stahiki yanayolingana na thamani halisi ya mali hiyo kwa wakati. Uraia 41.Rasimu imetamka Uraia kuwa ni mmoja ambao ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Moja ya masuala makuu ya kidola (sovereign functions) ni uraia. Suala la uraia limeorodheshwa kuwa ni miongoni mwa Mambo ya Muungano. 42.Uraia ni msingi wa utambulisho (identity) unaompa raia haki ya kulindwa na nchi yake, ikiwa ni pamoja na haki zake za binadamu za asili na zisizoondosheka (inherrent and inalienable rights) kama zilivyotambuliwa au zitakavyotambuliwa 13 katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba za Nchi Washirika na Mikataba ya Kimataifa. 43.Uraia kama ulivyowekwa katika Rasimu ya Katiba, umejengwa katika msingi wa uzalendo usiotiliwa shaka (patriotism) unaompatia raia wajibu wa kuitetea, kuilinda na kuifia nchi yake bila ya mashaka. Kwa hiyo, Uraia ndiyo kigezo na sifa ya kupewa dhamana ya uongozi wa Taifa na kuajiriwa katika mihimili ya Serikali na vyombo vya Ulinzi na Usalama. Rasimu inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na uraia wa kujiandikisha ambao, katika kujidhihirisha kwake, ni uraia wa nchi moja usiojenga au kuleta hisia za kuwabagua au kuwatenga raia katika matabaka na madaraja yanayotokana na tofauti ya hali au fursa zao. 44.Rasimu ya Katiba pia inapendekeza kuwapatia hadhi mahsusi watu wenye asili au nasaba ya Utanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kuchukua Uraia wa nchi nyingine. 45.Lengo ni kuwarahisishia watu wenye asili ya Tanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine wakija hapa nyumbani wasipate usumbufu usio wa lazima na pia ili warahisishiwe ushiriki wao katika ujenzi wa taifa kwa kuwawezesha kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Utaratibu kama huu unafuatwa katika nchi kadhaa, kwa mfano Ethiopia, India na Ujerumani ambako umeonyesha mafanikio. 14 Mihimili ya Serikali Mheshimiwa Mwenyekiti; 46.Sura ya Saba hadi Sura ya Kumi zinahusu Mihimili ya Serikali. Katika sehemu hii kuna mapendekezo ambayo yataleta mabadiliko makubwa. 47.Tukianza na taasisi ya Urais, kuna mapendekezo manne makubwa. Pendekezo la kwanza ni kumuondoa Rais kutoka kwenye Bunge. Hali ilivyo sasa, Rais ni sehemu ya Bunge na Mawaziri wake ni Wabunge. Nia ya pendekezo hili ni kutenganisha mamlaka na madaraka ya mihimili (separation of powers). Kazi kubwa ya Bunge ni kuisimamia Serikali. Bunge haliwezi kuisimamia Serikali kwa uhuru kama Serikali nayo ni sehemu ya Bunge. Kwa kifupi, lengo la pendekezo hili ni kuongeza mamlaka na madaraka ya Bunge. 48.Katika pendekezo la pili, mtu atakuwa amechaguliwa kuwa Rais kama atapata kura za wapiga kura zaidi ya nusu (absolute majority), badala ya utaratibu wa sasa wa kupata wingi wa kura (simple majority). Msingi wa pendekezo hili ni kwamba, Rais si kiongozi wa Serikali tu bali pia ni Mkuu wa Nchi na Amri Jeshi Mkuu. Kwa sababu hiyo, Rais ndiye alama na taswira ya nchi na watu wake, na Rais ndiye alama ya umoja na uhuru wa nchi na mamlaka ya nchi. Kwa maana hiyo, ni muhimu Rais kuonekana anakubalika kwa wananchi walio wengi. 49.Pendekezo la tatu ni kuruhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa Mahakamani. Kwa hali ya sasa, matokeo ya uchaguzi wa Rais yakishatangazwa na Tume ya Uchaguzi, hakuna ruhusa ya kuyahoji matokeo hayo. 15 50.Katika uchaguzi wa Rais, inawezekana kutakuwa na sababu za msingi kuamini kwamba uchaguzi huo haukuwa halali. Ni jambo la msingi kuhakikisha kwamba Rais amechaguliwa kihalali. Hata hivyo, tahadhari imewekwa ili kuhakikisha kwamba ruhusa hii isitumiwe vibaya. Kwanza, mtu anayeweza kuhoji ni yule tu aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais. Sharti hili litazuia watu kutumia vibaya ruhusa ya kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais. Pili, ni Mahakama ya Juu tu ndiyo yenye madaraka ya kusikiliza shauri la aina hii na ni lazima uamuzi juu ya shauri hilo utolewe ndani ya muda wa mwezi mmoja. Wenzetu wa Kenya na mataifa mengine duniani wanao utaratibu kama huu. 51.Pendekezo la nne linahusu madaraka ya Rais. Suala la madaraka ya Rais limezungumziwa kwa uzito sana katika kipindi hiki. Wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, suala la madaraka ya Rais lilijitokeza sana. Wakati wa kukusanya maoni wananchi nao walilitolea maoni mengi. 