Hassan Mwinyi ateuliwa kuongoza waangalizi wa Afrika Mashariki uchaguzi mkuu Uganda

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ameweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mkubwa zaidi kuongoza waangalizi wa uchaguzi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwenye Uchaguzi Mkuu wa Uganda unaofanyika kesho Alhamisi, Februari 18, 2016.

Mwinyi ambaye Mei 8 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 91, ameteuliwa kuwa Kiongozi wa Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye Uchaguzi Mkuu wa Uganda na sasa amepiku rekodi iliyowekwa na Arthur Moody Awori, aliyeongoza timu ya waangalizi wa jumuiya hiyo waliosimamia Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015.

Awori ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Kenya, alikuwa na umri wa miaka 88 wakati alipoteuliwa na EAC kuongoza waangalizi wa jumuiya hiyo kwenye uchaguzi huo wa Tanzania.

Taarifa ambazo Raia Mwema imezipata kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa mzee Mwinyi amekuwa kivutio miongoni mwa waangalizi hao takribani 50 kutoka EAC kutokana na umakini na utimamu wa mwili na akili zake, ingawa umri wake unaonyesha vinginevyo.

“Kusema kweli wenzetu huku wamemfurahia sana mzee Mwinyi kutokana na busara zake na uzoefu mkubwa anaouonyesha katika wadhifa wake huu wa sasa.
“Watu waliposikia kwamba ana umri wa miaka 90 walidhani watakutana na mtu mzee lakini kwa kweli wameshangazwa na utimamu wake wa mwili na akili. Ameendesha mafunzo kwa waangalizi na kusema kweli Mwenyezi Mungu amemjalia afya njema rais wetu mstaafu,” alisema Shy-Rose Bhanji, ambaye ni mmoja wa wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) aliyeteuliwa kuwa mmoja wa waangalizi wa uchaguzi huo.

Mwinyi ambaye Watanzania pia wanamfahamu kwa jina la utani la ‘Mzee Ruksa’ alizaliwa katika kijiji cha Kivure mkoani Pwani, mwaka 1925, pia ndiye mtu pekee hapa nchini ambaye amewahi kuwa Rais wa Zanzibar na kisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Gazeti hili limeambiwa na vyanzo vyake vya kuaminika kutoka nchini Uganda kuwa akiwa nchini humo, Mwinyi anaendelea na ratiba yake ya kawaida ya kufanya mazoezi na kuswali swala zote kwa mujibu wa matakwa ya dini yake ya Kiislamu.

Timu hiyo ya waangalizi wa EAC inaundwa na watu tofauti wakiwamo wabunge kutoka EALA, vyombo vya utawala bora kutoka nchi hizo, mashirika yasiyo ya kiserikali na Tume za Uchaguzi za nchi hizo.

Katika EALA, Tanzania inawakilishwa na Shy-Rose, Maryam Ussi na Abdullah Mwinyi ambaye ni mtoto wa mzee Mwinyi.

Kwa mujibu wa taratibu, nafasi ya kiongozi wa waangalizi (kama Mwinyi) huteuliwa baada ya mashauriano ndani ya sekretarieti ya EAC, huku wabunge kutoka EALA huteuliwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki.

Nchi zote nne za EAC zimepewa nafasi tatu za wabunge wao walio katika EALA kuwa waangalizi wa uchaguzi huo; huku wale wa Uganda ambao ni wenyeji wakiwa hawajatoa mbunge.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa Uganda, msemaji wa Mwinyi, Dk. Abdallah Makame, alisema hali iko shwari na kwamba wanataraji uchaguzi utakwenda vizuri kama ilivyopangwa.

“Kwa Tanzania Alhamisi ni siku ya kazi lakini huku Uganda wao wameifanya iwe siku ya mapumziko na hivyo watu hawatakwenda kazini na watapiga kura kuchagua Rais na wabunge wao,” alisema.

Uchaguzi wa Uganda
Rais Yoweri Museveni wa Uganda anawania tena urais wa Uganda kupitia chama chake cha National Resistance Movement (NRM) huku akishindana na wagombea wengine saba kutoka vyama tofauti wakiwamo watatu binafsi.

Wagombea urais wengine wa Uganda ni Dk. Kizza Besigye wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC), Benon Biraaro wa chama cha Uganda Farmers (UFP), Abel Bwanika wa People’s Development (PDP) na Amama Mbabazi wa chama cha Go Forward.

