Hadithi ya Kakakanzi na Bibikuku
Walikuwako watoto wawili, mtu na dada yake. Majina yao Kakakanzi na Bibikuku. Mama yao akawaambia, “Watoto, msiende kutembea mwituni.”
Wakasema, “Hatuendi mama, tunacheza tu.”
Lakini katika mchezo, wakajaribu kumkamata kipepeo. Kipepeo mzuri kabisa akacheza-cheza angani, akaruka-ruka mauani.
Kila akiruka mbele wakamfuata. Polepole kipepeo akaingia mwituni. Na watoto wakamfuata. Hawaoni mwitu, wanaona kipepeo tu. Hawakumbuki maneno ya mama, wanakumbuka kipepeo tu.
Hivi wakaingia mwituni, wakaingia sana. Miti mirefu, na kichaka na giza. Walikuwa wamekwenda mbali mno. Hawamwoni mtu, hawaoni njia. Walikuwa wamepotea.
Bibikuku akaanza kulia machozi. Kakakanzi akasema, “Usilie machozi Bibikuku, tutafika tu.”
Wakaenda mbele, wakaenda wee… mpaka usiku.
Wakashikwa na usingizi, wakalala katika majani makavu.
Asubuhi yake wakainuka tena. Wakazidi kutafuta njia. Mara wakaona nyumba ndogo. Wakafurahi kuona nyumba, wakaenda kuiangalia.
Kumbe, ni nyumba ya ajabu; kuta na viambaza vyote vya mkate wa kumimina. Na sukari juu yake. Walikuwa na njaa, walianza kuondoa vipande vya kiambaza, wakala mkate mzuri mno
Walipokuwa wakila mara mlango ukafunguliwa. Akatokea kizee kungwi, mbaya sana, macho yake mabaya kama simba.
Akawaambia watoto, “Kumbe mnakula nyumba yangu. Karibuni ndani nina chakula tayari kwenu.”
Wakaingia.
Na walipokuwa ndani yule kizee akamkamata Kakakanzi. Akamfunga ndani ya sanduku yenye kidirisha. Lo! Lo! Kakakanzi sandukuni.
Na Bibikuku ikampasa kufanya kazi nzito. Kazi ya kupasua kuni na kuteka maji na kutwanga.
Kila siku kizee yule akapitisha chakula kwa mtoto kwenye dirisha la sanduku. Kila siku kizee kamwambia, “Nyosha mkono niupapase, nione kama umenenepa.”Kwa maana yule kizee kungwi alitaka kumchinja na kumla.
Lakini Bibikuku akafanya hila, akampa kaka yake mfupa wa mbuzi, naye akiambiwa na kizee, “Nyosha mkono niupapase nione kama umenenepa, hutoa mfupa wa mbuzi. Kizee Kungwi macho yake mabaya, haoni vizuri. Akapapasa mfupa, akaona amekonda, na hakutaka kumchinja bado, kwa maana amekonda.
Siku nyingi zikapita, Kakakanzi sandukuni, Bibikuku kazini. Lakini siku moja kizee kungwi akalala usingizi. Hapo Bibikuku akatwaa ufunguo wa sanduku, akaifungua.
Kakakanzi akatoka upesi, wakatoroka wote wawili. Wakarudi nyumbani. Baba yao akawapokea kwa furaha, akasema, “Kumbe, ninyi mlikuwa wapi? Sehemu gani?”
Mama yao akafurahi kabisa, naye akasema, “Ninyi watoto wangu, ni ukaidi kwenda mwituni bila ruhusa? Msifanye mara ya pili”
Wakajibu, “Mara ya pili hatuendi, hatutaki kumwona kizee kungwi.”