52.Baada ya uchambuzi na tathmini ya maoni yote na Taarifa ya Utafiti, Tume imependekeza kwamba Rais abaki na madaraka ya msingi kama Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali. Madaraka hayo yameainishwa katika Ibara ya 72 ya Rasimu. Hata hivyo, madaraka ya Rais akiwa Mkuu wa Serikali na hasa kwa upande wa uteuzi wa viongozi, ama yamepunguzwa au yamewekewa utaratibu. Rais amepunguziwa madaraka ya kuteua watumishi wa umma wa ngazi za kati na ngazi za chini. Watumishi hao uteuzi wao utakuwa kwenye madaraka ya Tume za Utumishi. 16 53.Rais, atabaki na madaraka ya kuwateua viongozi wa kitaifa, kama vile Mawaziri, Majaji, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wenyeviti na Wajumbe wa Tume za kitaifa. Pamoja na kubaki na madaraka hayo, Rais amewekewa utaratibu wa uteuzi. Baadhi ya viongozi watateuliwa moja kwa moja na Rais na baadaye watathibitishwa na Bunge, kwa mfano, Mawaziri. Wengine watapendekezwa na Kamati ya Uteuzi na baada ya kuteuliwa, watathibitishwa na Bunge, kwa mfano, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama watateuliwa na Rais kwa kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa. Wengine watateuliwa kutokana na ushauri wa Tume za Utumishi, kama vile Majaji na Makatibu Wakuu. Bunge Mheshimiwa Mwenyekiti; 54.Kwa Bunge la Muungano, madaraka yake na mamlaka yatabaki kusimamia mambo ya Muungano. Kinachobadilika sasa ni Bunge kutokuwa na mamlaka juu ya mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika kama ambavyo imekuwa kwa upande wa Zanzibar. Hata hivyo, Bunge la Muungano litapata taarifa ya uratibu na utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali. 55.Imependekezwa pia kwamba Spika na Naibu Spika wasitokane na Mawaziri, Naibu Mawaziri au Wabunge. Lengo la pendekezo hili ni kupata viongozi ambao wataonekana hawaegemei upande wowote. Imependekezwa pia kwamba Wabunge wasiwe Mawaziri. Pendekezo hili limetokana na maoni ya wananchi 17 kwamba wanahitaji Wabunge kuwa karibu na wapiga kura wao. Wengine wanaamini kwamba wabunge ambao ni Mawaziri wanapendelea majimbo yao ya uchaguzi badala ya kutumikia taifa kwa ujumla kwa usawa. 56.Lakini lengo jingine la pendekezo hili, ni kutenganisha madaraka ya mihimili. Kama Bunge likiwa na madaraka ya kuthibitisha Mawaziri itakuwa vigumu kwa Wabunge kuwakataa Wabunge wenzao watakaoteuliwa kuwa Mawaziri, kisha kuendelea kukaa pamoja kwa utulivu ndani ya Bunge. 57.Tume imependekeza ukomo wa ubunge kuwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa Mbunge wao kabla ya kumaliza muda wa kipindi chake cha miaka mitano. Pendekezo hili linatokana na maoni ya wananchi waliotaka kuwepo ukomo wa ubunge ili kuondoa dhana ya umiliki wa jimbo la uchaguzi, kutoa fursa kwa wananchi wengine wenye uwezo kugombea nafasi ya ubunge, kuongeza uwajibikaji wa wabunge katika majimbo ya uchaguzi na kuongeza mamlaka ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao. 58.Pia, ni maoni ya wananchi kuwa kusiwepo uchaguzi mdogo ili kupunguza gharama. Endapo nafasi ya ubunge itaachwa wazi kutokana na mbunge wa chama cha siasa kupoteza Ubunge, basi Tume Huru ya Uchaguzi itajaza nafasi hiyo kutokana na orodha ya majina yaliyowasilishwa na chama cha siasa husika na kwa kushirikiana na chama hicho. Uchaguzi mdogo utafanyika tu pale ambapo nafasi ya ubunge iliyo wazi imetokana na mbunge huru. 18 Mahakama 59.Kuhusu Mahakama, pendekezo