SEHEMU YA 09
TULIPOTOKA...
Mambo yameharibika! Tetemeko kubwa la ardhi linatokea nchini China katika Jimbo la Yunaan, watu wengi wanakufa na wengine kujeruhiwa. Miongoni mwa watu waliojeruhiwa viabaya, yupo mtoto wa bilionea mkubwa aliyeuawa na bilionea wa Kichina, Tai Peng.
Baada ya kuchukuliwa majeruhi, Richard anapelekwa hospitalini ambapo baada ya muda nesi anaingia na kumwambia kwamba kuna ndugu zake wamefika mahali hapo kuja kumuona. Anashtuka kwa kuona kwamba hana ndugu, je hao walikuwa wakina nani?
Upande wa pili, wakili Pei Pei ambaye alichukua fedha benki na bilionea, mzee Walusanga anachukuliwa yeye na familia yake na watu wasiojulikana na kupelekwa sebuleni, hapo, wanataka kujua kitu kimoja tu, mahali pesa hizo zilipokuwa.
Pei Pei hataki kusema kitu, yupo radhi kufa lakini si kuongea ukweli. Huku akiwa amegoma kabisa, mtoto wake wa kwanza anapigwa risasi, anaambiwa aseme fedha zilipo, anagoma, hivyo mtoto wake wa pili kuelekezewa bunduki. Ili kumuokoa mtoto wake, anatakiwa kusema ukweli mahali fedha zilipo.
SONGA NAYO…
Wakili Pei Pei alibaki akitetemeka, machozi yalikuwa yakimbubujika huku moyo wake ukidunda kupita kawaida. Wakati huo, watu hao walikuwa mahali hapo kwa kutaka kujua kitu kimoja tu, sehemu ambapo alikuwa amezihifadhi fedha alizozitoa benki na mzee Walusanga.
Sauti ya yule mtu ikiwa inahesabu ilisikika vilivyo masikioni mwake, tayari mtoto wake mmoja alikuwa amepigwa risasi na sasa hivi walitaka kumpiga risasi mtoto wake mwingine endao tu asingeweza kusema ukweli juu ya mahali fedha zilipokuwa.
Moyo wake haukutaka kabisa kuitaja sehemu hiyo, alibaki kimya huku akiendelea kutetemeka, moyoni alikuwa akimuomba Mungu amuepushie mbali tukio hilo la mauaji lakini kwa wakati huo, aliyasikia maombi yake yakigonga ukuta na kumrudia, hayakusikika kwa Mungu hata chembe.
“Paaaaa….” Ilisikika sauti ya risasi, akayainua macho yake na kumwangalia mtoto wake, alitaka kufahamu kama alipigwa risasi au la. Alichokiona hakuamini, mtoto wake wa pili naye alikuwa chini huku damu zikimtoka kifuani, alikuwa amepigwa risasi moja katika sehemu ambayo wala hakukuwa na nafasi ya kupona tena.
“Noooooo!!!!” alisema Pei Pei kwa hasira.
Alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, kile alichokuwa amekiona kilikuwa ni kitu kilichomuuma mno. Alibaki akilia tu, ghafla akajikuta akisimama na kumvama yule mtu aliyekuwa na bunduki kwa lengo la kutaka kupambana naye.
Kwa wakati huo hakutaka kuogopa, hakujali kama watu wale walikuwa na bunduki au la, kitu pekee alichokuwa akitaka kukifanya ni kupambana na watu hao tu. Japokuwa alikuwa na nguvu za ajabu ambazo hakujua zilitoka wapi lakini alishindwa kupambana nao, akajikuta akipigwa na kitako cha bunduki na kudondoka chini.
“Tunahitaji kujua mahali fedha zilipo,”alisema jamaa yule huku akiikoki bunduki yake, kwa wakati huu, alitaka kumuua mke wake pia.
Huo ukawa mtihani mgumu kwa Pei Pei, hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya. Tayari aliwapoteza watoto wake wawili ndani ya dakika tano tu, hiyo ikaonekana kutokutosha, pia watu hao walitaka kumuua na mke wake aliyekuwa akimpenda.
Ni kweli alijua mahali fedha zilipokuwa, alijua kila kitu lakini moyo wake haukuwa radhi kuzungumza kitu chochote kile. Yeye mwenyewe alijishangaa, moyo wake ulikuwa tayari kuipoteza familia yake lakini hakuwa radhi kusema mahali fedha zile zilipokuwa.
“Nisamehe mke wangu,” alisema Pei Pei huku akilia, alimwambia mkewe wa uchungu mkubwa moyoni mwake.
Jamaa yule hakunyamaza, aliendelea kuhesabu zaidi, alianzia kumi kushuka chini. Katika kila namba aliyokuwa akiitaja, Pei Pei hakusema kitu, alikuwa kimya huku akiendelea kulia kama mtoto. Ilipofika moja tu, mlio wa risasi ukasikika mahali pale na mke wake kudondoka chini na damu kuanza kumtoka.
Ilikuwa moja ya picha mbaya ambazo aliwahi kuziona katika maisha yake, hakuamini kwamba ndani ya kipindi kifupi angeweza kuipoteza familia yake kwa ajili ya kuzilinda fedha alizopewa ambazo hata hazikuwa zake, upendo wake mkubwa kwa usiku wa siku hiyo ukamponza na kujikuta katika maumivu makali.
Roho ya Pei Pei ilionekana kuwa ya kishujaa, watu wale hawakuamini kama mtu alikuwa tayari kuiona familia yake ikiuawa lakini si kusema mahali fedha zilipokuwa. Alichokifanya jamaa yule mara baada ya kuona Pei Pei hakusema kitu, akachukua bunduki yake, akaikoki na kumuelekezea Pei Pei.
“Zamu yako imefika. Tuambie mahali fedha zilipo,” alisema jamaa yule.
“Nipo tayari kuteswa, nipo tayari kuuawa kama ilivyouawa familia yangu, ila sitokuwa tayari kusema mahali fedha zilipo. Kama mnataka kuniua, sawa, niueni nikaungane na familia yangu huko ilipo,” alisema Pei Pei kijasiri mpaka kuwafanya watu wale kushangaa.
“Kumi…tisa…nane….saba….” alihesabu jamaa yule lakini bado Pei Pei hakutaka kuufungua mdomo wake kutaja mahali fedha zilipokuwa, alikuwa tayari kuuawa mahali hapo.
“Nyie niueni tu,” alisema Pei Pei.
Familia yake yote ilikuwa imeuawa, hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuendelea kuishi tena, angeishi vipi na wakati familia yake nzima ilikuwa imepigwa risasi, kwake, hayo yalikuwa ni zaidi ya maumivu, hakukuwa na kitu kilichomuuma duniani kama kuona familia yake ikiuawa, tena mbele ya macho yake.
Jamaa yule alipomaliza kuhesabu, akabonyeza kitufe cha bunduki, bahati nzuri kwa Pei Pei na bahati mbaya kwa mpigaji yule wa risasi, haikutoka risasi yoyote ile, risasi zote zilikuwa zimekwisha.
“Nini tena? Muue tusepe zetu,” alisema jamaa mmoja.
“Hakuna kitu.”
“Unasemaje?”
“Risasi zimekwisha.”
“Hapana. Haiwezekani.”
Alichokifanya jamaa yule ni kuifungua risasi yake, hakukuwa na risasi yoyote ile, yaani pamoja na kujiandaa kuja ndani ya nyumba hiyo, hawakuwa wamebeba risasi nyingi kitu kilichoonekana kuwa kama uzembe mkubwa.
“Yaani ni lazima afe hata iweje,” alisema jamaa yule.
“Kwa hiyo tumuue vipi?”
“Tumechome moto ndani ya nyumba hii.”
“Mmmh!”
“Haina jinsi, tufanye hivyo,” alisema jamaa yule.
Huo ndiyo mpango waliokuwa wameafikia kwamba ilikuwa ni lazima Pei Pei achomwe moto ndani ya nyumba yake. Walichokifanya ni kumfunga kamba mikono yake na kisha kuelekea nje ambapo wakachukua dumu la mafuta ya petroli lililokuwa garini na kuanza kuimwagia nyumba ile kuanzia ndani mpaka nje.
“Piga kiberiti,” alisema jamaa mmoja na mwingine kukiwasha kiberiti, kilichofuata, ni mlipuko kubwa na nyumba ile kuanza kuteketezwa kwa moto.
****
Bado Richard alikuwa akitetemeka kitandani pale, nesi aliyeondoka ambaye alisema kwamba kulikuwa na ndugu zake waliokuja kumuona alimtisha, kijasho chembamba kiliendelea kumtoka, huku akiwa kwenye hali hiyo, mara mlango ukafunguliwa.
Mtu aliyeingia, alikuwa nesi mwingine, alipomuona tu akiwa amefumbua macho yake, tabasamu kubwa likautawala uso wake, akaanza kumsogelea na kuanza kuyapima mapigo yake ya moyo.
“Moyo wako unakwenda kasi sana, kuna nini?” aliuliza nesi yule.
“Nataka kuondoka kurudi nyumbani, tena sasa hivi,” alisema Richard huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea.
“Uondoke kurudi nyumbani! Hapana, subiri kwanza bado haujawa sawa,” alisema nesi yule huku akiiweka mashine ile ya kusikilizia mapigo ya moyo shingoni mwake.
Richard hakutaka kuongea kitu chochote, ili asifikiriwe vibaya, akajifanya kuwa mpole. Nesi yule alipomaliza kazi zake ndani ya chumba hicho kikubwa, akaondoka zake.
Richard hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba hicho, alichokifanya ni kuchomoa sindano zote za dripu alizokuwa amechomwa na kisha kutoka itandani pale. Kitu pekee kilichokuja kichwani mwake wakati huo ni kuondoka kuelekea mitaani na kwenda kumtafuta rafiki yake, Shu Yan.
Hatua zake kuufuata mlango wa nyuma zilikuwa ni za harakaharaka, hakutaka kutembea taratibu kwa kuhisi kwamba watu wale waliojitambulisha kama ndugu zao wangefika na kumchukua kitu ambacho hakutaka kitokee.
Huku akiwa ameukaribia ule mlango wa nyuma, mlango wa mbele ukafunguliwa, alipogeuka nyuma na kuangalia, nesi yule aliingia na wanaume watatu, kwa jinsi walivyoonekana, walionekana kuwa watu hatari.
“Yupo wapi?” aliuliza jamaa mmoja kwa sauti kubwa, hakujali kama sehemu waliyokuwepo ilikuwa ni hospitalini na wagonjwa walikuwa wengi.
“Alikuwa hapa,” alijibu nesi yule huku akikishika kitanda alichokuwa amelazwa Richard.
“Yupo wapi?” alirudia swali lile, wakati huu akaitoa bunduki yake, nesi akashtuka zaidi.
“Alikuwa hapa,” alijibu nesi yule huku akitetemeka.
Wakiwa bado wanaangalia huku na kule, kwa mbali wakamuona Richard, walimfahamu vilivyo, alikuwa kijana mwenye ngozi nyeusi, walipomuona tu, hapohapo wakaanza kumfuata, alichokifanya Richard ni kuufungua mlango ule wa nyuma na kisha kuanza kukimbia, watu wale wakaanza kumkimbiza, wagonjwa na nesi, wote wakapigwa na butwaa.
Tayari hatari ilikuwa mbele yake, alikuwa akikimbia kwa kasi huku akifungua mlango huu na kuufunga, aliufungua huu na kuufunga. Japokuwa alikuwa akijisikia uchovu mwilini mwake lakini hakutaka kujali, aliendelea kupiga hatua kwa kasi, alipofika nje, akaongeza mwendo na kukimbia zaidi.
“Simamaaaaaa,” ilisikika sauti ya mlinzi mmoja wa getini, alikuwa ameshika bunduki, alionekana kuwa na wasiwasi na Richard.
Wakati anasema hayo, walinzi wenzake wawili nao wakatokea, kama alivyokuwa amefanya mwenzao, nao wakachukua bunduki zao na kumnyooshea Richard ambaye alibaki akitetemeka.
“Wanakuja kuniua,” alisema Richard huku akitetemeka.
“Nani anakuja kukuua?” aliuliza mlinzi mmoja.
Hata kabla Richard hakujibu swali hilo, mlango ule ukafunguliwa na wanaume watatu waliokuwa na bunduki wakatokea. Kwanza kitedo cha kumuona Richard amesimama mbele yao kama hatua thelathini kiliwashangaza, kitu pekee kilichowashtua, kilikuwa ni uwepo wa walinzi waliokuwa wameshika bunduki na kumnyooshea Richard.
Ghafla, wakaona bunduki za walinzi wale zikianza kuwaelekezea wao, walichokifanya, ni kuanza kurushiana risasi mahali hapo. Ilikuwa ni lazima kufanya hivyo, kumpata Richard halikuwa jambo jepesi, walihitajika kumwaga damu kwanza.
“Paaaaa….paaaaa….paaaaa” milio ya risasi ikaanza kusikika mahali hapo. Eneo la hospitalini likaonekana kuwa uwanja wa vita, kwa jinsi hali ilivyoonekana, ilikuwa ni sawa na filamu za kina Anord na Rambo.
Je nini kitaendelea?
Je Richard atakamatwa?
Na je wakili Pei Pei atauawa kama familia yake?
Je fedha zipo wapi?
Je Richard atazipata fedha hizo?
Itaendelea.