Wagombea wengine watatu wa nafasi hiyo, Venansius Baryamureeba, Joseph Mabirizi na Faith Kyalya; ambaye ni mgombea pekee mwanamke, wanawania nafasi hiyo kama wagombea binafsi.

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa tatu chini ya mfumo wa vyama vingi nchini Uganda na katika chaguzi zote zilizopita, Museveni ameibuka mshindi na kufanikiwa kukaa madarakani kwa takribani miaka 30.

Hadi sasa, Museveni ndiye Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko wengine wote miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, akiwa ameingia madarakani akitokea msituni mnamo mwaka 1986.

Museveni ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikosoma kati ya mwaka 1967 hadi mwaka 1970 ambapo pia alikuwa mwanaharakati na kiongozi wa Chama cha Wanafunzi Wanamapinduzi wa Afrika (USARF).

Kama ilivyokuwa katika chaguzi tatu zilizopita, mpinzani mkuu wa Museveni anatarajiwa kuwa Besigye wa FDC; swahiba wake wa kisiasa aliyewahi kuwa daktari wakati wakiwa msituni, ambaye juzi Jumatatu alikamatwa na Polisi katika tukio lililosababisha vurugu jijini Kampala na maeneo mengine nchini humo.

Tayari, Uganda imeweka historia kwa Museveni kushiriki katika mdahalo wa wagombea urais uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita; na wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ndiye rais wa kwanza aliye madarakani miongoni mwa nchi za Afrika kushiriki katika mdahalo wa namna hiyo.
Utaratibu ukoje?

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, katika uchaguzi huu kuna jumla ya wapiga kura milioni 15 walioandikishwa.

Katika nafasi ya urais, mshindi anatakiwa kupatikana kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa na kama mshindi hatapatikana katika hatua ya kwanza, uchaguzi utarudiwa ‘raundi’ ya pili kwa kushindanisha washindi wawili wa kwanza katika duru la kwanza.

Hii ni tofauti na Tanzania ambapo katika Uchaguzi wa Rais, mshindi ni yule anayepata kura nyingi kuliko washindani wake; hata kama hajapata asilimia 50 ya kura zote.

Katika uchaguzi wa wabunge, sheria zake zinafanana na zile za hapa Tanzania kwani mshindi ni yule aliyepata kura nyingi kuliko wengine.


Chanzo: Raia Mwema
 
summary ya habari hiyo ni kuwa waganda wameshangaa mzee mwinyi kuwa na umri mkubwa wa miaka 91 lakini ana utimamu na mwili wake ni imara ukilinganisha na umri wake kiasi kwamba ameendesha mafunzo ya waangalizi wa uchaguzi kwa umahiri mkubwa na bila kusahau amekuwa akiamka asubuhi na kufanya swala kama kawaida. machache kati ya mengi ni hayo
 
hivi wazenj wana siri gani,maana hata aboud jumbe yupo,na atakua kamaliza miaka 100 yule


Wazenj wengi ni wasomi wa dini ya kiiaslam,kama umesoma qul, an mwenyezi mungu kupitia mtume wake amefundisha kila kitu hasa kuzingatia afya yako ili uweze kumuabudu vyema,hasa kwenye vyakula, kitugani ule na kitugani usile, na wakatigani unapaswa ule na chakula kikiwa ktk hali gani, na ukishindwa amekupa mwezi mmoja kila mwaka ili upunguze sumu mwilini (fungeni mpate afya) maneno haya unayaona ya kawaida lakini ni mapana sana. LEO HII MTU ANAFUNGA HETI KWA KILE ANACHOKIPENDA! Ni kutojua umuhimu wa funga. MTUME MUHAMAD ALIKUA PROFESA NA UKIFUATA MAFUNDISHO YAKE MTU HAWEZI KUKUDANGANYA.utaishi sana. Maana ukiwa na afya njema hata mwenyezi mungu utamuabudu vyema kabisa, na ndio lengo lake kufundisha haya ili usitoe sababu za kiafya.
 
AKishindwa Museven tutegemee uvhaguzi ulikuwa siyo huru wala haki.Hiyo African Democracy

Mkuu hakuna uchaguzi nikama hapa kwetu Tz kupanga mistari ya uchaguzi kudanganya jumuia za kimayaifa lakin matokeo yapo teyari.

hakuna demokrasia ni uhuni tu musseven niwalewale ooo ni yuleyule kama hapa kwetu.
 
