[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: contentheading, width: 100%"]Mahalu awataja Mkapa, JK mahakamani Kisutu [/TD]
[TD="class: buttonheading, width: 100%, align: right"]
Send to a friend [/TD]
[/TR]
[/TABLE]
[TABLE="class: contentpaneopen"]
[TR]
[TD="class: createdate"] Friday, 05 August 2011 08:53 [/TD]
[/TR]
[TR]
[TD] 0digg
Nora Damian
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama kuwa alimtaarifu Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu hali ya ofisi ya ubalozi ilivyokuwa mbaya.
Mahalu na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, wanakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi na kuisababishia Serikali, hasara ya zaidi ya Sh2bilioni wakati wa ununuzi wa jengo la ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Rome, Italia.
Jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahalu alitumia zaidi ya saa tatu kujitetea huku baadhi ya utetezi wake ukitawaliwa na kukataliwa kwa baadhi ya nyaraka alizoziwalisha kama ushahidi.
Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Mahalu alidai kuwa mwaka 2001 wakati Mkapa alipokwenda Brussels nchini Ubelgiji, alionana naye na kumtaarifu kuhusu hali ya ofisi za ubalozi huo kuwa mbaya.
"Mwezi Mei mwaka 2001, nilitaarifiwa kuwa Mkapa atakwenda Ubelgiji na mimi nilimwomba Katibu Mkuu wangu, Balozi Kibelo aniruhusu nikamweleze juu ya matatizo yaliyokuwa kwenye ofisi yetu,"alidai Mahalu na kuongeza:
"Nilionana na Rais Mkapa na aliniambia anafahamu suala hilo kwa kuwa ofisi za ubalozi huo, zilikuwa zimefungwa kwa muda mrefu hivyo aliniambia atajitahidi kupata fedha za kujenga ama kununua jengo lenye hadhi za ofisi za ubalozi."
Mkapa ni mmoja wa mashahidi wa upande wa utetezi ambaye tayari aliwasilisha utetezi wake wa maandishi ulioandaliwa kwa njia ya kiapo kumtetea Profesa Mahalu.
Kwa mujibu wa kiapo chake kilichowasilishwa mahakamani hapo, Mkapa anadai kuwa jengo la ofisi ya ubalozi mjini Rome, lilinunuliwa wakati ambao yeye akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai kwamba ununuzi wa jengo hilo ulifanyika kwa mujibu wa sera ya Serikali ya kumiliki au kujenga ofisi za kudumu na makazi kwa mabalozi nje ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza gharama kwa Serikali.
Maelezo zaidi ya Mahalu
Mahalu alidai kuwa baada ya kuonana na Mkapa, alimjulisha Balozi Kibelo juu ya mazungumzo yao na kwamba alimuahidi kuwa atalifuatilia na kulipeleka katika bajeti ya wizara husika.
Alidai kuwa masuala yote ya fedha yalikuwa yakiletwa kwake, lakini alikuwa hayashughulikii moja kwa moja kwa sababu chini yake kulikuwa na mhasibu.
Aliendelea kudai kuwa Desemba 2001, Rais Jakaya Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alikwenda nchini Italia na kwamba aliiona hali ya ofisi za ubalozi huo zilivyokuwa.
"Rais Kikwete alikuja na aliona ofisi zilivyokuwa kwani japo alikuwa mfupi kuliko mimi, alishindwa kukaa kwenye meza iliyokuwa pale ofisini,"alidai Mahalu na kuongeza kuwa: "Aliahidi kwamba tutapata ofisi nyingine itakayokuwa na hadhi na mwonekano mzuri".
Balozi Mahalu alidai kuwa mwaka huo huo, Rais wa Zanzibar, Dk Ally Mohamed Shein ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais naye alikwenda nchini Italia na aliona ofisi za ubalozi huo zilivyokuwa.
"Dk Shein alisikitishwa sana na hali ile na aliahidi kwamba akirudi nyumbani, ataongea na viongozi kuhakikisha tunapata jengo kubwa lenye hadhi ya kibalozi,"alidai.
Alidai kuwa Juni, 2001 alipigiwa simu na Katibu Mkuu wake na kujulishwa kuwa maombi ya wizara ya kutengewa fedha za ununuzi wa jengo jijini Rome yatakubalika bungeni kwa kuwa wizarani yalikuwa yameshapitishwa.
"Niliagizwa kwamba nijipange na maafisa wangu kwa kuangalia majengo yanayofaa yenye hadhi ya kuwa ofisi za ubalozi, nami nilifanya hivyo,"alidai.
Alidai kuwa namna ofisi za ubalozi huo zilivyokuwa, alikuwa hawezi hata kuwaalika mabalozi wengine ama hata kuandaa mkutano.
Alidai kuwa ubalozi huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na kwamba vifaa vyote vya masuala ya ubalozi likiwemo jengo, vilirudishwa kwa mwenyewe.
Alidai kuwa ilibaki ofisi ndogo ya kilimo iliyokuwa katika jengo dogo.
"Nilianzia kazi kwenye ofisi ndogo iliyokuwa na square metre (mita za mraba) kati ya 88 na 100,"alidai.
Profesa Mahalu alidai katika ofisi hiyo kulikuwa na meza ya miguu mitatu, kiti cha balozi ambacho hata hivyo, kilikuwa kibovu, kochi lililokuwa limevunjika na simu.
Alidai kuwa maafisa wake wengine walikuwa wanakaa kwenye vyumba vya kulala na kwamba jiko lilikuwa linatumika kama sehemu ya mapokezi ambayo katibu muhtasi na dereva wake walikaa hapo."Choo kilikuwa kimoja tu na kilikuwa kibovu wakati mwingine kikiharibika tulikuwa tunashindwa kukaa,"alidai.
Alidai kuwa baada ya kuona hali hiyo aliamua kununua samani za ofisi kwa fedha zake mwenyewe, lakini hata hivyo hazikuingia zote kutokana na udogo wa ofisi hiyo.
Vielelezo
Mahalu pia alionyesha mahakamani hapo vielelezo viwili vya barua moja, ikiwemo ile ya shukrani aliyoandikiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wa wakati huo marehemu Abdallah Ngororo ambayo Mahakama iliikataa kwa kuwa ni nakala.
Wakili wa Serikali Ponsiano Lukosi alipinga kupokelewa kwa barua hiyo kwa madai kuwa hawana uthibitisho kama imetolewa wizarani kwa sababu ni nakala ya barua.
Katika uamuzi wake Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ilvin Mgeta, alisema kuna haja ya kuthibitisha kielelezo hicho kama barua halisi ilipotea au uletwe ushahidi wa kuthibitisha kwamba ilitolewa na ofisi ya umma.
Kielelezo kingine alichowasilisha Mahalu ni barua yake aliyomwandikia Balozi Kibelo ya Juni 4 mwaka 2001, akimshukuru kwa kushughulikia suala la ofisi za ubalozi huo ambayo ilipokelewa na mahakama kama ushahidi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 26 itakapoendelea kusikilizwa.
[/TD]
[/TR]
[/TABLE]