HATARI: Majipu kutumbua majipu

Msanii

Platinum Member
Jul 4, 2007
25,253
36,508
Heko kwa kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya 5.
Pamoja na pongezi hizi lakini sitaacha kusema ninayoyaona kwenye utekelezaji wa sera ya kuwahudumia wananchi wanyonge wa Tanzania.

Serikali iwe makini na utendaji ama mwenendo wa Mawaziri wake ambao wanaamini kuwa kumpendezesha mkuu ni kuiga utendaji wake badala ya kujifunza utendaji wake unamaanisha na nini na tija ipi itakiwayo.

Rais ni Taasisi tena taasisi kubwa, Waziri Mkuu pia ni taasisi kwani sambamba na kuwa mkono wa kulia wa utendaji wa Rais lakini pia anasimamia wizara zote na mawaziri kuona wanatekeleza yale waliyoapa kutekeleza.

Kuna baadhi ya mienendo ya Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya inalenga kuharibu taswira nzuri ya utekelezaji wa dira ya Hapa Kazi Tu. Nikianza na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, utakuta ni walewale tangu kipindi cha fukuto la mtikisiko mkubwa wa maadili ya uongozi katika kada zote na hivi leo wamegeuka wakiwa wapiga dananda wakubwa wa sera za Awamu ya Tano. Lakini mikoa na wilaya zao kuna matatizo makubwa ambayo kimsingi yapo chini ya maamuzi yao kuyatatua. Migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za nchi, utendaji usioakisi maadili na utawala bora. Mfano hai ni mitafaruku ya wakulima na wafugaji ambapo kila kukicha tunashuhudia mapya, hivi juzi maafisa wawili wanyamapori wameuawa na wakulima wenye hasira baada ya mifugo yao zaidi ya 1000 kukamatwa kwa tuhuma za kuingia kwenye hifadhi ya taifa huku kukiwa na malalamiko kuwa kila wanapowakamata huwa wanatozwa faini kuanzia shs milioni kumi na zaidi kwa kila kundi la mifugo, na faini hizo hazikatiwi risiti na kama risiti itatolewa basi fedha inayoandikwa humo hailingani na faini iliyolipwa. Haya yanajiri na watu wakilalamika siyo kwamba wakubwa hawasikii bali wanaona haiwahusu saana.

Miradi mingi ya maendeleo haishuki katika ngazi za Kata hadi vijiji/ mitaa kwa muda mrefu huku HAZINA ikiendelea kupeleka fedha kwa kugharimia miradi iliyolengwa..... Miradi ambayo inafanikiwa kutekelezwa mingi yake huwa katika viwango hafifu. Huu ni ugonjwa sugu na wanaoulea ni walewale ambao leo wanaimba wimbo mpya.

Kinachoendelea sasa ni system yote ya uongozi kupiga kwata ya utumbuaji majipu huku mambo ya msingi yakiendelea kulala. Njaa inakuja, Magonjwa ya mlipuko yanashamiri, shule za msingi na sekondari zipo katika hali mbaya kabisa, Vituo vya afya havikidhi vigezo vya kutoa huduma maridhawa kwa wananchi, miundombinu ya barabara kuharibika kipindi kifupi tangu kujengwa kwake....

USHAURI.
Rais anajua anachokifanya na anakifanya vyema, vivyohivyo waziri mkuu na ofisi yake. Mawaziri mnapaswa kujikita kuhudumia zaidi ili kuleta uwiano wenye tija wa kiutawala. Katika hospitali siyo wahudumu wote wanakaa chumba cha kufunga vidonda ama kuchoma sindano wamegawanyika katika kada mbalimbali huku kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Wakuu wa Wilaya wasimamie utawala bora katika himaya zao vivyohivyo wakuu wa mikoa. Tumbueni majipu kwa sababu hakuna namna nyingine tena ila kabla ya kutumbua jipu mjiulize kama ninyi si majipu pia.

Tunahitaji maafisa ugani wafike maeneo mengi nchini kusaidia juhudi za taifa kuondokana na janga la njaa. maafisa misitu watoke mijini waende field kutimiza wajibu wao. Wataalam wa madini acheni kujazana mijiini enendeni kwenye maeneo yenye hadidu zenu mkalete tija kwa Taifa. Maafisa biashara wilaya safisheni madawati yenu ondoeni urasimu wa kuwahudumia wananchi kupata leseni na usajili wa biashara zao.

TRA ambayo kimsingi bado ni jipu baya mno kwa maendeleo ya uchumi wetu, achaneni na utoto wa kuendelea kutumia servers za majaribio kutoa huduma kwa miaka yote hii. Kila kukicha tatizo la server kuwa down limekuwa ni wimbo mzuri kutoka midomoni mwao. Mnakusanya kodi zetu hebu wekeni mazingira ya kodi hizo kuingia serikalini kwa wakati unaotakikana. Achaneni na mazoea.

UTUMISHI. iweke description ya productivity katika kila ajira wanayoitoa na kuwepo na job score cards kila idara ili kubaini majipu andamizi yaliyojificha kwenye utumishi wa umma.

Chonde chonde Rais Magufuli. kuwa makini sana na wasaidizi wako. kwenye kazi hakuna urafiki, kwenye kazi hakuna undugu
SASA KAZI TU
 
Back
Top Bottom