Mirungi imepigwa marufuku katika nchi mbalimbali za Scandinavia, lakini bado inajadiliwa Uingereza kama ni katika kifungu cha madawa ya kulevya au hapana!
Ni mmea ambao umewekewa sheria kali au kupigwa marufuku nchi nyingi duniani.
Mirungi imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wengi kuanzia
Yemen, Ethiopia, Kenya, Tanzania na nchi ambazo watu wa nchi hizi wanaishi. Uingereza ambapo bado ulaji wa Mirungi haujapigwa marufuku; kila siku ndege inateremsha Mirungi kutoka Ethiopia na Kenya kwa wingi, na biashara yake imekuwa na nguvu kwa jamii ya Wasomali, Wayemen, Waethiopia na Watanzania wanaoishi katika nchi hiyo.
Utagundua haraka sehemu au maeneo na nyumba zinazouzwa au kuliwa Mirungi kwa athari za uchafu wa vijiti vya Mirungi na majani yake yanayotupwa ovyo ovyo kila pahali na kuwa kero kubwa kwa wakazi wa jirani wa maeneo hayo na hata Manispaa au Serikali za Mitaa (Borough Councils) za maeneo hayo Uingereza.
Kadhalika, kwa unafuu wake wa usafirishaji kwa ndege, majani hayo husafirishwa kuelekea sehemu zingine kama
Wales, Rome, Amsterdam, Canada, Australia, New Zealand na
Marekani.
Ulaji wa Mirungi umekuwa ukiongezeka sana katika jamii mbalimbali hususan Yemen, Kenya na Tanzania na haswa walaji wa kiada wakiwemo wanawake na hata watoto- na kusababisha kuongezeka mahitajio yake.
Hii ni kwa sababu Mirungi ni kilevi cha kawaida katika jamii kama ilivyokuwa sigara ni kilevi kikubwa cha jamii ya Ulaya na Marekani hadi hivi karibuni baada ya kampeni za kila siku za kupiga vita. Ni kilewesho na uraibu ambao haujafikia daraja na uzito wa pombe. Haki ya uraibu huu umewatatiza Wasomi wengi wa Yemen na jamii zingine kufikia ufumbuzi wa kukata katika kuzima balaa hilo. Hata hivyo, kama tutakavyoona mbele ya makala hii, Wanasomii wengi wakubwa wa nchi mbalimbali duniani, wameeleza madhara yake.
Kwa kujitetea, walaji Mirungi wanaamini kuwa majani hayo huwapatia nguvu, na uchangamfu na mliwazo wa furaha Handasi au Nakhwa kwa lugha yao.
Hakuna Mirungi, hakuna nguvu, na hivyo hakuna kufanya kazi, Hakuna kufanya ngono (jimaa), kusoma, au chochote, hivyo ndivyo wanavyodai.
Pamoja na madhara yake na maonyo makali ya taasisi za tiba na mashirika ya Afya duniani, lakini inaelekea kumalizika matumizi ya Mirungi moja kwa moja, ni jambo linaloonekana litachukua miaka mingi sana na vizazi vingi huko Yemen na hata Afrika Mashariki. Yemen ni nchi ambayo uraibu huo umetawala hadi kufikia watu kulazimika kuwekea nyakati maalumu za ulaji.
Miaka kadhaa nyuma, Raisi wa nchi hiyo Aliy Abdullaah Swaalih aliwahi kueleza hadharani kuwa naye ni mlaji wa Mirungi lakini mwisho wa wiki; ingawa siku za mbeleni akaja kutangaza hadharani anajaribu kuachana nayo moja kwa moja. Mwaka 2002, wafanyakazi wote wa serikali ambao mwanzoni walikuwa wakila Mirungi kazini, walipigwa marufuku kuila kazini.
Lakini leo hii, ulaji umeongezeka sana kuliko ulivyokuwa huko nyuma.
Anasema mwandishi mmoja maarufu Yemen: Mirungi (Qaat)
ni kileo cha watu wetu. Ni kiongozi wa kijani anayeongoza nchi yetu. Ni ufunguo wa kila kitu na ni makutano ya vikao na minasabati yote ya kijamii. Ni kitu kisichoelezeka kinachoeleza kila kitu