Hili la wafanyakazi hewa ni mmojawapo ya fedheha zetu sote

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,487
13,612
Ni tendo lenye kuambatana na fedheha kubwa kwa mkuu wa mkoa kusimama akiwa amezungukwa na wakuu wa mikoa wenzake mbele ya waziri wa TAMISEMI halafu anaanza kusema, "mkoa wangu umegundulika kuwa na wafanyakazi hewa kadhaa". Mkuu wa mkoa mwingine nae anasimama na kusema kwa sauti kubwa, "mkoa wangu umegundulika kuwa na wafanyakazi hewa kadhaa"!!.

Sio jambo la kulifurahia hata kidogo, ni kielelezo tosha cha uwepo wa maadili ya hali ya chini sana. Na sipendi kulitazama hili jambo kwa kuegemea kwenye itikadi za kisiasa. Hili ni aibu ya wote.

Ukitaka kujua ni kwa kiasi gani taifa hili limepotea kimaadili na hata katika viwango vya ustaarabu wa kawaida, ukienda uwanja wa taifa kutazama mechi kubwa za soka, utaona watu wamepanga foleni ili wakate tiketi kutoka kwenye yale madirisha ya zile hiace zinazopaki nje ya uwanja.
Lakini atatokea mpuuzi mmoja atakayejifanya anaharaka kuliko wote aliyowakuta na ataanzisha fujo kwa yule mtu aliye mbele kabisa anayesubiri ahudumiwe. Wapuuzi wengine watamuiga na kuamua kutoheshimu foleni na matokeo yake zogo la ajabu litazuka na mtu anaweza kujikuta anaibiwa simu au kuchaniwa nguo yake.

Wakati mwingine hata barabarani unakuta kwenye junction maarufu, magari yamefungana na hakuna hata moja mwenye uwezo wa kupata upenyo ili achomoke na gari yake.
Sababu haswa ni madereva wawili ambao walijiona wana haraka kuliko madereva wengine wote!.
Matokeo yake magari yaliyofungamana na kushindwa hata kusogea yatasubiri mpaka trafiki aje aanze kazi ya kuamuru nani ampishe mwingine ili msongamano usio na ulazima uweze kuondolewa.

Hivyo sipendi kuzitazama sana itikadi za kisiasa ninapoyaangalia matatizo mengi tuliyonayo. Ni suala la maadili mabovu, ambayo pengine yametokana na malezi mabovu pia.

Kama uendeshaji wetu wa magari ni ushahidi wa upoyoyo na ujuha wetu, na kama hata ukataji wa tiketi pale uwanja wa taifa ni ushahidi wa jinsi tusivyoweza kujisimamia kwenye mambo ya kawaida tu, basi ninajikuta nikiamini kuwa tatizo linalodumaza ustawi wetu ni la msingi na limejikita ndani zaidi ya hisia na kule kujitambulisha kwetu kupitia itikadi za kisiasa.
 
Back
Top Bottom