Huyu Mzee nae bora angeendelea kuwa kimya kuliko huu unafiki, kwake kuna mshinda kudandia ya Uganda atayaweza?
 
Rais mstaafu wa Serikali ya awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ameweka rekodi ya kuwa kiongozi mkubwa zaidi kuongoza waangalizi wa uchaguzi miongoni mwa nchi za Afrika mashariki kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda unaofanyika kesho Alhamisi, February 18, 2016.

Mwinyi ambaye Mei 8 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 91 ameteuliwa kuwa kiongozi wa waangalizi wa jumuiya ya Afrika mashariki(EAC) kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda na sasa amepiku rekodi iliyowekwa na Arthur Moody Awori, aliyeiongoza timu ya waangalizi wa jumuiya hiyo waliosimamia uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015.

12705223_1041901332540991_3145360163214989803_n.jpg

Katika Viongozi Wote Wastaafu Tanzania, Namheshimu sana Mzee Ally Hassan Mwinyi, Kwa Kuwa Naamini Ni Mtu Muungwana sana. Na Hana Hila hila Na Unafiki!
 
summary ya habari hiyo ni kuwa waganda wameshangaa mzee mwinyi kuwa na umri mkubwa wa miaka 91 lakini ana utimamu na mwili wake ni imara ukilinganisha na umri wake kiasi kwamba ameendesha mafunzo ya waangalizi wa uchaguzi kwa umahiri mkubwa na bila kusahau amekuwa akiamka asubuhi na kufanya swala kama kawaida. machache kati ya mengi ni hayo
Mkuu umefanya vizuri kuweka summary ya kile kilichowashangaza Waganda! Sasa hili tutusa lilishindwa nini kuweka summary mpaka linatumwagia gazeti zima hapa? Elimu yetu ina shida sana, ama kweli kizazi hiki ni cha "cut and paste". Yaani vijana wengi hawawezi kabisa kufanya summary ya kitu chcochote!! Huu ni udhaifu!
 
AKishindwa Museven tutegemee uvhaguzi ulikuwa siyo huru wala haki.Hiyo African Democracy
Natabiri kitakachotokea Uganda kinaweza kuwa sawasawa ni kilichotokea Zanzibar Oktoba mwaka jsna.

Iwapo Museveni atarealize kuwa amebwagwa na Besigye, atakachofanya ni kumtuma 'Jecha' wa Tume ya Uganda kuyafuta matokeo yote kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na kasoro chungu nzima!

Nchi za Afrika Mashariki zina mfanano fulani, ilianza Kenya mwaka 2007 ambapo Kivuitu alileta balaa kubwa iliyoleta machafuko makubwa nchini humo hadi kusababisha akina Uhuru Kenyatta na mwenzie Ruto kuburuzwa ICC kule The Hague, baada ya 'Jecha' huyo wa Kenya kumtangaza Kibaki kuwa mshindi wa Urais, wakati in reality alibwagwa na Raila.

Huo ugonjwa wa 'kiafrika' umehamia Zenji Oktoba mwaka jana ambapo Jecha alikurupuka baada ya 'kuamrishwa' na watawala wa TZ aufute uchaguzi uliokuwa huru na haki uliofanyika visiwani humo hadi kusababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa kuwahi kushudiwa hapa TZ tokea Taifa hili lirejee kwenye mfumo wa chaguzi za mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Most likely sasa itakuwa zamu ya Uganda nchi pekee iliyokuwa imebaki ndani ya East Africa kukumbwa na kadhia hiyo iliyozoeleka ya kupuuza maamuzi ya wananchi wanayoyafanya kupitia kwenye sanduku la kura.

Tunaendelea kumwomba Mungu ili awaepushe waganda kuwaepusha wao wasiingie kwenye ugonjwa huo wa 'East Africa' wa watawala walioko madarakani 'kuamrisha' Tume zso kutomtangaza mgombea wa Urais kutoka chama cha upinzani, hata kama atakuwa ameshinda kwenye ballot boxes, kutokana na dhana waliyojijengea watawala wa nchi hizi zetu kuwa nchi 'zao' haziwezi kutolewa kwa vijikaratasi vya kupigia kura!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom