‘Kamati Kuu CCM kujivua gamba'
na Martin Malera, Dodoma
KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), kinafanyika leo mjini Dodoma, huku kukiwa na uvumi kuwa huenda kukatokea mabadiliko makubwa kwa wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho.
Miongoni mwa mabadiliko yanayoweza kutokea ni kuondolewa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusuf Makamba, Mhazini Mkuu, Ammos Makalla, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu Bara, George Mkuchika, Bernad Membe, Kidawa Hamid Salehe na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ramadhani Feroz.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa wiki moja sasa tangu kuanza kwa mkutano wa tatu wa Bunge mjini hapa, umebaini kuwa mazungumzo ya baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa NEC, ni kutaka Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, aisafishe sekretarieti na viongozi wengine kama hatua ya kujivua gamba.
Wakati wakitaka baadhi ya wajumbe wa sekretarieti watimuliwe, wanachama hao wa CCM wamekuwa wakitaja majina ya watu wanaodhani wanafaa kuchukua nafasi hiyo.
Duru za siasa kutoka ndani ya chama hicho Dodoma, zinawataja mtu kama Abdulhaman Kinana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi kuwa ndio wanaofaa kushika nafasi ya Makamba.
Baadhi ya wajumbe wa NEC wapo mjini hapa kwa zaidi ya wiki moja, wakidaiwa kupanga mikakati ya kupitisha hoja zao na kutoleana uvivu, hasa kwa wanachama wa CCM wenye mahusiano mabaya kiasi cha kushindwa kusalimiana.
Hadi sasa ajenda za kikao hicho zinatajwa kuwa ni tathmini ya uchaguzi mkuu kuanzia hatua ya kura za maoni, uteuzi hadi uchaguzi mkuu na ajenda inayohusu hali ya kisiasa nje na ndani ya chama na mengineyo kama mwenyekiti ataruhusu hoja hiyo.
Mmoja wa wabunge maarufu na mjumbe wa NEC, aliliambia gazeti hili kwamba kikao hicho kilichosubiriwa kwa hamu, lazima kifanye maamuzi mazito yakiwemo kuivunja au kuwatimua baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
"Kama kweli tunataka kuanza upya, lazima NEC ifanye maamuzi magumu ikiwemo kuwatimua baadhi ya watendaji ndani ya chama na hata wengine kuwapoka kadi yetu, vinginevyo tunajidang'anya," alisema mbunge huyo.
Tayari Kamati ya Maadili na Kamati Kuu (CC), imemaliza vikao vyake jana ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya NEC inayotarajiwa kukutana leo na kesho katika ukumbi maarufu wa White House mjini hapa.
Kwa muda mrefu sasa, CCM imekuwa katika wakati mgumu kutokana na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa muda mrefu na yaliyopata kuundiwa tume bila mafanikio.
Malumbano ya hivi karibuni, yalihusisha Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), dhidi ya viongozi wastaafu akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta.
Mbali ya malumbano ya wenyewe kwa wenyewe, chama hicho pia kimekuwa kikiandamwa na tuhuma za ufisadi hasa kwa baadhi ya wajumbe wake ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC).
Wapo wanachama wanaoamini kuwa suluhu ya kuondokana na hali hiyo ni kuwavua uongozi makada hao na kuwaacha na ubunge ambao umetokana na ridhaa ya wananchi wa majimbo yao.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shambwe Shitambala na Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Ileje, Henry Kayuni, wamejiunga na CCM mjini hapa.
Hafla ya kuwakabidhi kadi wanachama hao iliyohudhuriwa na wabunge wote wa CCM, ilifanyika katika viwanja vya ukumbi wa White House mjini hapa na walikabidhiwa na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi, Shitambala ambaye amepata kusimamishwa uongozi na CHADEMA, alisema kuwa amefurahi kurudi CCM kwani ni chama kikubwa na kuahidi atakuwa mwanachama mwaminifu kwa chama chake.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema kuwa kuna vyama vingi vya siasa nchini, lakini vingine ni mkusanyiko wa wanaharakati.
"Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo, Nashangaa kuna wabunge wa baadhi ya vyama, hata baada ya kuwa wabunge, lakini bado silka zao bado ni za kiwana harakati. Chama imara ni CCM," alisema kwa kifupi Kikwete.