HERE WE GO! Maajabu ya Fabrizio Romano, sikio ardhini

James Hadley Chase

JF-Expert Member
Mar 25, 2020
1,549
2,613
UNATAKA nikupe maajabu mengine ya Fabrizio Romano? Hakuna maajabu sana. Simu yake inaweza kuwa na namba 2,000 za watu mbalimbali duniani. Lakini kuna namba ‘ameisevu’ kwa jina la Jorge Mendes.

Kuna namba ameisevu kwa jina la Mino Raiola. Kuna namba ameisevu kwa jina la KIA Joorbachian. Usidhani amewapachika watu fulani majina ya uongo. Ni majina ya mawakala maarufu duniani. Mawakala wakubwa na wadogo.

Hapa kuna kamchezo kanaendelea kati ya Romano na mawakala. Ni marafiki wa karibu. Bahati nzuri wote wanasaidiana. Huyu akifanya kazi yake vizuri basi anamsaidia mwenzake.

Romano anaweza kutulia katika mgahawa wa Enrico Bartloni jijini Milan. Ghafla simu yake ikalia. Jina linaonekana Jorge Mendes. Nyuma ya pazia kuna mazungumzo ambayo yanafanyika.

Jorge anamwambia Romano mteja wake, Cristiano Ronaldo anaweza kuondoka Manchester United kama atapata ofa sahihi kwingineko.

Dakika moja baadaye atamwambia Roma wameonyesha nia na wamempigia simu. Kwa nini Mendes anamwambia Romano?

Sio tu kwa sababu ya urafiki wao, lakini anajua Romano akienda kuandika Twitter, klabu nyingine zitasoma habari yake na zinaweza kuonyesha nia kwa Ronaldo.

“Ronaldo is open to quit Manchester United this summer and AS Roman have shown the interest.” Romano anakuja kwetu kutuandikia hivi.

Hii ni habari njema kwa Jorge Mendes kwa sababu anajua kuna timu zitataka kuipiga kumbo Roma kwa ajili ya kumpata mteja wake.

Hapa Romano anakuwa amemsaidia Mendes, pia Mendes anakuwa amemsaidia Romano kuipata habari ambayo wengine hawana. Na baada ya hapa unajua kinachofuata? Ghafla simu ya Mendes itaita. Kutoka wapi? Chelsea.

Wanamwambia wafahamishwe kuhusu maendeleo ya Ronaldo na uwezekano wake wa kuondoka katika dirisha.

Hapo Chelsea wanakuwa wameipata habari hii kutoka kwa Romano. Mtu wa kwanza kupewa mrejesho wa ofa ya Chelsea kutoka kwa Mendes atakuwa Romano.

“Chelsea wamepiga simu ya kuulizia kama Ronaldo anapatikana katika dirisha hili.”

Ikifika hapa, Romano anarudi kwetu tena na kutuambia “Here we go again, Chelsea are on race to sign Ronaldo if he will decide to quit Old Trafford.” Uzuri ni Romano anafanya kazi kwa uaminifu na hatuambii chanzo chake. Anaishia hapo hapo.

Hawezi kutuambia chanzo chake ni wakala wa Ronaldo. Lakini kila maendeleo ya Ronaldo na masuala ya uhamisho Romano anakuwa wa kwanza kuripoti kwa sababu ya chanzo chake cha uhakika ambacho ni Mendes.

Wakala gani hatataka kufanya kazi na Romano? Anawasaidia kufanya kazi zao za udalali. Romano hawezi kuwa mahala, lakini ana namba za simu za mawakala wa mastaa wa Afrika, Amerika Kusini, Ulaya, Amerika Kaskazini na kwingineko.

Kumbuka wakati akifanya hivyo na Mendes, simu yake nyingine inafanya hivyo kwa Raiola ambaye anakuwa anamfahamisha kila maendeleo kuhusu Romelu Lukaku. Simu aliyotumia kuongea na Mendes ikikatika inaingia simu ya wakala wa David Luiz, Giuliano Bertolucci.

Simu yake inapata joto kila dakika. Kuna habari ambazo anazitafuta na kuna habari ambazo zinamtafuta kwa ajili ya kuongeza thamani za wachezaji. Katika biashara ya kisasa, mchezaji hapaswi kuwindwa na klabu moja tu. Ili wakala apate dili zuri mchezaji anapaswa kuwindwa na klabu nyingi.

Mtu anayeaminika zaidi kwa sasa ni Romano. Anaaminika kuliko hata Skysport au BBC. Hivyo ni rahisi kwa wakala kuisaka namba ya Romano kuliko yeye kusaka namba za mawakala. Uzuri ana namna ya kuchuja habari hizi na kutozithibitisha kama hana uhakika.

Wakala ndiye ambaye anamwambia mchezaji anakwenda kupimwa afya keshokutwa. Ingawa klabu hazipendezwi na kuvuja kwa habari hizi, lakini wanakuwa hawana jinsi kwa sababu wanashindwa kudhibiti urafiki wa wakala na Romano.

Lakini hapo hapo ni ngumu kwa klabu kujua habari za usajili zimevuja wapi kwa sababu Romano anaweza kuwa na uhusiano wa karibu na watu wa ndani ya klabu kama ambavyo nitaelekeza katika mtiririko huu kesho.

Katika uhamisho wa mchezaji kuna watu wengi wanahusika. Wanasheria, maskauti, wafanya mazungumzo (negotiators).

Ni ngumu kwa klabu kujua ni wapi habari yao imevuja, ingawa kila siku klabu huwa zinafanya siri suala la uhamisho wa mastaa kwa sababu ya kuogopa upinzani kutoka katika klabu nyingine ambao utaongeza dau la mchezaji.

Jaribu kuangalia namna ambavyo Arsenal ilifanya siri kuinasa saini ya Fabio Vieira. Imekuja ghafla tu, lakini hata hivyo dakika za mwisho ilivuja. Sio mchezaji ambaye sakata lake lilidumu kwa muda mrefu.

Unaweza kuona namna ambavyo sakata la Gabriel Jesus lilizungumzwa kwa muda mrefu kabla yake.

Ni nadra pia kwa wakala kumdanganya Romano kwa sababu anajua atamhitaji tena katika biashara za siku za usoni.

Kama Mendes akimdanganya Romano kuhusu dili yake moja, ni rahisi kwa Romano kulalamika ameingizwa chaka.

Siku nyingine simu ya Mendes ikilia katika simu ya Romano kujaribu kumweleza kuhusu dili fulani kwa lengo la kumpandisha bei, Romano anaweza kukataa huku akitoa shutuma za namna alivyoingizwa chaka katika uhamisho fulani uliopita.

Uaminifu kati Romano na mawakala ndio huu ambao kila siku umekuwa ukitupa habari za uhakika ambazo zimemfanya Romano atambe kwa kiasi kikubwa.

Ni uhakika huu huu ambao unamfanya aweze kuandika kwamba ‘Dili limekamilika kwa asilimia mia”.

Romano amewekeza katika namba za simu za mawakala kwa kiasi kikubwa. Endelea kumuamini. Hana maajabu ya kuota dili fulani limekamilika. Hayupo kila mahala ila simu yake inaitwa kila mahala.

Kwa jinsi ambavyo amejijengea mtandao wake ilikuwa rahisi kwake kuaminika kwa kiasi kikubwa kuliko vyombo vingine vya habari.

Alikuwa anajua nini anakitaka wakati akianza kusaka habari hizi. Kesho nitakunong’oneza kitu kingine ambacho kinamfanya Romano aonekane anafanya maajabu.

Mwanaspoti
 
Jamaa noma sana halali, 24 hrs, 7days a week anakimbiza tu, amenifanya niwaone Skysports miyeyusho, now niko twitter kwa Fabri Romano.
Japo Romano anatamba wakati wa usajili tu lakini anatamba haswaaa...sasa hivi nna uhakika hata vilabu vikubwa vitakuwa vinamfatilia Romano kimya kimya.

Unadhani Ten Hag hafatilii habari za usajiliza timu yake kwa Fabrizio Romano??
 
Kuna jamaa anaitwa "Ornstein" sina uhakika kama nimepatia spelling za jina lake.

Huyu habari zake kuhusu usajili wa primier league huwa ni za uhakika zaidi, kuliko hata Fabrizio Romano. Sema Romano yeye ni Ulaya nzima ila Ornstein ni premier league tu.
David ornstein ni habari nyengine, uzuri wa fabrizio romano yupo karibu sana na mashabiki wa mpira wa miguu kutokana na style yake ya kupost taarifa mara kwa mara ukilinganisha na hao wenzake ndio maana jamii inamuona kuwa ni mbora zaidi.

David ornstein akikwambia demu wako anachepuka na daemushin unatakiwa umuamini bila ya kuhoji.

Fabrizio romano = here we go
David ornstein = exclusive
 
David ornstein ni habari nyengine, uzuri wa fabrizio romano yupo karibu sana na mashabiki wa mpira wa miguu kutokana na style yake ya kupost taarifa mara kwa mara ukilinganisha na hao wenzake ndio maana jamii inamuona kuwa ni mbora zaidi.

David ornstein akikwambia demu wako anachepuka na daemushin unatakiwa umuamini bila ya kuhoji.

Fabrizio romano = here we go
David ornstein = exclusive
Ornstein nae yupo moto ila moto wa Romano naona ni wa petrol, jamaa anagusa kila kona.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom