Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,806
- 31,823
Said Abeid
Mjukuu wa Mohamed Abeid
Said Abeid nini uzawa wangu tumekutana miezi michache iliyopita Msikiti wa Maamur wakati wa Asr mimi nilikuwa napita njia na sala ikanikuta nikiwa maeneo hayo kwa hiyo nikaingia hapo kusali.
Wakati natoka kuna mtu akanisalimia ambae baadae akajitambuliha kwa jina la Said Abeid na kwa kumtazama usoni nikaona ile bashasha nami nikarejesha na hapo akanifahamisha kuwa tuko pamoja katika Saigon Group katika Whatsapp.
Kwa hakika mimi sikuwa namfahamu ingawa katika moja ya nyakati tunepishana katika Saigon
Club lakini akanambia yeye ni mtoto wa Dar es Salaam Karikaoo, Mchikichini kuelekea Msimbazi na Jangwani huko ndiko ilipokuwa hodhi ya babu yake, Mohamed Abeid Muarabu mwenye asili ya Yemen.
Akanambia babu yake alikuwa na shamba kubwa Mchikichini.
Leo mtu ukimweleza habari ya mashamba Mchikichini lazima atashangaa kwani sisi tunazaliwa Mchikichini tumekuta majumba watu wakiishi hakuna hata bustani. Ndipo alipomtaja babu yake Mohamed Abeid na shamba lao lililokuwa maarufu watu wakiita apokuwa akiishi babu yake, ‘’Shama kwa Mohamed Abeid.’’
Hapo hapo nikajua kuwa nimepata mgodi wa dhahabu kwangu mimi kazi ni kuanza kuchimba madini. Katika, ‘’paper,’’ yake ‘’The Dockworkers of Dar es Salaam,’’ John Iliffe alilitaja Shamba la Mohamed Abeid na nini kilifanyika pale wakati wananchi wanapambana na ukoloni wa Mwingereza.
Nilimuuliza Said Abeid kama ana picha ya babu yake, Mohamed Abeid. Alinambia anayo na akaahidi kunipatia. Baada ya mazungumzo kidogo akanifahamisha kuwa yeye yuko hapo msikitini wamefiwa wanasubiri kwenda kuzika Makaburi ya Kisutu. Nilimpa pole kisha tukaagana.
Hiki hapo chini ndicho kisa cha Shamba kwa Mohamed Abeid:
Waliosimama nyuma wa kwanza mwenye koti jeusi ni Mohamed Abeid na katika mstari wa katikati wa pili kulia huyo mtoto aliyeshikwa ni Abeid Mohamed baba yake Said Abeid hii picha ilipigwa miaka ya 1920
'…shida zilipozidi kumuelemea Mwafrika kutokana na sheria za kazi zilizojaa dhulma na kwa kupewa mishahara midogo, watu walikigeukia chama cha African Association ili kupata msaada na uongozi.
Hali hii ndiyo iliyomsukuma Abdulwahid katika siasa na ikamfanya aelewe maana ya harakati za wananchi dhidi ya utawala wa kigeni akiwa bado kijana mdogo sana. Kidogo kidogo Kleist alianza kumkabidhi Abdulwahid kazi za African Association na mara akawa msaidizi wa baba yake katika siasa za Dar es Salaam.
Ilikuwa katika kutimiza haya ndipo Abdulwahid akajikuta anahusika na ule mgogoro wa makuli ulioibuka bandarini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukichemka pole pole chini kwa chini kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa vita. Hatimaye, Abdulwahid alihusika na harakati za siri za wafanyakazi bandarini ambao, wakiwa wamechoshwa na sheria za kazi za ukandamizaji na wakiwa wamechoka kunyonywa na makampuni ya meli, walikuwa wanapanga kuitisha mgomo.
Chama cha African Association ndicho kiliwakilisha maslahi ya wananchi wa Tanganyika na kimya kimya kiliunga mkono zile harakati za chini kwa chini za wafanyakazi katika kutafuta haki zao. Abdulwahid, kijana mdogo mwenye elimu na akiwa karibu zaidi na uongozi wa African Association kuliko Mwafrika yoyote pale mjini, alichaguliwa kuongoza harakati za tabaka la wafanyakazi zilizokuwa zinaibuka. Haya ndiyo mambo serikali ya kikoloni ilihofia na ndiyo ilikuwa sababu ya kumfanyia khiyana asiingie Makerere. Utawala wa kikoloni ulifahamu kuwa msukumo wa Kleist na mwanae aliyeelimika ungeipa Tanganyika uongozi uliokuwa unakosekana Tanganyika na pengine hata ndani ya Al Jamitul Islamiyya.
Ili kuifanya serikali iwasikilize mahali ambapo hapakuwa na sheria za kazi, ilibidi iwekwe mikakati ambayo ingeifanya serikali iweke sheria hizo katika vitabu vyake. Kamati ndogo ya siri iliundwa na Abdulwahid akatiwa ndani ya kamati hiyo ili kuongoza mgomo uliokusudiwa. Kazi ya kamati hiyo ilikuwa kupanga na kuratibu mikakati ya kuitisha mgomo ambao ungelisaidia katika kuondoa ile dhulma iliyokuwepo. Makuli waliitisha mkutano pembeni kidogo mwa mji, mahali palipokuwa pakijulikana kama ‘’Shamba kwa Mohamed Abeid,’’ katika bonde la Msimbazi.
Sehemu hii ilichaguliwa makhususi mbali na macho ya watu ili ipatikane faragha. Makuli walikula kiapo na kusoma, ‘’Ahilil Badr,’’ ili kujikinga na unafiki, usaliti pamoja na shari ya vizabizabina wangeokataa kugoma. Ubani ulifukizwa na Qur’an ilisomwa.
Wakijikinga na kiapo hicho cha mashahidi wa vita vya Badr na huku wakichochewa na ushujaa wa mashahidi waliokufa katika katika vita vya Badr wakipigana na washirikina wa Makka wakiwa pamoja na Mtume Muhammad (Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu Yake), makuli walichagua tarehe 6 Septemba, 1947 kuwa ndiyo siku ya kuanza mgomo wao.
Mapema asubuhi moja kile kilichoanza kama mipango ya siri dhidi ya makampuni ya wazungu bandarini, kililipuka na kuwa mapambano ya dhahiri. Watu katika mitaa jirani ya alipoishi akikaa Abdulwahid walikuwa hawajatoka vitandani mwao alifanjiri moja waliposikia vishindo na makelele vimetanda mtaani.
Makuli, baadhi yao wakiwa vidari wazi, walikuwa wameizingira nyumba ya Kleist, wakipiga makelele wakimtaka Abdulwahid atoke nje. Makuli wale walipiga kwata njia nzima kutoka bandarini huku wakitoa maneno ya kupinga ukoloni na wakiimba kupandisha morali zao. Tukio hili halikuwa na kifani. Ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Tanganyika kwa wananchi kushuhudia katika mitaa ya Dar es Salaam uasi wa dhahiri kama huo dhidi ya serikali ya kikoloni.
Abdulwahid, wakati ule kijana mdogo kabisa, akichungulia kupitia dirisha la chumba chake alichokuwa amelala, alishangazwa kuona umati mkubwa wa watu nje ya nyumba yao. Aliweza kuwatambua baadhi ya wenzake katika kamati ile ya siri iliyokuwa inapanga mipango ya mgomo. Alipotoka nje kuonana nao makuli wenye hasira walimfahamisha kuwa mgomo ulikuwa umeanza na wasingerudi kazini hadi madai yao yote yamekubaliwa...''