kubwa ni kuundwa kwa Mahakama ya Juu na kwamba Mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani ndizo ziwe Mahakama za Muungano. Mahakama Kuu ziendelee kutokuwa za Muungano kama ilivyo sasa. Hata hivyo, inapendekezwa kuwa Mahakama Kuu ya Tanganyika na Mahakama Kuu ya Zanzibar ziwe na mamlaka sawa katika kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano (concurrent jurisdiction). Hivi ndivyo ilivyo hivi sasa kwa upande mmoja, ambapo Mahakama Kuu ya Zanzibar, japokuwa si sehemu ya Mahakama za Jamhuri ya Muungano, lakini imepewa mamlaka na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kusikiliza na kuamua kuhusu mashauri ya kesi za madai na jinai yanayohusu sheria za muungano. Pendekezo jingine ni kuuweka Mfuko wa Mahakama ndani ya Katiba. Vyombo vya Kikatiba Mheshimiwa Mwenyekiti, 60.Masuala mengine ambayo yameainishwa na kuwekewa masharti ya Kikatiba ni Utumishi wa Umma katika Jamhuri ya Muungano, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji na Tume ya Haki za Binadamu. Tume ya Utumishi wa Umma 61.Rasimu ya Katiba inaweka utumishi wa umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya Katiba. Sura ya Kumi na Moja inaainisha misingi na kanuni kwamba utumishi wa umma ni dhamana kutoka kwa wananchi na hivyo, mtumishi anatakiwa kutumikia wananchi kwa uadilifu na uaminifu. Misingi mingine ni kudumisha na kukuza viwango vya juu vya maadili ya kitaaluma, na kuhakikisha 19 kwamba uteuzi na uajiri katika nafasi mbalimbali unazingatia uwezo wa kitaaluma, uweledi, maarifa, ujuzi, umakini na uzoefu katika eneo husika. Msingi mwingine ni kutoa huduma kwa umma kwa njia ya haki, usawa na bila upendeleo. Misingi hii itatumika katika mihimili yote ya dola, taasisi na idara zote za Serikali, mashirika, makampuni na wakala wa Serikali. 62.Ili kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa utumishi wa umma, Rasimu ya Katiba inaanzisha Tume ya Utumishi ya Umma wa Jamhuri ya Muungano ambayo itaongozwa na Mwenyekiti na wajumbe wengine sita watakaoteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge. Tume ya Utumishi wa Umma itakuwa ni chombo cha juu katika Utumishi wa Umma chenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu mambo yote ya utumishi wa umma. 63.Ibara ya 188 inaainisha majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ni pamoja na kumshauri Rais juu ya uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma, kutoa miongozo mbalimbali ya kusimamia mchakato wa ajira katika utumishi wa umma na kuhamasisha utekelezaji wa misingi na kanuni za utumishi katika Sekta zote za Utumishi wa Umma. Tume pia itakuwa na mamlaka ya kuunda na kupanga mishahara na marupurupu ya watumishi wote, wakiwemo viongozi wa kisiasa. Tume Huru ya Uchaguzi Mheshimiwa Mwenyekiti, 64.Rasimu ya Katiba, kama ilivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, imetambua haki ya kupiga kura kuwa ni haki ya msingi ya raia ambayo ni lazima 20 itambuliwe na kulindwa na Katiba. Kwa umuhimu huo, inapendekezwa kuwepo kwa mfumo wa wazi wa utaratibu wa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi na kura ya maoni. 65.Ili kusimamia taratibu za uchaguzi, Rasimu ya Katiba inapendekeza Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano. Tume ndiyo itakayosimamia masuala ya uchaguzi na kura za maoni. Yapo masharti kuhusu upatikanaji wa wajumbe kwa uwazi kupitia utaratibu wa kuomba nafasi na kuchujwa na Kamati ya Uteuzi kabla ya kuteuliwa rasmi na Rais. 66.Rasimu ya Katiba inaanzisha Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi. Wajumbe hao ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mwenyekiti, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Spika wa Bunge la Tanganyika, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Jaji Mkuu wa Tanganyika, Jaji Mkuu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili