SULEIMAN JONGO NA HAMIS SHIMYE
HALI ya hewa ndani ya CHADEMA imechafuka kutokana na baadhi ya wanachama kusema watapinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa viti maalumu, endapo utakaorudiwa utaendelea kuwa na mwelekeo wa upendeleo.
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe na Msimamizi wa uchaguzi huo, Dk. Kitila Mkumbo, kuuahirisha kutokana na rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya chama hicho kilisema wajumbe wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) hawajaridhishwa na uamuzi wa Mbowe.
Wajumbe hao walisema uamuzi wa kuahirisha uchaguzi ulilenga kuwabeba wabunge waliomaliza muda wao, ambao waliangushwa kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Kiramuu, mjini Dar es Salaam.
"Wajumbe hatujaridhika, katika uchaguzi ule tuliamua kufanya mabadiliko na kuleta chama chenye sura mpya, lakini Mwenyekiti amekataa uamuzi wetu na kufuta uchaguzi,'' kilisema chanzo hicho cha habari. Chanzo hicho kiliongeza: "Ukabila tumepania kuumaliza kwa kuanza kubadilisha taswira ya wabunge wote wa viti maalumu kutoka kanda ya kaskazini ili uwepo usawa.''
Mjumbe mwingine ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema uamuzi wa Mbowe ni wa ‘funika kombe mwanaharamu apite', kwani alijua watu wake wameanguka kwenye uchaguzi huo. "Uchaguzi haukuwa na rushwa bali ni kubwagwa kwa wabunge, Halima Mdee, Susan Lyimo, Anna Komu na Grace Kihwelu, huku Lucy Owenya pekee akipitishwa kutokana na heshima ya mdhamini wa chama, Philemon Ndesamburo,'' alisema mjumbe huyo.
Chanzo kingine ndani ya CHADEMA kilisema Kamati Kuu ya chama hicho imeamua mfumo wa kuwapata wabunge viti maalumu usiwe wa kupigiwa kura, badala yake watateuliwa na chama. "Tunayajua aliyoamua Mbowe kwenye Kamati Kuu, kwani hakutakuwa na uchaguzi wa wabunge wa viti maalumu na badala yake watateuliwa na Kamati Maalumu,'' alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Erasto Tumbo, alisema viongozi wa juu walifanya mkutano na leo au kesho watatoa uamuzi wa hatima ya nafasi hizo. "Kikao cha juu ndicho kitaamua. Sijui ni njia ipi itatumika kuwapata wagombea hao kwa kuwa mimi si msemaji wa mambo hayo. Viongozi ndio wenye jukumu la kutoa ufafanuzi na leo au kesho taarifa itatolewa," alisema Tumbo.
Katika siku za hivi karibuni chama hicho kimekuwa kwenye migogoro ya uchaguzi mara kwa mara, hususan kutokana na kuwepo makundi miongoni mwa viongozi wakuu wa chama hicho. Mwaka jana matokeo ya uchaguzi wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA) yalifutwa na uchaguzi kuahirishwa, ambapo aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, David Kafulila, aliamua kukihama chama hicho na kujiunga na NCCR-Mageuzi. Uchaguzi wa BAWACHA pia uliahirishwa kutokana na kuibuka madai ya upendeleo.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Tarime kupitia chama hicho, Charles Mwera, amekihama na kujiunga na CUF, akidai kuwepo kwa ubabaishaji na rushwa.
Jimbo la Segerea pia hali si shwari kutokana na mwanachama aliyebwagwa kwenye kura za maoni katika chama hicho, Fred Mpendazoe kurudishwa kinyemela na kuondolewa mshindi Rachel Mashishanga. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanachama wamesema wanakihama chama hicho, huku wengine wakisema wataipigia kura CCM