Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Said Miraj amemshushia tuhuma tatu mgombea urais wa chama hicho visiwani Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, huku akisisitiza kuwa ili kukinusuru chama hicho ni lazima afukuzwe.
Miraj ambaye kabla ya kujiunga na ADC alikuwa kada wa CUF, ameyataja shutuma hizo kuwa ni; Hamad Rashid kutumiwa na CCM kushinikiza uchaguzi uliofutwa Zanzibar kurudiwa, ubadhirifu na kupanga njama za kutaka uongozi wa chama hicho kinyume na katiba na taratibu.
Hata hivyo, Hamad Rashid amejibu madai hayo akisema: “Tuhuma dhidi yangu zimeanza siku nyingi tangu nikiwa CUF. Kama mazungumzo ya CUF na CCM yanaendelea sipaswi kusema nitashiriki uchaguzi wa marudio? Labda tuwaulize hao waliopo katika mazungumzo sababu za kutovishirikisha vyama vingine vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa Zanzibar.
Kwa nini nisiamini Miraj anatumiwa na CUF. Nilieleza wazi kuwa ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) haikutenda haki kufuta uchaguzi. Kama nia yangu ingekuwa kuwa mwenyekiti wa ADC ningegombea tangu zamani.”
Hamad Rashid ambaye alipewa kadi namba moja baada ya kujiunga na ADC Julai 23 mwaka jana, alisema yeye ndiye aliyemshinikiza Miraj kujiunga na chama hicho na kugombea uenyekiti.
Katika tuhuma zake, Miraj alisema: “Hamad alifukuzwa CCM kwa hila, akafukuzwa CUF kwa kutaka madaraka na sasa analeta hayo mambo ADC. Huku tutamfukuza pia maana anataka kukifanya chama hiki kuwa tawi la CCM.”
Akizungumza jana, Miraj alisema atatoa msimamo wake kuhusu suala hilo Januari 11 katika mkutano na waandishi wa habari akisema: “Ikiwa mimi nitang’oka katika chama nitaeleza uozo wote anaoufanya Hamad Rashid na ikiwa nitabaki katika chama nitatoa masharti yangu.”
Miraj alisema Hamad Rashid ni mlezi wa chama hicho na si kiongozi na jukumu lake ni kutoa ushauri kwa viongozi wa ADC, hivyo hapaswi kuingilia utendaji na kutoa matamko.
“Kuna njama za kutaka kuniondoa mimi niliyechaguliwa kikatiba na zinafanywa na wajumbe wa bodi ya wadhamini ya ADC akiwamo Hamad,” alisema huku akionyesha barua za malalamiko kuhusu suala hilo zilizoandikwa na wanachama 30 kwenda ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.
“Iweje (Hamad) aitishe vikao kuhoji yanayofanyika ndani ya chama? Baada ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar aliandika barua kupinga matokeo bila viongozi wa ADC kujua. Alitoa kauli uchaguzi Zanzibar urudiwe wakati akijua mazungumzo yanaendelea kati ya CCM na CUF.”
Alisema Hamad Rashid alionekana kuwa msaliti tangu mwanzo na ndiyo sababu viongozi wakuu wa ADC hawakushiriki kampeni za chama hicho visiwani Zanzibar.
Chanzo: Mwananchi