hasara za kushindwa kumwelimisha mwanamke | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

hasara za kushindwa kumwelimisha mwanamke

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Apr 26, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 26, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  MWAKA 2008, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), lilitoa ripoti iliyoonyesha kuwa nchi nyingi duniani zimehamasika kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa kike.

  Hata hivyo, taarifa hii haikani hali halisi kuwa katika nchi nyingi hasa zile zinazoendelea, elimu kwa watoto wa kike bado limekuwa suala la kubahatisha.

  Kwa mfano, ripoti hiyo inasema asilimia 60 ya watoto wenye umri wa kwenda shule lakini wanashindwa kusoma katika nchi mbalimbali duniani hususan zile zinazoendelea, ni wasichana.

  Hata wale wanaobahatika kusoma lakini wakakatisha masomo, wasichana ni 100 milioni katika watoto 150 milioni wanaodondoka shuleni kwa sababu mbalimbali.

  Bila shaka zinapotajwa nchi zinazoendelea, Tanzania haikosekani. Ni kwa sura hii, Tanzania haiwezi kujiengeua kutoka katika kundi lenye idadi kubwa ya watoto wa kike wanaokosa fursa za elimu.

  Disemba 2010, Shirika la Haki elimu lilitoa taarifa iliyoweka bayana ukweli kuwa, kutowapa fursa watoto wa kike, ni hasara kubwa kwa taifa kwa kuwa watoto wa sasa ndio wanawake wa kesho.

  Hivi nani hajui nafasi na mchango wa wanawake katika ustawi wa familia na maendeleo ya nchi kwa jumla?Mchango wao kama mhimili muhimu katika jamii, ndio unaotulazimisha kupiga kelele kuhusu elimu kwa wasichana.

  Nafasi ya mwanamke katika jamii ni sawa na ile ya injini katika gari.Kwa kuwa injini ndiyo inayoipa gari uhai wa kutembea, vivyo hivyo kwa wanawake kwani nao wana mchango muhimu katika kuisukuma jamii kupata maendeleo ya kweli.

  Hata tunapoziangalia jamii katika nchi zilizoendelea, mojawapo ya mafunzo tunayoweza kupata ni kuwa wanawake walithaminiwa tangu wakiwa wasichana wadogo kwa kuwezeshwa kupata haki na fursa muhimu ikiwemo elimu tena iliyo bora.

  Kwa nchi kama Tanzania iliyo na dhamira ya kujiletea maendeleo, fikra, tabia na mitazamo hasi dhidi ya wanawake hazina budi kuwekwa kando na kusahaulika kabisa na wanajamii.

  Haya ni mabadiliko na kimsingi hayahitaji gharama kubwa kuyafanya.Lililo muhimu ni nia thabiti, uelewa wa hali halisi kuhusu haki za wanawake na kisha kuwa na hamasa ya pamoja kama jamii.Kwa pamoja haya yatatusaidia katika mapambano ya kutafuta haki kwa wanawake.

  Faida za kumwezesha mwanamke katika nyuga mbalimbali ikiwemo elimu, zipo dhahiri shahiri.Tukianza na uchangiaji wa pato la taifa, wanawake wamekuwa mstari wa mbele kulipa kodi na ushuru wa kila aina, tena kwa uaminifu mkubwa.

  Mbali ya kulipa kodi, wanawake waliojiriwa ama kujiajiri ni wanunuzi wazuri wa bidhaa na huduma nyingi ambazo zinalipiwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Tafiti mbalimbali zinaonyesha mwanamke hufanya kazi za uzalishaji kwa muda mrefu (takribani saa 18).

  Hili linathibitishwa na Sera ya Maendelo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2010 inayosema kuwa asilimia 80 ya nguvu kazi vijijini ni wanawake na kwamba wao ndio wanaozalisha asilimia 60 ya chakula cha jamii.

  Aidha sera hiyo inasisitiza kuwa asilimia 90.4 ya wanawake ni wazalishaji mali katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, japokuwa wanakabiliana na matatizo ya nyenzo duni, ukosefu wa mitaji, ujuzi mdogo na kutokuwa na haki miliki ya ardhi.

  Kwa namna hii, ikiwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Tanzania, bado hatuoni haja ya kuwawezesha wanawake ikiwemo kuwapa elimu bora ya kilimo kwa faida ya nchi?

  Zipo tafiti nyingine zinazothibitisha kuwa hata katika suala la mgawanyiko wa majukumu na kazi, wanawake wanachangia maendeleo kwa kiwango kikubwa kwa kufanya kazi zenye manufaa kwa jamii kwa miaka mingi.

  Kwa mfano, katika jamii nyingi za vijjini wanaume wamekuwa na tabia ya kutoroka na kwenda mijini kutafuta kazi wakiacha lundo la watoto chini ya uangalizi pekee wa wanawake.

  Hivyo wanawake hubaki na jukumu la kuwapatia watoto matibabu wakiumwa,kuwasomesha na kuwapa chakula na mavazi. Wakati wanawake wakitaabika na maisha, wanaume wapo mafichoni wakila raha huku wakitoa udhuru kwa kuwaeleza wake zao eti mambo sio mazuri huko waliko!

  Tanzania ya sasa inayumbishwa vilivyo na uwepo wa mila na desturi zinazorudisha nyuma maendeleo na hata utu.Uzoefu unaonyesha wanawake wakielimika,huwa mstari wa mbele kuleta mabadiliko dhidi ya mila zinazokinzana na maendeleo.

  Hata amani na utulivu katika jamii, wanawake ndio wanaoongoza kwa kutunza tunu hizi adhimu kwa taifa. Si aghlabu kusikia wanawake wakiwa chanzo cha migogoro na fujo za kisiasa au mapigano ya koo kama ilivyo katika baadhi ya maeneo nchini.

  Furaha Maugo ni mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi 0765434357
   
Loading...