Haya madhambi yalijulikana, yakaendelezwa na mifumo mibovu

mcubic

JF-Expert Member
Mar 3, 2011
10,307
6,514
Na Jenerali Ulimwengu

TANGU Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania ,John Pombe Joseph Magufuli, aingie madarakani yapata miezi mitatu iliyopita, tumeshuhudia hekaheka nyingi zilizosababishwa na hatua alizochukua yeye mwenyewe pamoja na wasaidizi wake wakuu.

Hatua alizozichukua kwa kiasi kikubwa zimekuwa hazitokani na sera mpya, ama utungaji wa sheria mpya, wala mabadiliko katika utendaji, kanuni na taratibu za utendaji serikalini. Kinachotokea chini ya utawala wa Magufuli ni kufufua sheria na taratibu za zamani ambazo zilikuwa zimefishwa na utawala uliopita na kuzifanya zifanye kazi, basi!

Hii ina maana gani? Ina maana kwamba tulikwishakuingia katika utamaduni wa kutupilia mbali sheria na taratibu za kuendesha utawala wa nchi, na badala yake tukawa tunaendesha nchi kwa hisia za wakubwa, kulingana na jinsi walivyoamka siku hiyo wanapotoa uamuzi.

Hivi majuzi tena, Magufuli amefanya uamuzi mwingine wenye maana kubwa kwa nchi yetu alipoamuru kukomesha vibali vya kuingiza sukari kutoka nchi za nje, biashara ambayo hakuna shaka kwamba ilitumika mara nyingine kuvihujumu viwanda vyetu vya uzalishaji wa sukari.

Najiuliza bila kupata jibu, hivi, kabla ya Magufuli kuingia madarakani, serikali ilikuwa haina macho ya kuona, masikio ya kusikia au akili za kufikiri na kubaini ukweli huu? Hivi, ni kweli kwamba serikali ilikuwa haijaambiwa na watu katika sekta hii kwamba kuendelea kuagiza sukari kutoka nje ni hujuma ya waziwazi dhidi ya viwanda vyetu?

Siamini kwamba serikali ilikuwa haijui. Na wala siamini kwamba hata maeneo mengine tuliyodhihirishiwa na hatua za Magufuli na wasaidizi wake hayakuwa yanajulikana. Yalikuwa yanajulikana, tena sana. Kilichotokea ni kwamba wakuu waliokuwa wakisimamia maeneo hayo waliona mwanya wa kujinufaisha, au waliagizwa wafumbe macho, wazibe masikio na wafifize bongo zao ili maslahi binafsi yapate faida.

Hali hii inashangaza katika nchi ambayo ina mifumo ya kijasusi kila mahali, polisi, posho. Iwapo mambo yote haya yanafanyika, na watu wanajua kwamba yanafanyika, vyombo vyote hivi ni vya nini, na ni kwa nini wakuu wa vyombo hivi wasichukuliwe kwamba ni wahujumu dhidi ya maslahi ya nchi?

Hujuma zote hizi kwa muda mrefu zimekuwa ni sehemu ya gumzo katika vijiwe. Katika vijiwe ndiko tunapata taarifa za kijasusi kuhusu nani amepewa kibali cha kufanya nini ambacho ni kinyume cha taratibu, na ni kwa sababu gani karuhusiwa kufanya hivyo, na ni kutokana na uhusiano gani mahsusi alionao na mkubwa yupi. Haya yote yako kijiweni, lakini wakuu wa usalama wanajifanya hamnazo.

Chini ya sheria ya uhujumu uchumi, wapo watu wengi waliopatilizwa kwa makosa madogo sana. Tunao mawaziri wa zamani waliohukumiwa kwenda jela, na hivi sasa wanafanyishwa kazi za kijamii kama mwendelezo wa adhabu yao. Kwa nini nisitie shaka kuhusu adhabu za mawaziri hawa iwapo mambo makubwa zaidi yanatendeka, kila mtu anajua kwa sababu yanaongelewa waziwazi, lakini hakuna anayeadhibiwa kama mawaziri hawa?

Sisemi kwamba linapobainika kosa mkosaji asiadhibiwe mpaka wakamatwe wakosaji wote, la hasha! Nisemacho ni kwamba inapokuwa makosa mengi yamejulikana, wakosaji wamebainika, makosa hayo yanajulikana na wakosaji wamebainika na wanaongelewa barabarani, kuwachukulia hatua watu wawili au watatu na kuwaacha wengine, ni ishara kwamba kuna namna.

Ni aina hii ya utendaji katika mifumo yetu ya utawala na utekelezaji wa sheria inayotutia hofu sisi wengine kwamba hatutawaliwi kwa misingi ya sheria, na kwamba ingawaje sote tu sawa lakini wako wengine ni sawa zaidi kuliko wengine, kama zilivyosema sheria za “Shamba la Wanyama,” riwaya ya George Orwell.

Ndiyo maana baadhi yetu tumekuwa tukifanya kampeni bila kuchoka kudai katiba mpya itakayotuhakikishia utawala wa sheria ulio bayana, na itakayoweka wazi haki za wananchi na jinsi ya kuhakikisha zinaheshimiwa. Hilo ni pamoja na mamlaka ya wananchi ambayo hayana budi kuwekwa juu ya ofisi zote nchini na juu ya watawala wote nchini.

Suala hili ni muhimu kwa sababu tunayaona madhara ya kuwaachia watawala uhuru wa kuamua watakavyo, hasa pale tunapopata bahati mbaya ya kuwa na watawala wenye utovu wa maadili au nakisi ya nidhamu. Hata kama si hivyo, hatuwezi kuwa na uhakika wa mienendo ya watawala kwa kuamini kwamba wao wenyewe watajiwekea vizingiti ili wasitende maovu. Binadamu wa aina hiyo walikuwapo zamani, si leo.

Nimeandika huko nyuma kwamba kadri juhudi za kujenga utaifa zinavyofifia ndivyo tutakavyoshuhudia watawala wakiibia nchi yao wenyewe. Hili linaonekana waziwazi hivi sasa, kwa sababu tunaendelea kuwakubali watawala ambao hawamo kabisa katika mradi wa kujenga utaifa, na nchi waliyokabidhiwa wanaiona kama mahali pa kuchuma na kisha wajiendee zao.

Anayehitaji ushahidi kuhusu hili na ajikumbushe: Yapata miaka takriban ishirini iliyopita vyombo vya habari nilivyoviongoza vilifichua wizi uliofanywa na waziri wa serikali ya wakati huo. Tulizingirwa, tukatishwa, lakini hatukukubali kuiachia stori hiyo hadi waziri huyo akajiuzulu, lakini kwa mkuu wake wa kazi kueleza masikitiko makubwa kwamba amempoteza msaidizi mahiri!

Katika mifumo mingine labda tungepongezwa kwa kufanya kazi iliyotakiwa ifanywe na vyombo vya dola. Kinyume chake tuliandamwa na baadhi yetu tukalipa kwa gharama kubwa. Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya waziri huyo mbali na kujiuzulu kwake kulikolalamikiwa na rais wake. Baadaye hatukushituka hata kidogo kwamba rais mwenyewe, katika kipindi hicho hicho, alikuwa amejigawia mgodi wa serikali na kuufanya wa kwake!

Zote hizo ni ishara kwamba mali ya nchi haina mwenyewe, na kwa hiyo hakuna mwenye uchungu nayo, na hiyo ni dalili niliyoisema ya nakisi ya utaifa kiasi kwamba tunaiona nchi kama mahali pa kuchuma kwa ajili ya wajanja wachache walioiteka. Tofauti yao na wakoloni ni kidogo sana, kwa sababu wakoloni hawakuwa na dhima ya kujenga taifa wala utaifa.

Dhima ya ukoloni ilikuwa ni kupora, kuchimba, kuchota, kukata au kung’oa chochote walichoweza kupata na kukipeleka kwao kwa ajili ya maendeleo na ukwasi wa himaya yao; hawakuwa na nia ya kutuendeleza isipokuwa katika kutufundisha kuwa wapagazi wao ili tuweze kuwasaidia katika uporaji huo, basi.

Kwa hiyo kama tunayo nia ya kweli ya kujenga taifa na utaifa hatuna budi kujiwekea misingi mipya kabisa, kwa sababu ile tuliyokuwa nayo ilikwisha kuyoyoma na hatunayo tena. Hatuna budi kuanza upya, la sivyo tutaendelea kudidimia kuelekea tulikokuwa kabla ya ujio wa wakoloni, ndiyo kusema idadi ya makabila yaliyotapaa katika nyika ya kile kilichokuja kuitwa Tanganyika (Zanzibar ni kitu kingine, nayo itakuwa na maelezo yake siku nyingine).

Dawa pekee inayoweza kuwadhibiti watawala wetu ili watutumikie kama vile walivyosema watatutumikia ni kuwawekea utaratibu wasioweza kuuzunguka. Utaratibu huo hauna budi kutokana na katiba ya kweli iliyoandikwa kwa maelekezo ya wananchi wenyewe baada ya majadiliano ya kina.

Vinginevyo tutaendelea kama tulivyo leo, wajanja wachache wakichukua kila fursa wanayopewa na mifumo mibovu kutuumiza na wananchi walio wengi wakiwa hawana mahali pa kukimbilia, mithili ya watumwa.

Raia Mwema
 
Back
Top Bottom